Tuesday, 2 June 2015

WAKIMBIZI WA BURUNDI WAONGEZEKA NYARUGUSU

Idadi ya wakimbizi waliopo katika kambi ya Nyarugusu, Kigoma imezidi kuongezeka na kufikia 51,095 huku 32 wakilazwa kutokana na kuugua ugonjwa wa kipindupindu.

Wagonjwa hao ni waliolazwa katika kambi hiyo pamoja na wale waliopo uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, alisema vifo vya wagonjwa wa kipindupindu havijatokea tena katika siku tatu za hivi karibuni baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa.
“Kutokana na ushirikiano kati ya mashirika ya kimataifa pamoja na madaktari wasio na mipaka, Wizara ya Afya tumedhibiti ugonjwa na idadi ya vifo kupungua,” alisema.
Alisema katika eneo la kituo cha uhamiaji cha Manyovu kuna raia 208 ambao wameingia nchini kupitia barabara kuu ya Burundi-Tanzania wakisubiri kupelekwa katika kambi ya Nyarugusu kwa ajili ya usajili.
Idadi ya raia wanaoingia nchini wakitokea Burundi imezidi kuongezeka kutokana na raia hao kukimbia machafuko na vurugu kupinga msimamo wa Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea nafasi ya urais kwa muhula wa tatu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!