RAIS Jakaya Kikwete ametunuku watu 42 nishani akiwamo askari wa kike, Koplo Laura Mushi (32) kwa ushupavu alioonesha baada ya kupambana na kujiokoa dhidi ya majambazi waliomvamia hivi karibuni katika kituo cha ulinzi Mikumi, Morogoro.
Askari huyo alitunukiwa nishani sanjari na viongozi mbalimbali wakiwemo wastaafu, katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni nishani ya kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano.
Vile vile, Rais Kikwete alimtunuku Jumanne Ngoma nishani kwa ugunduzi wa madini ya tanzanite. Ngoma alikuwa mtunukiwa pekee katika kundi la wananchi wazalendo, ambao kwa vitendo na tabiawameipatia sifa na heshima kubwa Jamhuri ya Muungano.
Askari shupavu Askari huyo alitunukiwa nishani ya ushupavu kwa kuelezewa kwamba, alivamiwa na watu hao waliosadikiwa kuwa majambazi ambao walimfunga kamba shingoni na kuanza kumburuza kuelekea porini.
Katika maelezo yaliyosomwa kabla ya Rais Kikwete kumtunuku nishani, ilielezwa kwamba Machi 14 mwaka huu, saa 7:56 usiku akiwa katika kituo cha ulinzi na silaha aina ya sub machine gun ikiwa na risasi 30 ndani yake, alivamiwa na watu wasiojulikana.
Walimkaba shingoni kwa kamba na kuanza kumburuza kuelekea eneo la pori lililoko karibu na kituo hicho cha ulinzi. Wakati anaburuzwa kwa lengo la kumuua na kumnyang’anya silaha aliyokuwa nayo, alijitahidi kuzuia kamba hiyo ili aendelee kupumua wakati huo huo akidhibiti asipokonywe silaha hiyo.
“Ukiwa katika hali hiyo ya kukabwa shingo, uliweza kufungua usalama wa bunduki uliyokuwa nayo na kupiga risasi nne. Hali hiyo ilisababisha wahalifu hao kuacha kukuburuza na wakakimbia kusikojulikana,” alisema……. “Kitendo ulichofanya kilikuwa ni cha kishupavu na kizalendo na kiliwezesha kuokoa maisha yako pamoja na silaha hiyo.
Aidha kitendo hicho kimeleta heshima kubwa kwa jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla. Kwa kutambua kitendo hicho cha kishupavu, mimi Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakutunuku nishani ya ushupavu”.
Kwa mujibu wa wasifu uliosomwa kabla ya Rais Kikwete kumtunuku nishani, askari huyo alizaliwa Agosti 23 katika Kata ya Kimangeni tarafa ya Kifumbu, wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Okeseni iliyoko Moshi Vijijini kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1997 na ya Sekondari katika shule ya Shimbwe kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001.
Alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 2003 na kufanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili. Mwaka 2007 alijiunga na JWTZ.
1 comment:
Hongera sana piga kazi
Post a Comment