Mbunge Amina Abdallah Amour (CUF-Viti Maalum), ameitaka serikali kuwalinda watoto kufuatia wimbi la utekaji na uuaji unaofanywa dhidi yao hususan wale wenye ulemavu wa ngozi.
Kadhalika amehoji kwanini watoto wanaopotea kwenye miji mikubwa, ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, taarifa za kutoweka kwao zinatangazwa kwenye vyombo vya habari, lakini habari za kupatikana kwao haziripotiwi.
Amina aliuliza swali hili la msingi kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, akitaka kufahamishwa mkakati wa serikali, katika kuondoa tatizo la upotevu kiholela wa watoto.
Akijibu Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pindi Chana (pichani), alikiri kuwa vyombo vya habari vinatangaza zaidi habari za watoto kunaopotea kuliko wanaopatikana, hali aliyoihusisha na mwamko mdogo wa watoa taarifa, kutotoa mrejesho watoto wao wanapopatikana.
Kwa mujibu wa Chana, sababu za kupotea watoto ni nyingi, ikiwamo baadhi ya wanandoa kunyang’anyana watoto, ndoa zinazo legalega na uvunjifu wa amani hivyo watoto kutoroka ili kutafuta mahali salama pa kuishi na wakati mwingine watoto kulelewa na walezi wasiyokuwa na uwezo wa kuwalinda kama vile bibi na babu.
“Ulinzi wa watoto ni mtambuka, lakini ni jukumu la kwanza kwa mzazi, akisaidiwa na jamii iliyomzunguka , serikali kuu na za mitaa kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema Chana.
Alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa watoto, imeunda Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi wa Mtoto na inaendelea kuratibu uundaji wa Timu ya Ulinzi wa Mtoto katika ngazi za wilaya na kata zote nchini
No comments:
Post a Comment