Aidha, Rais Kikwete ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa maofisa wote wa serikali ambao wanahusika kulipa mishahara hewa kwa watumishi ambao wameacha kazi, wamefariki, wamestaafu na wanaendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao za benki.
Rais pia ameiomba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuisaidia serikali kuboresha mfumo wa zabuni ambako serikali inapoteza fedha nyingi kwa kupitia mchakato mrefu mno wa kupatikana kwa wazabuni wa kutoa vifaa na huduma kwa Serikali.
“Naagiza kuwa tutume ujumbe wenye nguvu za kutosha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alitoa agizo hilo baada ya kupokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, mwaka jana katika hafla iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, jana.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kujulishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad, kuhusu alichokigundua katika ukaguzi wake kuhusu usimamizi na matumizi ya fedha za serikali. Mambo mengine yaliyogunduliwa ni malipo yasiyokuwa na nyaraka, hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha iliyotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa (nugatory expenditure) na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maafisa masuuli.
Profesa Assad alimweleza Rais Kikwete pia kuwa Ofisi yake inapendekeza kuwa taasisi zote za serikali zisiendelee kununua vifaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EDF), stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Kwa wale ambao wanatumia fedha za serikali vibaya wachukuliwe hatua. Wenye ushahidi wa waziwazi wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kwa wale ambao hakuna ushahidi wa kuweza kuwafikisha mahakamani lakini wamekula fedha za serikali wachukuliwe hatua nyingine kama vile kuachishwa kazi kwa manufaa ya umma, ama kushushwa vyeo ama kuchukua hatua nyingine za kiutawala,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, Profesa Assad amemwambia Rais Kikwete: “Ukaguzi wangu pia umebaini kuwa watumishi waliocha kazi, waliofariki, waliostaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao. Vile vile, fedha za makato ya mishahara ya wafanyakazi hao zimeendelea kupelekwa kwenye taasisi husika kama vile Bima ya Taifa ya Afya, Mamlaka ya Mapato na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.”
Profesa Assad alisema kuwa tatizo hilo linaendelea kuwepo hata kama linapungua kwa sababu ya mfumo wa udhibiti ambao serikali imeanzisha na kuwa kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, mwaka jana, 2014, kiasi cha Sh. Bilioni 141.4 zilitumika kulipa watumishi hao hewa.
CAG amewasilisha Ripoti yake kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na pia kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008.
Profesa Assad, amewasilisha ripoti tano zikiwamo za Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, Miradi ya Maendeleo na Ripoti ya Ufanisi (Value for Money Audit).
Rais Kikwete alimshukuru Mkaguzi Mkuu na watumishi wengine wa CAG kwa kuwasilisha ripoti yenye ubora wa kiwango cha juu na ameahidi kuwa ataiwasilisha Ripoti hiyo Bungeni Jumatatu ya Machi 31 ili ipate kujadiliwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment