MSIBA! Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Juma Abdallah Juma (51), mkazi wa Bunju ‘B’ jijini Dar anadaiwa kufia kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar huku ndugu wakiibuka na madai kuwa, alipigwa na polisi wa kituo alichowekwa mahabusu, Uwazi lilifuatilia.
Akizungumza na gazeti hili, dada wa marehemu Juma, Mwanaidi Abdallah alisema, awali, marehemu na ndugu zake wawili, Muhisan (42) na Baraka (30) walikamatwa Juni 16, mwaka huu na askari wa vituo vya polisi vya Wazo, Boko na Tegeta kwa madai wanahusika na wizi wa magari matatu.
Ndugu huyo alisema, askari hao waliyataja magari hayo kuwa ni Toyota Prado (thamani ya Sh. milioni 30), Mistubishi (Sh. milioni 30) na BMW (Sh. milioni 65).
Iliendelea kudaiwa kuwa, askari hao waliwachukua na kuwapeleka vituo tofauti ambapo, Muhisan alipelekwa Kituo cha Tegeta, marehemu Juma, Wazo na Baraka alisukumizwa Boko.
“Baada ya kusikia hivyo, tulikwenda Tegeta, tulimkuta Muhisan, akatuambia Juma yupo Kituo cha Polisi Wazo lakini hali yake si nzuri (hakufafanua kivipi). Lakini baadaye wote walihamishiwa Kituo cha Kawe. Tulipofika huko pia tukazuiwa kumuona, polisi wakasema ndugu yetu ni jambazi.
CHANZO:GPL
“Tulihangaika sana. Baada ya wiki moja tukamuona tena kwa kuomba kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wazo. Kusema kweli hali yake ilikuwa inasikitisha. Alikuja kutusalimia akiwa anatambaa, amevimba uso, mikono, miguu yote na mmoja ulikuwa umepasuka.
“Tuliomba apelekwe hospitali kufanyiwa uchunguzi tujue anasumbuliwa na nini, tukaambiwa tutoe shilingi 15,000 nauli ya Bajaj.
“Siku ya pili tulipokwenda tukakuta amefungwa bandeji kwenye miguu, wakasema tumnunulie dawa ya kupunguza maumivu, tukafanya hivyo.“Mke wa Muhisan alidamka kupeleka chai kwa mumewe, kufika akaambiwa ndugu zenu wote leo wamepelekwa Mahakama ya Kinondoni.
“Tulipopata taarifa hizo... tulijipanga na wadhamini tukaenda mahakamani. Kufika tukakuta ndiyo wameitwa na wakati huo Juma amebebwa na Muhisan na Baraka hawezi kutembea sawasawa. Walisomewa mashitaka yao kuwa waliiba magari kwenye Yadi ya Mazrui iliyopo Kijitonyama (Dar) wakiwa wametumia silaha aina ya bastola.
“Washitakiwa wakaandikiwa kwenda Gereza la Segerea lakini wakaambiwa gari limejaa, ikabidi wapelekwe Kituo cha Polisi Oysterbay kukaa kwa muda.
“Jumanne ya wiki iliyopita, tukapeleka chakula asubuhi, Juma hakuweza kula. Tulipokwenda baadaye, Muhisan akasema hali ya Juma ni mbaya. Tukafanya mpango wa gari la magereza akatibiwe lakini kabla gari halijafika, polisi walikwenda kumchukua kwa kumbeba kwenye machela, wakamuweka kwenye gari, kabla hawajaondoka, Juma alikata roho.
“Sisi tulitoka pale kwenda Hospitali ya Mwananyamala na wao walielekea huko. Walipofika wakaufikisha mwili moja kwa moja mochwari,” alisema Mwanaidi kwa huzuni.
Ili kujua ukweli wa mambo yota hayo, Uwazi lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camillius Wambura ambaye alikiri kuwa na taarifa za kifo cha Juma, lakini akasema:
“Juma aliletwa hapa baada ya kukosa nafasi kwenye gari alilokuwa anatakiwa kupanda kwenda Segerea. Habari za kupigwa au kutokupigwa zitatafsiriwa baada ya uchunguzi kufanyika kwa sababu mpaka sasa mwili wake bado upo mochwari kwa uchunguzi (kesho).
“Mtuhumiwa alifariki dunia baada ya kuugua akiwa kituo cha polisi kabla ya kupelekwa hospitali kupata matibabu ya ugonjwa wake.”
No comments:
Post a Comment