Monday, 20 April 2015

IGP: MASHEHE YAKEMEA UHALIFU


MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu na viongozi wa dini ya Kiislamu nchini, wameungana kukemea vitendo vya uhalifu nchini.

Wamezitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza katika vitendo hivyo. Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na IGP Mangu na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu katika mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao katika kuimarisha usalama nchini.
Kaulimbiu ya mafunzo hayo ilikuwa “Amani na usalama ndio maisha yetu”. Mafunzo hayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu hapa nchini.
Mangu alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa katika kuhakikisha vitendo vya uhalifu, vinadhibitiwa nchini kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Alisema wahalifu wa sasa wana mbinu nyingi, hivyo kitu kikubwa kitakachoweza kusaidia katika mapambano hayo ni mshikamano wa dhati kutoka kwa viongozi hao katika kuwafichua ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwakilishi wa Shehe Mkuu wa Tanzania katika kikao hicho ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Ulamaa katika Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA), Shehe Abubakar Zuberi alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani, ambazo zimeanza kujitokeza hapa nchini.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia zao na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kubaki salama kwakuwa amani tuliyonayo ni neema ambayo tunapaswa kuilinda kwa nguvu kubwa.
“Vilevile hatuna budi kuimarisha malezi katika familia zetu maana tunaposhindwa kuwalea watoto wetu vizuri ndio chimbuko la kushamiri kwa vitendo vya uhalifu wa aina mbalimbali hivyo tujielekeze katika kutoa mafunzo bora katika familia,” alisema Shehe Zuberi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Shehe Khamis Mataka alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yoyote na hata ndani ya msikiti hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu walio ndani ya misikiti.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyi Baraka, Shehe Issa Othman alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo viongozi wa dini waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!