Katika toleo letu la jana kulikuwa na habari iliyomuhusu mwanamke mmoja wa Dodoma ambaye alikuwa amepelekwa kituo cha afya cha Muungano wilayani Chamwino kwa ajili ya kujifungua, lakini akakutana na vitendo vya kikatili vilivyochangia mtoto afie tumboni.
Kwa mujibu wa habari hiyo, muuguzi aliyekuwa zamu siku hiyo aliamua kumchapa viboko mjamzito huyo baada ya kumuona anashindwa kujikakamua ili kumsukuma mtoto atoke na alikuwa akifanya hayo akidai kuwa mwanamke huyo ni mzembe na anadeka ndio maana alikuwa anashindwa kujifungua.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikiri kuwapo kwa taarifa za mama huyo kuchapwa viboko akiwa chumba cha kujifungulia na kwamba wameagiza uchunguzi ufanyike ili kupata taarifa sahihi za tukio hilo na hatua zichukuliwe.
Wakati uchunguzi huo ukifanyika, hatutaki kuamini kuwa kifo cha mtoto huyo kimesababishwa na kupigwa kwa mama yake, lakini kinachotushangaza ni jinsi mama huyo alivyoshughulikiwa hadi kupoteza kiumbe hicho alichokitunza tumboni kwa miezi tisa.
Muuguzi huyo ni mmoja tu kati ya wengi ambao wamekuwa wakiwafanyia vitendo visivyo sahihi wagonjwa wanapoenda hospitalini kwa ajili ya kupata tiba, hasa wajawazito ambao hulundikiwa mzigo wa maneno kuanzia wanapofika hadi wanapojifungua. Imekuwa ni kawaida kwa kina mama wajawazito kusimangwa, kutolewa maneno machafu na kucheleweshewa huduma na matokeo yake baadhi hujikuta wakipoteza watoto na wengine kulazimika kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji.
Wengine wamekuwa wakilalamika kuwa wauguzi huwaomba rushwa na wasipotoa, hufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na kudhalilisha.
Mambo hayo husababisha wanawazito wanaoishi kwenye maeneo ya nje ya miji, kuona ni heri kujifungulia majumbani au kwa waganga wa jadi ambako wanaona hakuna unyanyasaji kama wanaofanyiwa hospitalini na matokeo yake hukumbana na athari kubwa zaidi.
Tunatambua kuwa wauguzi wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na Serikali kutotenga fedha za kutosha kwenye sekta hiyo, lakini hatuamini kuwa hali hiyo ndiyo inayosababisha wauguzi wafanye vitendo vya unyanyasaji kwa wagonjwa, na hasa wajawazito.
Tunaamini kuwa katika mazingira hayo magumu, bado wauguzi wanaweza kuonyesha moyo wa upendo, kufanya kazi kwa weledi na maadili angalau kwa kiwango kinacholingana na mazingira waliyonayo ili juhudi za kuhimiza kina mama wajifungulie hospitalini au kwenye vituo vya afya zizae matunda.
Itakuwa ni kitu cha ajabu kama Serikali inapiga kelele kuhimiza wananchi kwenda kwenye vituo vya afya au hospitalini wakati wauguzi nao wanafanya vitendo ambavyo vinakatisha tamaa wananchi kwenda sehemu hizo.
Wakati mama huyo akiendelea kupata matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, ni vizuri kwa uongozi wa mkoa kufanya uchunguzi wa kina kama ulivyoahidi ili kupata taarifa sahihi za tukio hilo lililotokea Aprili 3 mwaka huu, takriban siku 20 zilizopita.
Imekuwa ni kawaida kwamba tukio lolote baya likiripotiwa na vyombo vya habari, wahusika huwa wepesi kusema wanafuatilia kupata taarifa kamili na wanapoona hali imepoa, nao wanachana nalo na hakuna hatua zinazochukuliwa. Matokeo yake ni vitendo hivyo kuendelea kuwa sugu.
Hatutarajii kwamba uongozi wa mkoa wa Dodoma utaingia kwenye mkumbo huo wa kusubiri hali ipoe, bali utatekeleza ahadi yake ya kufanyia kazi taarifa hizo ili wahusika wachukuliwe hatua.
Na kwa kuwa huduma duni ni tatizo sugu hospitalini na kwenye vituo vya afya na hospitalini, Serikali haina budi kufuatilia vitendo hivyo ili kuvikomesha.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment