Kikwete atahitimisha kipindi chake cha miaka 10 ya kuongoza nchi mwishoni mwa mwaka huu baada ya kupatikana kwa mrithi wa kiti chake kwenye Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike mwishoni mwa Oktoba.
Tayari Kikwete ameshahudhuria sherehe za mwisho za Uhuru akiwa Rais zilizofanyika Desemba 9 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sherehe hizo zinazofanyika Aprili 26 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya kuunganisha mataifa ya Tanganyika na Zanzibar yaliyoungana mwaka 1964.
Akizungumzia sherehe hizo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema alisema maandalizi yamekamilika na kwamba kauli mbiu ni Miaka 51 ya Muungano, Tudumishe Amani na Umoja, Ipigie Kura ya Ndiyo Katiba inayopendekezwa na Kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Mkuu wa wilaya, ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, alisema milango uwanjani hapo itafunguliwa kuanzia saa 12:30 asubuhi ili kuwaruhusu wananchi kushiriki tukio hilo la kihistoria litakaloambatana na michezo ya halaiki, ngoma za asili, vikundi vya burudani na gwaride la heshima litakalohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment