Monday, 1 June 2015

KODI KWA MAHOSPITALI BINAFSI IPUNGUZWE


Serikali  imeombwa kuangalia upya tatizo la ukubwa wa kodi kwa hospitali binafsi kwani lengo kuu ni kutoa hudumu bora kwa gharama nafuu kwa kila Mtanzania.


 
Ombi hilo lilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam (RMC), Dk. Amish Kanabar, wakati wa ujio wa Mwenge wa Uhuru kwenye hospitali hiyo ambao ulizindua jengo jipya la ghorofa 10 la hospitali hiyo.
 
Alisema hospitali binafsi na za serikali zina lengo la kuwahudumia Watanzania kupata afya bora, hivyo hakuna haja ya kutoza kodi kubwa kwani hali hiyo inazidumaza na kushindwa kukua kwa kasi.
 
Alisema katika kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora, RMC imechukua mkopo ghali kutoka benki na hata kuweka rehani hisa za wanachama wake ili kufanikisha ujenzi wa jengo jipya.
 
“RMC  inafanya jitihada kuhakikisha inakuwa chuo cha mafunzo ya uuguzi na utaalam wa tiba na afya ili kupunguza pengo la nguvu kazi katika sekta ya afya Tanzania. Mara zote RMC imekuwa ikishirikiana na sekta ya umma, Manispaa ya Ilala na Lions Club ya Dar es Salaam Host na Shirika La Nyumba La Taifa, “ alisema.
 
Alisema hospitali inatoa huduma kwa wastani wa wagonjwa 500 kwa siku na kwamba upanuzi wa jengo una maslahi mapana kitaifa kama vile kuwezesha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa gharama nafuu, kutekeleza kwa vitendo sera za Mkukuta II na Dira ya Taifa 2025 na kuongeza wigo wa ajira na mafunzo kwenye sekta ya afya Tanzania

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!