WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Profesa Mark Mwandosya (65) na Mbunge wa Afrika Mashariki, Charles Makongoro Nyerere na Balozi mstaafu Ali Karume, jana waliungana na makada wengine wa CCM, kutangaza nia ya kuwania urais wa Tanzania, kwa lengo la kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwandosya, msomi mahiri aliyefundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1974 na 1987 na kurejea chuoni hapo tena mwaka 1994 hadi 2000 alipoingia bungeni na kupewa kazi ya kuziongoza wizara za Maji, Mawasiliano na Uchukuzi na sasa Kazi Maalumu, Ikulu, alitangaza nia yake akiwa viwanja vya Ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini hapa.
Viwanja hivyo vilivyopo eneo la Soko Matola ndivyo vilivyotumiwa na mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere kuendeshea mikutano yake wakati wa harakati za kutafuta Uhuru wa Tanganyika.
Makongoro, mmoja wa watoto wa Mwalimu Nyerere, alitangaza nia yake kijijini kwao Butiama, wilayani Butiama mkoani Mara akiwa na kundi la wafuasi.
Makongoro mwenyewe baadaye aliwashukuru kwa kumuunga mkono, licha ya kuwa hakuwagharamia nauli, chakula wala malazi. “Nawashukuru wote waliokuja kwa kujilipia nauli, chakula na malazi,” alisema Makongoro.
Na huko Zanzibar, Balozi Karume alitangaza nia na kuahidi kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, akisema ameipaisha mno kimataifa Tanzania.
Mwandosya na nyayo za Nyerere
Akihutubia mamia ya wananchi waliofika kwenye mkutano wake wa kutangaza nia, wakiwemo viongozi wa jadi na wa vyama upianzani, Profesa Mwandosya alisema yeye si bingwa wa kujisifia, kama wanavyofanya wengine.
Alisema bado kuna haja ya kuendeleza mikakati 10 iliyopo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ili kujenga uchumi imara wa nchi, kama ilivyoasisiwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
“Wakati umekifa wa kudhamiria ifikapo mwaka 2030 Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati, lakini iwe ikiziongoza nchi nyingine zilizopo kwenye kundi hilo na ifikapo mwaka 2050 nchi yetu iwe imetoka katika kundi la dunia ya tatu na kuingia katika kundi la nchi za dunia ya kwanza. Hili linawezekana lakini ni vipi tutafanikiwa, hilo ndilo swali la kujiuliza,” alisema.
“Lakini lazima tuhakikishe tunaondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji wa ndani na nje. Wengi tumekuwa tukifikiri uwekezaji lazima watu watoke na mamilioni nje ya nchi, tunapaswa kuhamasisha uwekezaji wa ndani ili fedha zetu zibaki hapa ndani,” alifafanua Mwandosya, aliyechangia Sh milioni 10 kwa ajili ya kuchukulia fomu, licha ya kuwa CCM inatoza Sh milioni moja kwa fomu ya urais.
Akizungumzia vipaumbele vyake, Mwandosya alisema katika elimu angependa kuona elimu ya msingi inakuwa ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Pia, alisisitiza umuhimu wa wanawake kupewa kipaumbele katika kupewa elimu. Kwa upande wa sekta ya afya, alisema kwa muda mrefu taifa limejikita katika kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya matibabu, badala ya kuwekeza kwenye mikakati ya kinga, jambo ambalo litawezesha serikali kuepukana na gharama kubwa.
Alisema ni wakati kwa serikali kuhakikisha kila mdau wa sekta ya afya, anawajibika ipasavyo kwa kuiwezesha jamii kujikinga na maradhi badala ya kuhangaikia matokeo ya maradhi.
Kwa upande wa ajira kwa vijana, alisema bado kuna changamoto, lakini hii ni kutokana na vijana wengi kuwa na mawazo ya kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri.
Karume avutiwa na Rais Kikwete
Balozi mstaafu Ali Karume amesema akifanikiwa kushika hatamu ya kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha anayaendeleza yote yaliyofanywa na Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete, ambayo yameleta mabadiliko makubwa nchini, kiasi ya Tanzania kusifiwa taifa la amani.
Alisema hayo jana katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati, Dunga mkoa wa Kusini Unguja, alipokuwa anatangaza dhamira yake ya kuwania Urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Alisema sifa ambazo Tanzania inazipata nje ya nchi, kwa kiasi kikubwa zimeletwa na Rais Kikwete, ambaye umahiri wake mkubwa katika siasa za kimataifa umeirudishia hadhi Tanzania mbele ya washirika wa maendeleo.
Balozi huyo alisema akipitishwa na chama chake, kuwania urais na kama akibahatika kuwa kiongozi wa Tanzania, atahakikisha vita dhidi ya rushwa inaendelezwa kwa taasisi zilizopo kujengewa uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Alifafanua kuwa rushwa bado ni tatizo licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa, ikiwemo kuundwa kwa taasisi za kupambana na tatizo hilo. Alisema juhudi zinahitajika, ikiwemo kuipa mamlaka zaidi ya utendaji na uwezo wa kufanya kazi.
Aidha, Karume aliyejaribu pia kuwania urais mwaka 2010, lakini hakupenya katika mchakato wa ngazi ya chama, alitaja baadhi ya vipaumbele ambavyo atahakikisha vinaimarishwa ni sekta ya kilimo, ikiwemo kuwawezesha wakulima kulima na kuuza mazao yao huku viwanda vya kusindika vyakula vikijengwa.
Makongoro Butiama
Akiwa katikati ya umati mkubwa wa watu katika kitongoji cha Mwitongo, Butiama, Makongoro alitangaza nia na kusema hawezi kusema kwamba atawafanyia nini Watanzania ilhali Ilani ya chama hicho haijapitishwa na vikao halali vya chama.
Alisema Ilani ya chama ndiyo inayoongoza kila kitu, ambapo mgombea yeyote wakati anajinadi atakuwa anatoa ahadi zake kutokana na maelekezo yaliyomo ndani ya Ilani hiyo.
Aliwashangaa wanaCCM wenzake ambao wamekwishatangaza nia ya kuwania urais na kutoa ahadi nyingi, ilhali chama hakijapitisha ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa sababu CCM inaongozwa kwa vikao na kufuata katiba na taratibu zake.
Aidha, akizungumzia kilichomfanya akihame chama hicho na kuhamia NCCR-Mageuzi na kuingia bungeni mwaka 1995 kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani, alisema alishauriwa na waasisi wa CCM wakati akiwania ubunge katika Jimbo la Arusha wakati huo.
“Mimi na mke wangu tulimfuata Mwalimu Nyerere na nikamwambia jinsi ninavyotaka kukihama chama hicho na jinsi nilivyoshauriwa na waasisi hao, alinikubalia na kunipa baraka zote,” alisema baadaye aliamua kurejea CCM na kuongeza kuwa CCM ni chama kizuri chenye Katiba nzuri na utaratibu wake ni mzuri, lakini katiba hiyo pamoja na taratibu zake imekuwa ikikiukwa kwa makusudi na baadhi ya wanachama ambao wengi wao nimatajiri wanaotumia fedha zao kukigawa chama.
Alidai matajiri hao fedha zao nyingi ni chafu na wamezichota serikalini wakiwa katika chama hicho na kwamba yeye hakatai watu kuwa matajiri, lakini wawe na utajiri wa halali.
Aliongeza kuwa, viongozi hao ambao baadhi yao tayari wamekwishatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, wamekwishakigawa chama chao.
“Watoke watuachie chama chetu, wanataka kukipeleka wapi watoke watuachie chama chetu,” alisema na kuongeza kuwa akiteuliwa na chama chake na baadaye kuwa Rais wa nchi na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, atahakikisha chama kinarudi kwenye misingi yake aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Alisema atawabana wabadhirifu wote wa mali za umma ambao wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya, kwani wanakiuka misingi ya chama hicho kwa makusudi na amewaita viongozi hao kuwa ni vibaka.
Alisema yeye, licha ya kutokuwa na pesa za kutoa rushwa na pia siyo mtoa rushwa na asiye na makundi, anaamini atapatiwa nafasi hiyo kwa sababu anazo sifa za kutosha na pia ni mwadilifu na anafuata misingi ya katibaya chama hicho.
Aidha, alisema Rais Kikwete anaijali sana familia ya Mwalimu Nyerere, hivyo ni mtu anayejali watu. Kabla ya kutangaza nia, wazee wa kabila la Wazanaki wakiongozwa na Chifu Wanzagi walisema imefika hatua sasa Mwalimu Nyerere atambuliwe na kukumbukwa kwa kuenziwa kwa mtoto wake kupewa nafasi hiyo ya Urais kama ilivyokuwa kwa watoto wa Hayati Abeid Karume (Amani Karume wa Zanzibar) na Jommo Kenyatta ambaye mtoto wake, Uhuru ndiye rais wa sasa wa Kenya.
Leo ni zamu ya Prof Sospeter Muhongo na Frederick Sumaye kutangaza nia kuwania urais.
Imeandikwa na Joachim Nyambo (Mbeya), Ahmed Makongo (Butiama) na Khatibu Suleiman (Zanzibar).
No comments:
Post a Comment