Friday, 24 April 2015

WAJAWAZITO, WATOTO WALIVYOHATARINI KATIKA MIGODI GEITA

Ni katika Kijiji cha Nyakabale kilichopo mjini Geita. Kijijini hapo kuna nyumba nyingi zilizojengwa, unazoweza kuzifananisha na makambi ya wakimbizi.

Wakazi wa eneo hilo wanaonekana wakichapa kazi, huku magari yakipishana na pikipiki zilizobeba viroba vya mawe zikipita, nyingine zikiwa zimebeba abiria wanne au zaidi mtindo maarufu wa ‘mshikaki’.
Hakika watu wa kijiji hiki hawakuwa wavivu kwani kila mtu alijishughulisha, si watoto, vijana, wanaume na wanawake.
Kwa juhudi wanazoonyesha, kama watu wote nchini wangekuwa wakifanya kazi kama wanakijiji hawa, bila shaka Taifa lingekuwa mbali kimaendeleo.
Walionekana wakibeba mawe, wengine wakianika udongo. Wengine wakiponda mawe, wengine wakifua dhahabu kwenye makarai na magunia.
“Lete mawe wewe acha kuzubaa, hali ya hewa inabadilika, mvua muda wowote itanyesha,” alisikika kijana mmoja akimwaambia mwenzake.
Pia makundi ya vijana yalikuwa yamebeba nyundo, sururu, wengine wakipanda, wengine wakishuka kutoka milimani.
“Oya, wahi mida ya kunywa chai,” alisikika mmoja wa vijana akihimiza wenzake saa nne asubuhi.
Hakika kijiji hiki kimechangamka, achilia mbali pilika nilizoziona, pia nilisikia kelele za mashine zikisaga mawe.
Zilikuwa ni kelele ya aina yake, zilizochangiwa na muziki uliokuwa ukitokea kwenye baa, hata kusikilizana ilikuwa shida kwangu, ingawa wenyeji walionekana kuzoea hali hiyo.
Ilikuwa ni kazi mtindo mmoja, starehe mtindo mmoja kwani baadhi walikuwa kazini na wengine walionekana wakinywa pombe asubuhi na mapema.
“Wewe mama ongeza bia moja, hapa ni starehe na kazi mtindo mmoja ...leta tukushikie mtoto huyo. Mtakujaje na watoto kazini?” kijana wa umri wa unaofikia miaka 18 alimhoji binti wa umri wake aliyekuwa akiwahudumia.
Eneo hilo pia kuna wanawake wengi. Wengine wajawazito, wengine wananyonyesha na wengine wakiwa wamewabeba wao wachanga migongoni, huku wakigoroga udongo uliochanganywa na maji kwa kutumia mikono yao kwenye makarai.
Baadaye niligundua kuwa matope hayo ni udongo unaoelezwa kuwa na dhahabu, iliyochanganywa na sumu ya zebaki. Ulikuwa ukisafishwa tayari kwa kupata dhahabu.
Katika kijiji hicho, watoto wadogo wenye umri wa wastani unaofikia miaka mitano hadi miwili hawakuwa nyuma, nao walikuwa karibu na mama zao. Walikuwa wakicheza, wengine wakiiga walichokuwa wakifanya mama zao kwa kukoroga udongo kwenye makopo.
“Nipe kopo langu...mama niwekee udongo na mimi nikoroge,” alisikika mtoto wa umri wa miaka mitano akimweleza mama yake. Watoto wengine walikuwa wakicheza mpira, wengine wakichezea maji machafu yaliyotirirka kutoka kwenye mwalo wa kusafisha dhahabu.
Maji hayo ni yale ambayo tayari yamechanganywa na sumu ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Watoto wengine walikuwa wakikoroga udongo kwenye makarai. Watoto hao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka sita hadi 15.
Wengine walikuwa wakizurura ndani ya machimbo hayo, wakisubiri kupewa vibarua vya kusafisha dhahabu, huku wasichana wadogo wengine wakiwa wameketi katika baa wakisubiri wateja.
Ni vigumu kujua sababu ya kijiji hicho kuwa na  wanawake wengi na watoto wadogo ambao wanafanya kazi ya uchimbaji, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na sera ya mtoto.
Mmoja wa wanawake hao ni Kabula Satongima (35), mjane anayefanya kazi ya kukoroga udongo kwenye makarai mzaliwa Kijiji cha Bupandwa, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, anaeleza kuhusu maisha yake na alivyoingia kwenye kazi hiyo.
“Niliolewa nikiwa na umri wa miaka 14 katika Kijiji cha Nyiboko, Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara. Niliishi na mume wangu huko Nyiboko maisha yakawa magumu, Januari 2013, mume wangu alihamia Geita ikiwa ni katika kutafuta maisha,” anasema.
Satongima anaeleza kuwa aliamua kumfuata mumewe katika kijiji hicho na kwamba akiwa hapo alipata ujauzito wa mtoto wake wa mwisho.
“Lakini wakati naendelea kulea mimba yangu, mume wangu aliyekuwa akifanya kazi ya kuokota mawe yanayotupwa na Wazungu aliondoka nyumbani alfajiri na kwenda msituni kutafuta mawe. Akiwa huko alipigwa risasi na askari akafariki dunia,” anasimulia na kuongeza:
“Nililetewa tu taarifa na wenzake, hivi ninavyoongea, hata maiti ya mume wangu sikuiona na sijui alizikwa wapi.”
Mama huyo anasema: “Humu unavyotuona, wanawake wengi waume zetu wamekufa kwa kupigwa risasi na askari wanaolinda mgodi.”
Kuhusu sheria na haki za wanawake na ulinzi kwa mtoto, anasema: “Dada hizo sheria mimi sizijui... sijasoma, nina watoto wengi wasiponisaidia kazi tutakula nini nami sina uwezo wa kuwasomesha?”
Alipotakiwa kueleza amefanya kazi ya kuosha dhahabu kwa miaka mingapi na manufaa aliyopata Satongima anasema: “Kazi hii tunafanya tu, lakini hakuna tunachokipata. Zaidi tunaambulia magonjwa tu.”
Anasema amefanya kazi hiyo kwa miaka minne lakini hakuna alichonufaika nacho zaidi ya kujipatia mlo wa siku.
“Hii ndiyo kazi yangu ya kila siku, nikiamka asubuhi huwakusanya watoto wangu na kuja kufanya hii kazi,” anasema Satongima na kuongeza: Tukifika hapa tunatafuta vibarua vya kuosha dhahabu mimi na wanangu. Nikishapata huwapangia kazi wanangu na kila mmoja anatakiwa kuosha makarai manne kwa siku. Kila karai hulipwa Sh250, hivyo kwa siku tunaweza kupata Sh30,000.”
Maelezo ya mama huyo yanaungwa mkono na watoto wake mmoja wa watoto hao, Anna Otieno (8) anasema: “Huwa tunakuja na mama naye hutuambia tuoshe dhahabu. Sisi tunafanya kazi hiyo ili tumsaidie mama. Tunafanya tu licha ya kwamba tunaumia kwa kukaa chini muda mrefu. Pia baridi kali nyakati za jioni hadi kichwa kinauma.”
Hata hivyo, mama huyo na watoto wake hawafahamu madhara ya sumu ya zebaki.
“Mimi sijui kama ina madhara, ingawa nasikia watu wanasema hivyo. Lakini sina namna, siwezi kuiacha kwa kuhofia madhara. Nikiacha nitakula nini na wanangu?” anahoji Satongima.
Siyo mama huyo pekee aliyeonekana akifanya kazi ya kuosha dhahabu akiwa na watoto wake wadogo, pia wapo wengine akiwamo Savera John (20) anayesema alianza kazi hiyo miezi sita iliyopita.
“Nilipewa ujauzito na mmoja wa vijana wachimba madini. Hata hivyo, alipotea ghafla na haijulikani kama yupo hai au amekufa. Kutokana na hali hiyo, nalazimika kufanya kazi hii,” anasema Savera huku akiwekewa zebaki kwenye makarai aliyokuwa akikoroga kuosha dhahabu.
Mama mwingine mjamzito anaonekana eneo hilo na bila kujua madhara anayoweza kusababisha kwa mtoto aliye tumboni, anaomba kazi ya kuosha dhahabu kutumia zebaki.
“Kaka nimekuja leo, vipi kazi ipo?” aliuliza na kujibiwa: “Kazi ipo, wewe tu, kaa tukuchanganyie udongo.”
“Nina mimba ya miezi saba, mwanagu ana mwaka mmoja, nafanya vibarua ili nipate pesa ya kula. Sina mume kama unavyoniona,” anasema huku akiendelea na kazi hiyo hatari akiwa amekaa chini, na mtoto mgongoni.
Daktari Adam Sijaona wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, anabainisha madhara ya sumu ya zebaki  endapo mtu ataishika, kula au kuvuta hewa yake akisema; “ni sumu hatari kwenye mwili wa mwanadamu hasa inapotumika kwa muda mrefu kwa kuigusa, kula au kunusa.”
Binti wadogo, Tereza John (14) na Happyness Deusi (13) wanachenjua dhahabu katika udongo uliochanganywa na zebaki kwa mikono. Hawa wanaishi mbali na wazazi wao, Tereza anaeleza wazazi wake wako Kijiji cha Katoro.
“Huwa nalala huku kila siku kwa rafiki zangu, usalama wangu ni mdogo. Siku nyingine hubakwa na wachimbaji madini, siku nyingine nikikosa vibarua, nalala njaa,” anasema.
“Kaka nimekuja leo, vipi kazi ipo?” aliuliza na kujibiwa: “Kazi ipo, wewe tu, kaa tukuchanganyie udongo.”
“Nina mimba ya miezi saba, mwanagu ana mwaka mmoja, nafanya vibarua ili nipate pesa ya kula. Sina mume kama unavyoniona,” anasema huku akiendelea na kazi hiyo hatari akiwa amekaa chini, na mtoto mgongoni.
Daktari Adam Sijaona wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, anabainisha madhara ya sumu ya zebaki  endapo mtu ataishika, kula au kuvuta hewa yake akisema; “ni sumu hatari kwenye mwili wa mwanadamu hasa inapotumika kwa muda mrefu kwa kuigusa, kula au kunusa.”
Binti wadogo, Tereza John (14) na Happyness Deusi (13) wanachenjua dhahabu katika udongo uliochanganywa na zebaki kwa mikono. Hawa wanaishi mbali na wazazi wao, Tereza anaeleza wazazi wake wako Kijiji cha Katoro.
“Huwa nalala huku kila siku kwa rafiki zangu, usalama wangu ni mdogo. Siku nyingine hubakwa na wachimbaji madini, siku nyingine nikikosa vibarua, nalala njaa,” anasema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!