Friday, 12 June 2015

UMASIKINI VIJIJINI WAPUNGUA KWA ASILIMIA 22.7



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu (pichani), amesema umaskini vijijini umepungua kutoka asilimia 22.7 mwaka 2007 hadi asilimia 21.7, mwaka 2011/12.



 
Akiwasilisha jana bungeni taarifa ya hali ya uchumi 2014 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16, alisema kwa takwimu hizo umaskini vijijini umepungua kwa asilimia 6.1 katika kipindi cha miaka mitano, ikilinganishwa na asilimia 1.4 kipindi cha miaka 15 kati ya mwaka 1991/92 mpaka 2007. 
 
“Mwenendo huu unaashiria ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa (wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka), kwa kipindi cha miongo miwili na umezaa  matunda ya kupunguza umaskini mwa kiasi kikubwa na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi,” alibainisha
Waziri Nagu alisema Jiji la Dar es Salaam umaskini umepungua kutoka asilimia 14.1 mwaka 2007 hadi asilimia 4 mwaka 2011/12.
 
Alisema kwa mujibu wa tafiti za mapato na matumizi ya kaya, umaskini umepungua kwa asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2011/12.
 
Aidha, alisema umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 11.3 mwaka 2007 hadi 9.7 mwaka 2011/12.
 
DENI LA TAIFA
Waziri Nagu alisema hadi Machi, mwaka huu, deni la taifa lilifika dola za Kimarekani bilioni 19.48 Sh. (trilioni 35.01), ikilinganishwa dola za Kimarekani 18.67 (Sh. trilioni 30.6) Machi, 2014.
 
“Sababu za ongezeko hili ni riba na madeni mapya yaliyokopwa na serikali kwa ajili ya kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan ya usafirishaji na nishati,” alisema.
 
PATO LA TAIFA
Alisema mwaka 2004 pato la Taifa Tanzania Bara lilikuwa kwa wastani wa asilimia 7.0 ikilinganishwa na asilimia 7.3 mwaka 2013, na kwamba kwa bei za mwaka husika zilikuwa Sh. trilioni 79.4 sawa wastani wa pato la kila mtu Sh. 1, 724,416 dola za Kimarekani 1,038.
 
Alifafanua kuwa hiyo inalinganishwa na Sh. trilioni 70.9 mwaka 2013 sawa na wastani wa pato la kila mtu la Sh. 1,582,797 sawa na dola za Kimarekani 948 na kwamba jitihada kufikia lengo lililowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo la Dola za Kimarekani 3,000 ifikapo 2025.
 
AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI
Alisema akiba ya fedha za kigeni ilipungua kutoka Dola za Kimarekani milioni 4,676.2 kwa kipindi kinachoishia Desemba 2013 hadi dola za Kimarekani milioni 4,383.6 Desemba 2014.
 
“Hadi Machi mwaka huu, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola milioni 4,064.8 sawa na uwezo wa kuagiza bidhaa nje kwa kipindi cha miezi minne, hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka mahitaji ya uagizajj bidhaa kutoka nje ya nchi,” alibainisha.
 
MFUMUKO WA BEI
Alisema hadi Machi mwaka huu, wastani wa mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 4.3 na kupanda kidogo hadi 4.5 Aprili mwaka huu.
 
THAMANI YA SHILINGI
Dk. Nagu alisema hadi Machi, mwaka huu, dola moja ilibadilishwa kwa wastani wa Sh. 1,786.3, ikilinganishwa na Sh. 1,598.6 mwaka 2004.
 
MAUZO YA BIDHAA NJE
Waziri huyo alisema urari wa biashara na huduma mwaka 2014 ulikuwa na nakisi ya dola za Kimaekani milioni 4,853.9.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!