Edward Lyimo, akionyesha fuvu la baba yake mzazi.
Ni jambo linaloweza kuwa geni kidogo kwa baadhi ya makabila, lakini kwa baadhi ya Wachaga wa Kilema mkoani Kilimanjaro kuna mila ambazo kwa makabila na jamii nyingine zinaweza kuwa za kushangaza.
Jamii hii inaonekana kuwa tofauti na Wachaga wengine kwani wao huwafukua wapendwa wao waliofariki kila wanapotimiza miaka minane hadi 10 baada ya kuzikwa.
Mila hiyo ina taratibu zake za kufuata kabla ya kufikia hatua ya mwili kufukuliwa sehemu ulikokuwa umezikwa na kwenda kuhifadhiwa sehemu nyingine.
Kitendo cha kufukua maiti kimekuwa kikifanywa kwa kufuata taratibu maalumu za kimila na zisipofuatwa inaaminika huwa na madhara makubwa kwa ukoo ikiwamo kusababisha kifo.
Wenyewe wanasemaje?
Mmoja wa wanaukoo wa Lyimo, Edward Lyimo anasema utamaduni huo aliukuta tangu akiwa mdogo na unaendelea mpaka sasa akiwa mtu mzima.
“Si jambo la ajabu. Katika utu uzima wangu nimeshafukua ndugu zangu wengi tu waliokufa miaka ya nyuma na kuihifadhi eneo maalumu lililotengwa na familia kwa ajili hiyo,” anasema.
Anasema sherehe hufanyika kimila kwa kutumia jani maalumu linaloitwa sale kwa kuchomekwa kwenye kaburi la marehemu ambapo hufukuliwa siku moja baada ya kuwekwa kwa jani hilo.
“Kuna mzee maalumu ambaye anasimamia hatua zinazotakiwa kufuatwa na ndiye anafanya zoezi hilo la kuwafukua marehemu ambao miaka yao imekwishafika,” anasema na kuongeza kuwa mzee huyo ndiye mtu pekee anayefanya kazi hiyo.
Lyimo anafafanua kuwa inatakiwa kila ukoo unaofanya mila hiyo uwe unajua taratibu za kufukua, lakini kutokana na ugumu wa mila hiyo imekuwa ikishindikana kwa baadhi ya watu.
“Kulikuwa na wazee wawili ambao walikuwa wanafanya kazi hiyo na tulikuwa tukiwaona lakini wameshakufa na kulikuwa na mzee maarufu sana kwa mila na kuvunja laana,” anaeleza.
Anasema mzee huyo ndiye aliyekuwa akifanya mila hizo kijijini kwao na alikuwa na uwezo wa kuzunguka sehemu nyingi kusaidia watu katika mila zao.
Lyimo anasema baada ya mzee huyo kufariki, sasa wanamtumia mtu mwingine aliyerithi utaalamu huo wa kufukua maiti.
Mila ya kufukua maiti
Anaelezea kuwa ndugu wao anapofariki na kutimiza miaka minane baada ya kufa, huwa anaanza kuwatesa familia kama hawatamfukua kama mila zao zinavyoelekeza.
“Asipofukuliwa kunakuwa na mikosi, hivyo lazima tufanye hilo tambiko na kwa kuwa familia haina utaalamu huo, inabidi tuandae vitu vyote vinavyohitajika na kisha tunamuomba mtu wa mila atusaidie”.
Siku moja kabla muda wa saa 10:00 alasiri, yeye (mzee wa mila) anaotesha jani la sale pamoja na kumwaga pombe ya mbege kwenye kaburi ambalo mtu anatakiwa kufufuliwa. Kesho yake mzee huyo huenda kaburini kuliangalia jani hilo kama limenyauka au la. Kama halijanyauka ni ishara ya kwamba wakifukua kaburi hilo watakuta fuvu la mhusika.
“Nikikuta sale halijanyauka mbuzi anachinjwa na kunena maneno yanayotakiwa kuzungumzwa wakati namwaga damu ya mbuzi katika kaburi hili,” anasema na kuongeza: “Kisha wanaukoo wanaanza kufukua kaburi huku akiwaelekeza vitu vya kufanya.”
Anasema wanaukoo hufukua kaburi huku kina mama wakiendelea na shamrashamra za kupika maana inakuwa ni sherehe kubwa.
Anasema mara tu wanapoanza kuona mabaki ya marehemu wanasitisha kila kitu, huku wanawake wakiruhusiwa kusogelea eneo hilo na kuanza kupiga vigelegele.
Anasema kina mama wakishapiga vigelegele wanaanza kuwapa watu chakula kilichoandaliwa na huwa wanakaa sehemu husika siku nzima kwa sababu kazi hiyo huchukua muda mrefu hivyo inawabidi kula na kunywa.
Anasema baada ya vigelegele kumalizika, fuvu la mhusika linachukuliwa na kufungwa kwenye majani ya sale na kisha kuhifadhiwa ndani.
Fuvu hilo likishahifadhiwa ndani ni ishara kuwa mtu huyo yuko hai na si mfu tena kwa mila na imani za Wachaga wa Kilema.
“Nikishaliweka ndani naendelea kutafuta mabaki mengine ndani ya lile kaburi maana ukibaki hata msumari wa jeneza, tuliokuwa tunafanya kazi ya kufukua tunapatwa na mauzauza ya kutolala.
Anasema kesho yake huamka asubuhi mapema na kuchukua fuvu hilo na kulisafisha kwa kulipaka mafuta ya ‘msuka samli’ na kisha kulifanyia mila nyingine.
“Baada ya hapo nalishikilia na wanaukoo wanakuja mmoja mmoja kuja kulipaka fuvu hilo mafuta. Wakati wakipaka mafuta kwenye fuvu hilo, kila mtu anakuwa akiomba mahitaji yake.”
Anasema baada ya kupaka mafuta fuvu hilo huwa analibeba na kupeleka sehemu ya kulihifadhi akiandamana na baadhi ya wanaukoo kwa idadi sawa ya jinsi.
Lyimo anasema wakiwa wanaelekea sehemu hiyo aliyoiita ‘Mbuoni’ huwa hawaruhusiwi kugeuka nyuma hadi wanapofika sehemu wanapoweka fuvu hilo.
Anasema mara baada ya kuhifadhi fuvu hilo sehemu husika, hurudi na kuendelea na sherehe za kimila.
Sababu ya mila hiyo
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kyuo, Aloyce Lyimo anasema sababu ya kufanyika kwa mila hiyo ni ufinyu wa ardhi hali inayosababisha wananchi kuendeleza mila hiyo ya tangu enzi za mababu.
“Miaka ya sasa watu wanakufa kwa wingi na tukisema tusiwafufue vizazi vyetu vitakosa mashamba ya kurithi kwa kuwa makaburi yatakuwa kila kona ni mila nzuri na ya kuigwa.
Anasema kuwa zamani wazee walikuwa hawaziki, bali walikuwa wanahifadhi mwili huo ndani na baada ya miaka miwili wanachukua masalia na kuyahifadhi sehemu iliyotengwa.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment