Friday 19 June 2015

PUNGUZO LA ADA ZA ARDHI ISITUMIKE KUNUFAISHA MATAJIRI WACHACHE

Wananchi wa eneo la Kigamboni wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akizungumza na wananchi hao kuhusu uamuzi wa serikali kuwaruhusu kuwa sehemu ya uendelezaji wa Mji mpya wa Kigamboni katika mkutano uliofanyika viwanja vya Chuo cha Mwalimu Nyerere.

WIKI iliyopita Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliwasilisha bajeti yake ya mwaka 2015/16 ambapo wabunge wengi wakiwamo wa kambi ya upinzani waliipitisha kwa shangwe.


Wabunge wengi walifurahia bajeti hiyo kwa kuwa ilikuwa na mambo mengi mazuri ikiwa ni pamoja na punguzo la kodi, ada na malipo mbalimbali yanayohusiana na ardhi.
Wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema sababu ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali ni kujenga mazingira rafiki zaidi kwa wananchi katika matumizi ya ardhi.
Lukuvi amesema, kuanza Julai Mosi mwaka huu, kodi ya pango la ardhi imepungua kwa wastani wa asilimia 30 na kwamba viwango vingine vinavyomgusa mwananchi wa kawaida vimepungua kwa asilimia 50 au zaidi.
Akiorodhesha namna kodi zilivyopunguzwa, Lukuvi amesema kodi ya kupima mashamba imepunguzwa kwa asilimia 60 kutoka Sh 1,000 hadi Sh 400 na ile ya mashamba ya biashara imepunguzwa kwa asilimia 50 kutoka Sh 10,000 hadi Sh 5,000 kwa ekari.
Anasema ada ya upimaji ardhi imepungua kutoka Sh 800,000 hadi Sh 300,000 kwa hekta, sawa na asilimia 62.5 na kwamba tozo ya nyaraka za tahadhari na vizuizi imepunguzwa kutoka Sh 120,000 hadi Sh 40,000.
Gharama pia zimepunguzwa kwenye ubadilishaji wa majina, usajili wa nyaraka na nakala za hukumu kutoka kwenye mabaraza ya ardhi.
Pia ada ya maombi ya kumiliki ardhi imepunguzwa kwa asilimia 75 kutoka Sh 80,000 hadi Sh 20,000 na ada ya maandalizi ya hati imepunguzwa kwa asilimia 68 kutoka Sh 160,000 hadi Sh 50,000.
Kwa upande wa viwango vya tozo ya mbele (premium) Waziri alisema itapungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi.
Ingawa serikali imefanya vyema kupunguza ada za ardhi, zipo hisia kuwa punguza hili litawanufaisha zaidi wawekezaji na watu wachache wanaofanya biashara ya kununua na kuuza ardhi kuliko kunufaisha wananchi wa kawaida kwa kuwa wengi wao hawajui taratibu za kupima viwanja na kutafuta hati.
Wasiwasi ni kwamba matajiri wenye uwezo wa kununua ardhi kwa wakulima ndio watafaidika zaidi na punguzo hilo la ada za ardhi kisha kuuza ardhi hiyo kwa bei ya juu hivyo kuendelea kuwabebesha wananchi wa kawaida msalaba wa gharama kubwa za kununua viwanja na mashamba.
Wasiwasi huo unatokana na ukweli kwamba siku hizi kuna makampuni mengi yanayokwenda kwa wakulima na kununua kwa bei ya chini ardhi isiyopimwa kisha yanaingia gharama ya maombi ya kumiliki ardhi, kupima viwanja, kulipia hati na kisha kuwauzia wananchi viwanja hivyo kwa bei kubwa.
Bila shaka wenye makampuni yanayojihusisha na biashara ya kununua mashamba na kuuza viwanja wanachekelea zaidi punguzo hilo la tozo katika ardhi kwa kuwa wanajua watatumia bei ya chini iliyotolewa na serikali kupata mashamba na viwanja kisha kuziuza kwa kutumia bei ya makampuni binafsi ambayo ipo juu.
Tumeshuhudia makampuni haya yanayonunua viwanja kwa wakulima na kupima na kisha kuziuza kwa bei ya juu ambapo kiwanja kidogo (high density) huuzwa kwa mwananchi wa kawaida kwa bei kubwa na kumshawishi alipe kwa awamu hadi atakapomaliza deni.
Kwa vile kodi ya kupima kiwanja gharama za kupata hati ilikuwa juu, makampuni haya yalikuwa yakifanya ‘janja’ ya kumwambia anayetaka kiwanja kulipia kiasi fulani cha fedha kama utangulizi kisha yanatumia fedha hizo upimaji wa viwanja na ada ya kupata hati.
Ili kuziba mwanya wa kunufaisha makampuni na watu wachache wenye fedha, Serikali inapaswa kuweka bayana utaratibu na bei za kuuza na kununua viwanja kulingana na eneo husika na kuyabana makampuni yanayonunua mashamba kisha kupima viwanja na kuviuza kwa bei ya juu.
Ni kweli, serikali ina nia njema na wananchi wa kawaida nikiwemo mtu wa kipato cha chini lakini isipochukua hatua za kudhibiti mianya ya rushwa na dhuluma, punguzo hilo la ada za ardhi litawanufaisha watu wachache wenye fedha na kuwaumiza wananchi wengi.
Punguzo hilo la ada lingetolewa kwa wananchi wa kawaida na kuyabana makampuni makubwa na wawekezaji wa kigeni kuendelea kutumia viwango vya awali ili kulipatia taifa pato na kuondoa uwezekano wa watu wachache kutumia punguzo hilo kwa manufaa yao endapo wataachiwa mwanya wa kuwauzia wananchi ardhi kwa bei kubwa.
Wakati serikali inalenga kumpunguzia mwananchi wa kawaida tozo mbalimbali za ardhi ili kumpa ahueni, na wakati ikiamini kwamba kwa kufanya hivyo kodi zitakuwa rafiki na hivyo wananchi wengi watajitokeza kulipa kwa hiari, lakini ninachoona ni kwamba watakaofaidika zaidi ni wafanyabiashara.
Mbali na punguzo la kodi Waziri Lukuvi anapongezwa kwa kushughulikia migogoro mbalimbali ya ardhi ikiwa ni pamoja na kusaidia kuwarejeshea wananchi shamba la Utuamaini lililoko Halmashauri ya Mafya mkoani Pwani. Pia Lukuvi anapongezwa kwa kusimamia usuluhishi wa mgogoro wa shamba la Malonje lililoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mashamba haya yalikuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu na wananchi wasio na ardhi. Inadaiwa kuwa mgogoro wa shamba la Malonje linalomilikiwa na Kanisa la Efatha linaloongozwa na Nabii Josephat Mwingira, ulisababisha baadhi ya wanavijiji kupata majeraha ya kudumu na uhasama mkubwa kati ya kanisa hilo na wananchi .
Waziri Lukuvi amefanikiwa kumaliza mgogoro baina ya kiwanda cha saruji cha Wazo na wakazi walio jirani na kiwanda hicho wa Cha Simba. Lingine zuri alilofanya Lukuvi na anastahili kupongezwa ni kumaliza sintofahamu ya mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa kuweka utaratibu shirikishi unaopata fursa wakazi wa Kigamboni kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa mpango mpya wa maendeleo ya jiji.
Amebainisha njia tatu zitakazotumika katika utaratibu wa kuendelea eneo hilo. Mosi, mwananchi mwenyewe kundeleza eneo lake kwa kuzingatia ramani na mpango uliopo (master plan). Pili, mwananchi kulipwa fidia au kuuza eneo lake kwa mwekezaji kwa hiari yake huku akizingatia bei ya soko na njia ya tatu ni mwananchi kuingia ubia na mwekezaji kwa kutumia ardhi yake kama mtaji.
Kingine kizuri kilichomo kwenye mkakati wa Wizara hiyo, ni kwamba katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai 1, ardhi ya wananchi haitotwaliwa na mamlaka yoyote kabla ya kuwepo kwa uthibitisho wa fidia. Kwamba uthibitisho wa kulipa fidia ni lazima pia uwasilishwe kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kabla ya utwaaji wa ardhi ya mwananchi.
Waziri alisema zoezi la fidia lazima lizingatie pia ushirikishwaji wa kutosha wa wadau wote muhimu, wakiwemo viongozi wa kata, serikali za mitaa au vijiji na wananchi.
Lakini pamoja na hayo mazuri, ni muhimu suala la kodi na tozo za ardhi baina ya wananchi wa kawaida na wafanyabiashara liangaliwe upya.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!