Tuesday, 28 April 2015

SERIKALI SASA YATANGAZA AJIRA KWA WALIMU 41, 681


Serikali imetangaza ajira mpya za walimu 41,681 kwa ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada na mafundi sanifu maabara na kutakiwa  kuripoti katika vituo vya kazi kuanzia Mei 1 hadi 9,  mwaka huu.


 
Ajira hizo mpya zilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
 
Alibainisha kuwa walimu waliopangiwa wa ngazi ya Cheti ni 11,795, Stashahada 6,596, Shahada 12,665, na Mafundi sanifu maabara 10,625.
 
Alisema walimu  wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi kabla ya Mei 9 ili kuingizwa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara wa mwezi Mei.
 
“Walimu hawa ni wale wapya na wale ambao walitoka kazini kwenda kusoma, lakini wote tumewapangia vituo, kwa wale ambao walikuwa na vituo vya kazi warudi vituoni kwao. Pia ni muhimu kuwahi kuripoti kabla ya Mei 9, ukichelewa baada ya hapo huwezi kuingizwa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara wa mwezi huo, hivyo itakubidi kusubiri mwezi unaofuata,” alisema Sagini.
 
Kuhusu ajira hizo, alisema serikali imelenga katika halmashauri ambazo hazikuwa na walimu na zilizokuwa na uhaba mkubwa ili kuleta usawa na uwiano bora wa mwalimu kwa mwanafunzi.
 
Alisema shule ambazo hazikuwa na walimu na zenye uhaba mkubwa zimepangiwa walimu wengi zaidi huku ambazo zilikuwa zimejitosheleza hazikupangiwa kabisa.
 
Sugini alizitaja halmashauri ambazo zimepangiwa walimu wengi ni Kaliua, mkoani Tabora ambayo ilikuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 211, waliopangiwa ni  walimu 1,143 sawa na uwiano wa mwalimu mmoja wanafunzi 45.
 
 Nyingine ni Geita Vijijini, mkoani Geita ambayo ilikuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 65, waliopangwa ni walimu 963 sawa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
 
Halmashauri nyingine ni Biharamulo, mkoani Kagera ambayo ilikuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 66, imepangiwa walimu 360 sawa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
 
 Muleba ya mkoani humo aliitaja kuwa ilikuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 60 na kwa sasa imepangiwa walimu 523, sawa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafuzi 45.
 
Sigini aliitaja halmashauri nyingine kuwa ni Bunda, mkoani Mara ambayo ilikuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 74 imepewa walimu 797 ambayo itakuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
 
MIJINI, MAJIJI HAWAKUPANGIWA 
Kuhusu halmashauri ambazo hazijapangiwa walimu kutokana na kujitosheleza ambazo ni za maeneo ya mijini na majiji alizitaja kuwa ni Halmashari ya Arusha, Ilala, Kinondoni na Temeke (jijini Dar es Salaa) na Manispaa ya Dodoma.
 
“Wito kwa walimu wasitafute kuanza kuhama sasa wajikite kuripoti kwenye vituo vya kazi ili taratibu nyingine zifuate na utaratibu kutafuta uhamisho ufuate akiwa yuko kazini, nina sema hivyo kwa sababu tutaanza kupokea walimu wengi hapa wakitaka kuhama kabla ya kuripoti kituo cha kazi,” alisema Sagini.
 
Akizungumzia upangaji wa masomo, Sagini alisema walimu wa masomo ya sayansi (Fizikia, Kemia, Baiolojia na Hisabati) wamepangwa moja kwa moja katika shule ambazo hazina walimu wa masomo hayo.
 
 Alisema walimu wa masomo ya sanaa, kilimo, michezo watapangiwa masomo na waajiri wao ambao ni halmashauri husika kabla ya walimu hao hawajaanza kuripoti kazini. 
 
“Natoa wito kwa waajiri kuwa wapange walimu wapya na mafundi sanifu maabara kwa haki ili shule zote ziwe na walimu wa kutosha. Nasisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri  wa kuwapokea watumishi wapya na kuwafikisha kwenye vituo vyao vya kazi,” alisema Sagini.
 
 Aidha, akizungumzia malipo ya fedha za kujikimu kwa waajiriwa hao wapya, Sagini alisema, Ofisi ya Hazina imetenga Sh. bilioni 9 kwa ajili ya posho za kujikimu na fedha za nauli.
 
Alisema, mtumishi atalipwa posho hizo, wiki moja baada ya kuripoti kituo cha kazi mara baada ya kuripoti kwa mwajiri na mkuu wake wa kazi kusaini barua ya kumpokea. 
 
Sagini aliwataka waajiri kuwapokea na kuwaelekeza watumishi hao kwenye vituo vya kazi mara wanaporipoti katika halmashauri ili kuanza taratibu za malipo kwa wakati.
 
 “Wanatakiwa kulipwa posho zao wiki moja baada ya kuripoti kituoni, zikichelewa sana zisizidi wiki mbili, malipo hayo yatajumuisha fedha za kujikimu na nauli ambazo wamesafiria kwenda kituo cha kazi. 
 
 Pia, nimeziagiza halmashauri zote kuhakikisha zinawalipa posho hizo kutoka kwenye mfuko wa dharura wa halmashauri kama hazina itachelewa kupeleka fedha hizo,” alisema Sagini.
 
Pia aliwataka waajiriwa hao wapya kufuata taratibu kwa masula yanayohusiana na utumishi na kuwasilisha vyeti vyao vyote ili kuondoa utata na usumbufu wakati wa kujitambulisha na taratibu za mfumo wa mishahara.
 
 Sigini alisema orodha rasmi ya walimu na mafundi sanifu maabara waliopata ajira inapatikana kwenye tovuti ya Tamisemi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi 
 
KIDATO CHA TANO KUPANGIWA SHULE MWEZI UJAO
Mbali na hilo, Sagini pia alisema serikali inatarajia kuwapangia shule wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwezi ujao.
 Alisema, utaratibu wa kupanga shule utaanza kuanzia Mei na majina na shule watakazopangiwa wanafunzi yatatangazwa mwishoni mwa mwezi huo na Julai wataripoti shuleni.
 
 “Utaratibu wa kupanga shule utafanyika kwa mfumo kulingana na ufaulu wa mwanafunzi, hivyo tunatarajia kutangaza shule walizopangiwa mwishoni mwa Mei kabla ya kuanza shule Julai, lengo la kutangaza mapema ni ili watumie mwezi mmoja kujiandaa,” alisema Sagini.
 
UHABA WA CHAKULA MASHULENI
Kuhusu uhaba wa chakula mashuleni, Sagini alisema serikali ina mpango wa kufanya upya tathmini ya gharama za chakula shuleni kama zinakidhi mahitaji ili kuwaongezea bajeti mwaka ujao wa fedha.
 
 Alisema pia serikali ina mpango wa kupeleka fedha za chakula moja kwa moja kwenye akaunti ya shule badala ya kupitia kwenye halmashauri ili fedha hizo zifike kwa wakati.
 
“Kwenye suala la kukabiliana na njaa shuleni pia tunachangamoto ya kuongezeka kwa shule na wanafunzi, tutafanya tathmini ili kuona namna ya kuongeza kiwango cha fedha ili kutosheleza mahitaji ya chakula mashuleni na hii itakuwa kwenye mpango wa bajeti ya fedha kwa mwaka ujao,” alisema Sagini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!