Friday 19 June 2015

SHILINGI INAACHWA IPOROMOKE MPAKA WAPI?



Mkutano wa Bunge la Bajeti unafikia ukingoni wiki ijayo. Mengi yamezungumzwa na kutolewa ufafanuzi. Wizara za serikali zimewasilisha makadirio ya matumizi yake na bajeti kuu ya Sh. trilioni 22.4 imesomwa kujadiliwa na hakuna shaka kuwa itapitishwa.



 
Ukisoma kwa makini kile kilichowasilishwa na Waziri wa Fedha bungeni wiki iliyopita Juni 11, mwaka huu, kuna maswali mengi yanaulizwa kama kweli malengo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 yatatimia. Kubwa linalosumbua wengi ni kuzidi kuporomoka kwa thamani ya sarafu (Shilingi) ya Tanzania.
 
Kuna hatua kadhaa za kibajeti zilitajwa na Waziri wa Fedha kwamba zinalenga kuimarisha Shilingi. Miongoni mwake ni kuongeza kodi kwa baadhi ya bidhaa kutoka nje kama sukari ya viwandani; mchele na mabomba ya plastiki.
 
Aprili 28, mwaka huu katika safu hii tuliandika tahariri katika ukurasa huu tukisema ‘Tunataka hatua za kuiokoa Shilingi dhidi ya Dola sasa’ tulisema hayo baada ya kueleza kuwa ilikuwa ni dhahiri kuwa sarafu ya Tanzania siku baada ya siku ilikuwa inazidi kuelemewa na thamani ya Dola ya Marekani. Tulisema mporomoka huo wa Shilingi ulikuwa unatisha na unazidisha makali ya maisha kwa wananchi.
 
Kulingana na taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu soko la kubadili fedha za kigeni katika benki nchini (IFEM) hadi Aprili 26, mwaka huu Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 1,824.02. Tulisema wakati ule kuwa hicho kilikuwa ni kiwango cha juu kabisa cha kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania tangu mwaka 2004 kilipokuwa cha chini zaidi cha Sh. 1,014.30 kwa Dola.
 
Leo hii, takribani miezi miwili kasi ya kuporomoka imekuwa ni ya kutisha zaidi. Kwa mujibu wa BoT viwango vya IFEM Shilingi imepoteza nguvu zaidi na sasa imefikia Sh. 2,100 kwa Dola ya Marekani. Hali ni mbaya. Tunajua kuwa wapo watu ambao wamepuuza rai hii wakijikita kwenye dhana kwamba hizi ni nyakati za mfumo wa uchumi wa soko huria ambao huendeshwa kwa nguvu za soko, ugavi na mahitaji, lakini wamekwepa kutilia maanani ukweli kwamba kwa hali ya uchumi wa nchi hii kuiacha Shilingi kusukwa sukwa tu na nguvu hizo, kuna hatari kubwa ya kiuchumi kwa taifa hili. Tunasema haya kwa sababu pamoja na serikali kuwa na mipango yake ya maendeleo inayoanishwa kwenye kila bajeti ya kila mwaka, utekelezaji wake unategemea sana mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.
 
Ni rai yetu tena leo kwamba kama taifa ni fedheha na kujidanganya kusema eti hatuwezi kufanya lolote juu ya kuendelea kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania. Pamoja na kuukumbatia mfumo wa uchumi wa soko huria, ni kujidanganya kuiacha Shilingi ijiimarishe yenyewe bila kuwako kwa maamuzi ya kisera na kisheria ya kuijengea wigo.
 
Mathalan, wapo watu wamejenga hoja zenye nguvu kwamba kwa kiwango kikubwa tabia ya baadhi ya watoa huduma na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupanga bei zao kwa Dola za Marekani, hakika kunaongeza shinikizo kwa sarafu ya nchi hii bila sababu.
 
Kubwa zaidi kumekuwa na uagizaji wa vitu kutoka nje ambavyo vinahitaji Dola ya Marekani wakati kimsingi vitu hivyo havina maana, tija na wala havisaidii juhudi za taifa hili kupambana na umasikini mbali tu ya kuongeza mahitaji makubwa ya Dola na hivyo kuzidi kuikandamiza Shilingi kila uchao.
 
Mara kadhaa tumehoji kwenye safu hii kwamba kama Taifa kweli kuna uhalali wowote wenye tija kuangiza nje ya nchini bidhaa kama samani ambazo ni kama maboksi tu?; mapambo na wanasesere wa plastiki?; vifaa chakavu vya nyumbani kama vyombo, nguo kuukuu (mitumba) kwa kutumia Dola za Marekani?
 
Kwa bahati mbaya ulimbukeni wa kuagiza vitu kutoka nje umeingia hata kwenye vyakula ambavyo vimejaa kiasi cha kuozea katika masoko yetu. Siku hizi maduka makubwa ya bidhaa za chakula yamejaa mbogamboga, matunda na hata nyama ya ng’ombe na kuku; mayai na unga na bidhaa nyingine za vyakula kutoka nje.
 
Tunajliuza tena leo, hivi kweli serikali au mamlaka nyingine za usimamizi zinaona hatari inayotunyemelea kama taifa kwa kudekeza udhaifu huu wa kuhalalisha uhuru huu usiokuwa na tija wala ukombozi wowote dhidi ya umasikini wa nchi hii. Hivi ni nani hasa anajali juu ya kuendelea kuporomoka kwa thamani ya Shilingi?
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...



aziz bilalYesterday 23:12


1
Reply

Mpaka siku Jesus atakapokuja tena duniani.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!