LILE sakatala lililotamba kwenye vyombo vya habari la bi harusi, Bahati Mwakambonja (54), kutaka kufunga ndoa na kijana wa miaka 24, Isiaka Jeremiah limechukua sura mpya baada ya bwana harusi huyo kutoweka nyumbani Mkuranga, Pwani na kwenda kusikojulikana huku bibi huyo akishinda analia.
Bibi Bahati Mwakambonja anayedai kutorokwa na mchumbaake.
Timu ya Amani hivi karibubni ilifika nyumbani kwa mwanamke huyo mjini Mkuranga na kumkuta katika lindi la mawazo.Akizungumza na gazeti hili kwa masikitiko makubwa, Bahati alisema: “Mchumba wangu kakimbia jamani. Niliwashangaa sana viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kurasini (Dar) kukwamisha ndoa yangu na yule mchumba wangu, nimehuzunika kwa kiasi kubwa hadi sasa.
“Kwanza nikiri kwamba mimi sizai, hiyo ni mipango ya Mungu, huwezi kulazimisha hali niliyonayo. Tumekaa kwa muda mrefu bila kufunga ndoa lakini ilifikia hatua tukaamua kitu ambacho hata kwa Mungu ni baraka kwetu lakini matokeo yake imekuwa kinyume,” alisema mwanamke huyo.
Bibi huyo alisema kama kuolewa na huyo kijana alishaolewa kwa sababau walishaenda sehemu zote mbili, yaani nyumbani kwa mwanaume na kwa mwanamke.“Mume wangu alifanya mazungumzo na familia yangu na kuhojiwa maswali kadhaa ambayo aliyajibu na kuambiwa atoe mahari kitu ambacho alifanya kwa kutoa sehemu ya mahari.
“Hatua tuliyokuwa tunakwenda ndugu waandishi ya kukamilisha taratibu za ki-Mungu ambapo tunajua kila mtu ana sehemu anayoiabudu hapa duniani na mimi nilikwenda pale kwa sababu ni eneo ambalo nilikuwa nikipata huduma kabla ya kuhamia hapa Mkuranga.
“Lakini baada ya kufika eneo lile nikaambiwa mambo ambayo nilikuwa siyategemei hata siku mmoja, likiwemo la kuwasilisha barua ya talaka au cheti cha kifo cha mume wa kwanza.“Mimi niliachana na mume wa kwanza kwa muda mrefu sana na alinikataa kwa sababu sizai na kuwaambia wale waliosimamia ndoa ya awali kuwa anawaruhusu kama nikipata mchumba niolewe,” alisema Bahati.
Aidha, alisema kuna watu waliwafuata wakiwaahidi watawasaidia ili kufanikisha kufungwa kwa ndoa hiyo lakini matokeo yake baada ya wao kuondoka walishitukia taarifa hizo ziko kwenye magazeti.
Alisema baada ya Isiaka kuona taarifa hizo kwenye gazeti alitoweka na baadhi ya vielelezo kama picha walizopiga siku za nyuma.
“Mimi kama mtu mzima nimechaganyikiwa hasa baada ya ndoa yangu kukataliwa sehemu zote nilizokwenda na kibaya zaidi ni pale mume wangu kuondoka na vitu muhimu kwenda nisikokujua, hana simu.Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa, mama huyo kwa sasa anajitafutia kipato cha kila siku kwa kufundisha watoto wadogo wapatao 8 ambao kila baada ya kufundisha hulipwa shilingi 200 kwa siku. Alisema kuwa hana uchumi mwingine.
Alisema uhusiano wake na kijana huyo ulianza baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuolewa lakini chanzo kikubwa kilichomkutanisha na Isiaka ni ugonjwa wa kisukari uliyokuwa unamsumbua kwa muda mrefu.
Alisema yeye na mume wake wa kwanza walioana mwaka 1992 na kuachana 1995. Alikaa hapo mpaka Januari 2003 alipokutana na kijana huyo.
Aliongeza kuwa walipokutana na kijana huyo hawakuanza uhusiano moja kwa moja lakini baada ya kuona anampa msaada ambao hata mbele za Mungu inakubalika ndipo waliamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi hatimaye kulipa mahari na hatimaye kanisani ambako walikataliwa kutokana na tofauti ya umri.
Baadhi ya majirani waliozungumza na Amani kuhusiana na sakata hilo walisema:
“Ni kweli kijana huyo alikuwa akionekana eneo hilo na kila mtu alijua ni mfanyakazi wa mama huyo.
“Hakuna aliyefikiria kijana huyo ndiye mume wa mama huyo,” alisema jirani mmoja.
Amani lilimtafuta Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kurasini, Dar, Yusuf Ngelein ambapo alikiri kumfahamu Bahati kama muumini wake.“Alifika hapa na mwenzake kutaka taratibu za kufunga ndoa. Mimi kama kiongozi wa kanisa nilimpa vigezo vya kutimiza lakini hawakurudi maana yake walikuwa na upungufu,” alisema mchungaji huyo
NA MAKONGORO OGING, PWANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment