Umoja wa Vyama vya Madereva Nchini (UMDT), umefichua siri ya ajali zinazoendelea nchini kuwa zinatokana na shinikizo kutoka kwa waajiri wanaomiliki magari kuwataka kuyakimbiza mabasi ili kuwahi abiria siku inayofuata.
Katibu Mkuu wa umoja huo, Rashid Said, aliliambia NIPASHE Jumapili jana kuwa, wamiliki wao wamekuwa wakiwashinikiza kukimbiza magari kwa lengo la kufika mapema kwenye safari zao na kesho yake kufanya safari nyingine.
Alisema kutokana na masharti waliyopewa na serikali kubatilishwa, lakini imekuwa kinyume kitendo kilichowafanya, waamue kumwandikia barua Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuomba kukutana naye.
Alisema lengo la kukutana na Pinda ni kumweleza kero zao ambazo tayari walishaziwasilisha wiki tatu zilizopita mbele ya Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, ambaye baadhi alizitolea ufafanuzi na nyingine kuahidi kuzifanyia kazi.
Alisema licha ya waziri huyo kutoa tamko kwao kuwa, amesitisha zoezi la kurudi shule madereva mara wanapozihuhisha leseni zao baada ya miaka mitatu, lakini kumekuwa na matamko ya viongozi wa chini wa serikali kupinga hilo na mengine waliyokubaliana siku hiyo.
Alisema kutokana na mkanganyiko wa matamko hayo ambayo sasa yamewaacha njia panda, Aprili 20, mwaka huu kupitia kwa mwanasheria wao, walimwandikia barua Pinda kuomba kukutana naye ili wamweleze madai yao.
Alisema msukumo wa kumwandikia barua Pinda, ulikuja baada ya kikao cha Aprili 18, mwaka huu, ambacho kilikusudia kuwakutanisha wao na mawaziri wanne wa Wizara ya Miundombinu, Uchukuzi, Wizara ya Kazi na Mambo ya Ndani ya Nchi, kufanyika bila mawaziri hao.
Alisema mkutano wao uliwakutanisha na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), polisi na Naibu waziri wa Kazi, Makongoro Mahanga.
Alisema katika kikao hicho, hawakufikia muafaka wa kero zao walizoziwasilisha awali serikalini ndipo wakamwandikia barua Pinda.
Alisema katika hali isiyo ya kawaida, siku moja kabla ya kikao hicho, mawaziri hao walikutana na wamiliki wa mabasi kitendo ambacho wanakitafsiri kuwa kilikuwa hakina lengo zuri kwao.
Alisema wakati wanasubiri majibu ya barua kwa Pinda, walitarajia kukutana leo (Jumapili) na madereva ili kuwapa mrejesho wa kikao chao na Mahanga, lakini kutokana na Sikukuu ya Muungano watakutana Jumatano ijayo.
Akielezea kwa nini wanataka kukutana na Pinda, Said alisema lengo ni kumweleza yanayowasibu ikiwa ni pamoja na ongezeko la ajali za barabarani.
“Tunasikitishwa na kauli za baadhi ya viongozi ambao wanarusha tuhuma kwetu kuwa ni chanzo, lakini yapo mengi nyuma yetu,” alisema na kuongeza:
“Moja ya chanzo cha ajali hizi ni mashinikizo tunayopata kutoka kwa wamiliki wa mabasi tunayoendesha, tunao ushaidi wa madereva wenzetu waliopoteza maisha na wengine kupata ulemavu kutokana na mashinikizo haya,” alisema.
Alisema wapo waliopoteza maisha ambao kabla ya ajali kutokea waliwasiliana na madereva wenzao kuwaeleza kuhusu mashinikizo waliopata kutoka kwa wamiliki kuwataka wakimbize magari na walipotekeleza walikumbana na kifo.
Aliongeza kuwa basi linapofika mapema hupata abiria wa kurudi kesho yake mkoa mwingine lakini linapochelewa hulazimika kulala hadi siku inayofuata.
“Hatupendi kukimbiza magari lakini tunalazimika kufanya hivyo ili kulinda vibarua vyetu, usipotekeleza agizo la mmiliki wa chombo husika basi unafukuzwa kazi na anatafutwa mwingine atakayeendana na matakwa ya mmiliki, hili linafanyika kwa sababu hatuna mikataba nao ndio tatizo kubwa ambalo tunataka kuzungumza na Pinda,” alisema.
Alisema chanzo kingine ni dereva mmoja kuendesha mwendo mrefu bila kuwa na msaidizi huku akitakiwa kesho yake arudi alikotoka.
“Dereva huwezi kupumzika ukiwa ndani ya basi maana ukiangalia mwenzako anavyoendesha nawe ndani ya moyo wako unaendesha unajiongelesha yaani kwenye kona hii ingekuwa mimi ningeenda kasi au ningepunguza mwendo, kwa hiyo unakuta akili zao zinafanya kazi hawapumziki,” alisema.
Said alitaja chanzo kingine kuwa ni baadhi ya vyombo hivyo kumilikiwa na vigogo serikalini ambao kwa nafasi walizonazo husababisha mabasi yao kutokaguliwa na askari hivyo kusababisha ajali.
Alisema inapotokea ajali wamiliki wa vyombo bila kujali waliokufa husherehekea kwa sababu vyombo vyao wamevikatia bima.
“Basi linapopata ajali mmiliki kama utatoka hai atakuuliza limeumia kwa kiwango gani, kama ni kidogo wengine huwa wakali kwa nini dereva hujalibamiza sana..., wao wanaangalia kulipwa bima sio roho zinazoteketea kwenye vyombo hivyo,” alisema.
Alisema takwimu walizonazo zinaonyesha kuwa kati ya Januari hadi sasa jumla ya madereva 26 wamepoteza maisha kwenye ajali za barabarani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment