Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo (pichani), amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kugombea urais, ili wananchi wapate wigo mpana wa kuchagua anayefaa kuiongoza nchi.
Kardinali Pengo alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tawi la Dar es Salaam (SJUIT).
Kardnali Pengo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya wahitimu 798 wa ngazi za shahada, stashahada na astashahada ambao walitunikiwa na Mkuu wa Chuo, Dk. Arul Raj.
Alisema iwapo watajitokeza wagombea wengi wa urais, itawasaidia wananchi kuwafahamu wagombea wao vizuri, kuwapima kwa kulinganisha sifa zao kabla ya kuchagua mmoja kuwa kiongozi wa nchi.
Alisema kujitokeza kwa watu wengi wenye nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu ni jambo jema, kwani watakapo jitokeza wachache au mmoja, wananchi wanaweza kuchagua kiongozi asiye na sifa.
“Mimi nadhani ni jambo zuri kwa watu wengi kujitokeza kugombea nafasi ya urais, akijitokeza mtu mmoja kugombea urais wananchi watashindwa kufahamu kama anafaa kwani hakutakuwa na wa kumlinganisha naye,” alisema.
Baadhi ya makada ndani ya vyama vya siasa wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo na wengine wanatajwa.
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), makada kadhaa wamejitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapong’atuka Oktoba mwaka huu.
Waliotangaza nia hadi sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalah na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alitangaza akiwa ziarani nchini Uingereza na kueleza kuwa alifanya hivyo kimya kimya.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum); Prof. Mark Mwandosya na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, aliyetangazia nia hiyo nchini Uingereza.
Viongozi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mbunge wa Sengerema, Willium Ngeleja na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kwa upande wa Tanzania Labour Party (TLP) aliyejitokeza na alitarajiwa kupitishwa na Mkutano Mkuu ulioanza jana jijini Dar es Salaam ni Macmillan Lyimo.
Vyama vya Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimepanga kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Wanaotajwa katika vyama hivyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.
WAGOMBEA WANAOTUMIA FEDHA
Kadhalika, Kardinali Pengo aliwatahadharisha wananchi dhidi ya wagombea wa nafasi ya urais wanaotoa rushwa ili waingie Ikulu, kwani uongozi wa taifa hauwezi kununuliwa.
Alisema viongozi wakipatikana kwa njia ya rushwa wakishaingia madarakani watataka walipe madeni badala ya kuwahudumia wananchi.
“Wananchi wanapaswa kufikiri kwa kina na busara na kuachana na viongozi ambao wanawashawishi wawachague kwa kuwapa rushwa kwani watakapo ingia madarakani lazima walipe fadhila kwa waliompa fedha za kutoa rushwa wakati wa mchakato wa uongozi,” alifafanua.
TISHIO LA UGAIDI
Akizungumzia suala la tishio la ugaidi nchini pamoja na ujumbe mfupi wa maneno unaosambazwa kwa simu za kiganjani na watu kuhusu matukio hayo, alisema serikali pamoja na wataalamu wa usalama nchini wanapaswa kuchukua tahadhari mapema kuimarisha ulinzi wa wanachi.
Kardinali Pengo alisema kama kuna hofu juu ya ugaidi, basi serikali iwahakikishie usalama wananchi wake.
Alisema wanaosambaza ujumbe wa tishio hilo kuwa na uhakika wa kile wanachokisambaza, kwani kwa kufanya hivyo bila uhakika wanaweza kusababisha maafa makubwa na hofu.
AWASHAURI WAHITIMU
Awali, akiwahutubia wahitimu na uongozi wa chuo hicho, Kardinali Pengo alisema miaka ya nyuma serikali iliwekeza kwenye masomo ya sanaa zaidi kuliko sayansi, jambo ambalo limesababisha taifa kukosa wataalamu wengi wa sekta hiyo.
Alisema hali hiyo imebadilika kwani serikali sasa inawapa kipaumbele wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kuwapatia mikopo inayoweza kuwasaidia katika masomo yao.
“Nawashauri wanasayansi wangu mliohitimu leo hii (jana) na wale ambao bado wapo vyuoni kuondokana na fikra ya kuajiriwa serikalini pale wanapomaliza masomo yao, unaweza kujiajiri hata ukiwa umesoma masomo ya sayansi au sanaa,” alisema na kuongeza:
“Sayansi ni kwa ajili ya wanadamu hivyo itumike kuwanufaisha wanadamu kibinadamu.”
Kardinali Pengo alikuwa akitembea kwa kutumia fimbo ya kutembelea.
AELEZEA AFYA YAKE
Aidha, kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuelezea maendeleo ya afya yake na jinsi alivyopatiwa matibabu kuwa alifanyiwa upasuaji wa pili nchini India katika Hospitali ya Manipal iliyopo Bangolore, baada ya upasuaji wa kwanza aliofanyiwa mwaka 2013 Ujerumani kushindwa kumpa nafuu.
Alisema kinachomsumbua ni uti wa mgongo na hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji huo ingawa madaktari walimwambia atapona vizuri na kuacha kutumia fimbo baada ya miaka miwili.
“Kwa wale wanaotaka kujua afya yangu na ambao wananikumbuka kwenye maombi na wahakikishia kuwa hivi sasa naendelea vizuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment