Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesisitiza msimamo wake wa kusitisha kutoa huduma ya usafiri leo, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini Nchini (Sumatra) ikionya kuwa itamfutia leseni ya usafirishaji yeyote atakayegoma.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alisisitiza msimamo wao wa kugoma walioutoa juzi alipozungumza na NIPASHE jana.
Alisema mgomo walioutangaza uko palepale ingawa kuna mazungumzo kati yao na Sumatra yaliyotarajiwa kuendelea jana.
“Msimamo wetu wa kusitisha kutoa huduma za usafiri na kutotumia bei mpya ya nauli iliyotangazwa na Sumatra uko palepale,” alisema Mrutu.
Aliongeza: “Ila leo (jana) asubuhi tumewaandikia barua ya kuwataarifu kuwa nauli mpya ambazo wao wamezishusha hatuko tayari kuzitumia. Mara nyingi tumekuwa tukikubaliana sababu zinazofanya nauli kupanda, ikiwamo kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Lakini wenzetu wanachukilia haya mambo kirahisi sana.”
NIPASHE, ambayo ilitembelea Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) jana, ilishuhudia baadhi ya abiria wanaotegemea kusafiri kwenda sehemu mbalimbali kama vile Kigoma, Bukoba, Tunduma, Lusaka na Mwanza wakiendelea kukata tiketi kwa ajili ya kusafiri leo, kesho na keshokutwa.
Baadhi ya mawakala waliozungumza na NIPASHE katika kituo hicho, walisema wataendelea kukata tiketi mpaka watakapopata taarifa rasmi kutoka kwa wamiliki wa mabasi za kusitishwa kwa huduma hiyo.
Karani wa kampuni ya mabasi ya Otta High Class yanayofanya safari zake Dar es Salaam, Kahama na Bukoba, Hawa Jacobo, alisema wanaendelea kukatisha tiketi kwani hawajapokea taarifa zozote kutoka kwa mmiliki za kuwataka wasitishe suala hilo.
Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya makarani wameelekezwa na mabosi wao kusitisha kukata tiketi.
“Magari mengine yalikuwa yameshawekewa ‘booking’ kabla ya tamko la mgomo halijatolewa. Ila sisi makarani tumesikia kwenye vyombo vya habari na kwa baadhi ya wenzetu waliopata taarifa hizi,” alisema Hawa.
Karani wa kampuni ya mabasi ya Adventure yanayofanya safari zake Kigoma- Dar es Salaam, Mariam Abubakari, alisema hakuna taarifa rasmi waliyopata juu ya usitishaji wa ukataji wa tiketi.
Mmoja wa abiria, Halima Luvanda, ambaye alifika katika kituo hicho na kukata tiketi, alisema mgomo huo utawaathiri abiria.
Hivyo, akaishauri serikali kushauriana na wamiliki kabla mgomo haujatokea ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Abiria mwingine, Rose Chacha, alisema mgomo huo utawaumiza watu wa hali ya chini ambao mabasi ndiyo usafiri wao mkubwa wanaoutegemea kwa safari za ndani na nje ya nchi.
NIPASHE ambayo jana ilifika kwenye ofisi za Taboa kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya mgomo huo, ilishuhudia mmoja wa wajumbe wa chama hicho akitoa maelekezo kwa njia ya simu kwa mawakala wa kampuni za mabasi ya kusitisha ukataji wa tiketi kwenye ofisi za mabasi.
“Msiendelee kukatisha tiketi kwa abiria. Hata kama kuna abiria ambaye atakuwa amekatiwa tiketi atatakiwa kurudishiwa fedha zake ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza,” alisikika akiongea kwa simu.
KAULI YA SUMATRA
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema wamepokea barua kutoka Taboa ikilalamikia ushushwaji wa nauli.
Hata hivyo, alisema utaratibu unaotumiwa kukataa nauli mpya siyo sahihi kwa mujibu wa sheria ya usafirishaji ya mwaka 2009 inayoelekeza namna ya kupinga tozo ya nauli nchini kote.
“Naagiza maafisa wote wa Sumatra nchini ikitokea mmiliki yeyote kuanzia kesho (leo) hataingiza basi barabarani wamnyang’anye leseni ya usafirishaji. Nchi hii inaongozwa kwa sheria na taratibu,” alisema Ngewe. Juzi wamiliki wa mabasi walikutana katika mkutano wa dharura na kujadili mambo mbalimbali, ikiwamo ongezeko la nauli za mabasi ya masafa marefu na kukubaliana kusitisha huduma hadi pale Sumatra watakapotoa taarifa ya kuwa nauli za zamani zitaendelea kutumika.
Siku 18 baada ya madereva kugoma na kutikisa nchi, Taboa ilitangaza mgomo kuanzia leo wa kusitisha ukatishaji wa tiketi kwa safari za mikoani na nchi jirani.
Aprili 15, mwaka huu, serikali ilitangaza viwango vipya vya nauli, ambavyo vitaanza kutumika Aprili 30 kwa kushusha nauli za mabasi yaendayo mikoani, huku nauli za daladala mijini zikibaki palepale.
Viwango hivyo vipya vya nauli za mabasi vilitangazwa kwa punguzo la asilimia 7.8 kwa daraja la kawaida na asilimia 5.81 daraja la kati.
Ngwee alisema viwango hivyo vimebadilika kufuatia kushuka kwa bei ya mafuta mwishoni mwa mwaka 2014 na jamii kutaka nauli hizo kushuka ili punguzo hilo lifaidishe wote abiria na wenye magari.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment