Friday 10 April 2015

Mgomo wa Madereva umeripotiwa kuanza asubuhi ya Leo sehemu mbalimbali Nchini - Jijini Dar, wananchi wametembea kwa miguu na wengine kupanda malori ya mchanga!


MADEREVA wa mabasi ya mikoani na daladala wa jijini Dar leo wamefanya mgomo kupinga agizo la Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) lililowataka kwenda kusoma katika Chuo cha Usafirishaji (NIT).


Mwandishi wetu amezunguka maeneo tofautitofauti jijini Dar na kujionea hali halisi ya mgomo wa mabasi ya mikoani pamoja na daladala za maeneo tofauti ya Jiji la Dar.
Mwandishi wetu pia aliweza kufika eneo la Stendi ya Ubungo na kujionea hali ilivyokuwa asubuhi na kuzungumza na baadhi ya madereva ambao walikuwa na kauli tofautitofati kuhusiana na mgomo huo.
Mmoja wa madereva ambaye alijitambulisha kwa jina la Ally Abdallah Shalon anayefanya kazi zake kati ya Dar es Salaam na Dodoma, alisema kuwa sababu kubwa ya kutokufanya shughuli zake ni kutokana na kikao ambacho walipanga kukifanya leo kujadili agizo la Sumatra lililowataka waende shule kusoma.
Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Khamis anayefanya shughuli zake kati ya Mwanza na Dar es Salaam alisema sababu iliyomfanya agome ni kupinga sheria mpya ya Sumatra iliyopitishwa na jeshi la polisi kuwataka madereva wote wa abiria (Pasangers Services Vehicle) kwenda kusoma kozi ya miezi miwili kwa gharama ya shilingi laki tano.
Khamisi alisema sheria hiyo inawabana sana madereva kwani moja kati ya vipengele vya sheria hiyo imeeleza kuwa, dereva yeyote atakayekamatwa akiwa amezidisha mwendo kasi hakuna faini yoyote bali unapelekwa mahabusu kwa muda wa siku kumi na nne baada ya kumaliza siku hizo, anapelekwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
“Hii sheria inatubana sana, mtu ukihitaji kubadilisha leseni yako ikipitwa na muda unatakiwa kurudia tena kwenda kusoma darasani kwa muda wa wiki mbili kwa ada isiyopungua laki tano na kuendelea kitu ambacho kinatuumiza sisi madereva,” alisema Khamis.
MUSOMA
Huko Musoma, abiria zaidi 1000 waliokuwa wakisafiri kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam kupitia mkoani Mwanza na Shinyanga na wale wa kwenda mpakani mwa Tanzania na Kenya pamoja na wa ndani ya Mkoa wa Mara wameshindwa kusafiri baada ya madareva kuitisha mgomo leo.
KIBAHA
Zaidi ya mabasi 10 kutoka mikoa ya kanda ya ziwa yamekwama huko Kibaha mkoani Pwani kutokana na mgomo wa madereva leo.
BUKOBA
Mabasi yote ya abiria yaliyotoka Bukoba Mjini leo asubuhi kuelekea Dar, Mwanza na kwingineko yamezuiliwa wilayani Muleba kutokana na mgomo wa madereva unaoendelea nchini kote. Abiria wamerudi mjini Bukoba kurudishiwa nauli zao na kuahirisha safari.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!