Saturday, 13 June 2015

BEI YA DHAHABU SOKO LA DUNIA YAPOROMOKA-PROFESA NDULU



Mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu katika soko la dunia yameshuka na kufikia Dola za Marekani milioni 1,377.2  hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, ikilinganishwa na kilele cha dola za Marekani milioni 2,292.1 za kipindi cha mwaka 2012.



 
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Beno Ndullu (pichani), alisema bei ya dhahabu kwenye soko la dunia ambayo imekuwa ikipanda na kushuka, imedondoka na kufikia Dola za Marekani 1,198.9 kwa aunzi moja kwa mwezi Aprili mwaka huu, ikilinganishwa na kilele cha dola za Marekani 1.771 kwa aunzi ya mwezi Septemba 2011.
 
Profesa Ndullu alikuwa akizungumza jana na Wabunge mjini Dodoma, kuhusu mwenendo wa thamani ya Shilingi ya Tanzania.
 
Alisema hali hiyo imetokana na kushuka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa dhahabu nchini, ikichangiwa na uzalishaji mdogo inayotokana na migodi ya Tulawaka na Resolute kufungwa.
 
 "Dhahabu iliyouzwa nje ya nchi imepungua kutoka tani 40 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2011 hadi kufikia 35.5," alisema.
Akizungumzia mwenendo wa thamani ya shilingi Profesa Ndulu alisema kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2014 kulingana na misingi ya kiuchumi imekuwa ikishuka na kupanda ambapo kwa sasa ipo kwa zaidi ya shilingi moja ni sawa dola ya Marekani 1,844.5.
 
Profesa Ndulu alisema uchelewezeshaji wa fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara kutoka nje ya nchi na kuja kwa uchache kumeathiri soko la fedha za kigeni na kuchochea hisia ya kuwapo kwa upungufu wa fedha za kigeni.
 
Alisema katika kipindi cha miezi kumi ya kwanza ya mwaka 2014/15 fedha za wahisani zilizopokelewa zilikuwa dola za Marekani milioni 201.9 ikilinganishwa na makisio ya dola za Marekani milioni 542.9.
 
Aidha, Serikali ilitarajia kupokea mikopo ya kibiashara kutoka nje yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 800 lakini hadi mwezi Aprili 2015 ni dola za Marekani milioni 310 ndiyo zilipatikana.
 
Gavana Ndulu alisema pamoja na sababu hizo ila pia kuna zingine kama msimu wa mapato madogo yatokanayo na utalii wa bidhaa asilia, kuongezeka kwa malipo ya serikali nje ya nchi ambayo yanahusu Tanesco, TRL, na malipo kwa ajili ya mashine ya Biometric Voter Registration (BVR).
 
Alisema sababu nyingine ni kuongezeka kwa malipo ya wakandarasi, hisia za upungufu, na wasiwasi kuhusu uchaguzi na sababu nyingine nyingi.
 
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, alisema ni vema kuwapo na mkakati wa kupanua sekta hiyo ambayo inaonesha kuwa na vyanzo vingi vya kuchochea uchumi wa nchi akitolea mfano Hifadhi ya Sanane, ukerewe na zingine nyingi.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan alisema, BOT imeshindwa kudhibiti mporomoko wa shilingi nchini hivyo kujikuta kila siku fedha ya Tanzania inaporomoka.
 
Azzan alisema maduka mengi ambayo yapo mitaani ya kubadilisha fedha yamekuwa yakifanya biashara hiyo bila kutoa risiti jambo ambalo linakosesha kodi serikali. Kwa upande wake Mbunge wa Arumeru Magharibi, Godluck Ole Medeye, alisema ni jambo la ajabu hapa nchini kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni huku nchi zingine zinatumia fedha zao kwa kila bidhaa.
 
Alitoa mfano Malaysia ni moja ya nchi ambayo inafanya vizuri kutokana na kuwa na msimamo wa matumizi ya fedha yake ya ndani hivyo kukuza uchumi.
 
Ole Medeye alisema kuonesha kuwa Serikali haina nia thabiti ya kuachana na matumizi ya dola hata bajeti yake imeweka viwango vya fedha kwa njia ya dola badala ya kutumia fedha za ndani.
 
Akijibu hoja hizo Gavana Ndulu alisema wao wanazichukua na wanatarajia kuzifanyia kazi ili ziweze kunufaisha maisha ya Watanzania na nchi kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!