Saturday 28 March 2015

NATAMANI NINGEMWAMBIA RAIS MAMBO HAYA MATATU



Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watatu wa Mzee Hussein aliyepanga eneo la Kipunguni, Ilala jijini Dar es Salaam.
Hasiti kusema kuwa familia yake inaishi katika maisha duni. Kwa mfano, anasema ili maisha yaende mama yake ameamua  kuuza pombe za kienyeji eneo la Gongolamboto, huku  baba yake wa kambo akiwa ni dereva wa moja ya magari yanayosambaza bidhaa za kampuni ya Said Salim Bakhresa.

Ni mfano wa watoto waliozoea hali ya ugumu wa maisha, kwani kipato kinachoendesha familia yao ni kidogo hali inayomfanya asome katika mazingira magumu. Kila siku asubuhi hukabidhiwa Sh1,200 tu kwa usafiri wa  mabasi ya daladala na pia  chakula awapo  shuleni.
Anaitwa Juma Hussein, mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, ambaye mara kadhaa huonekana kwa sura ya unyonge licha ya kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wanaoongoza kwa ufaulu darasani.
Mwananchi ilimwomba kuzungumza naye  baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kuelezea mfumo wa damu unavyofanya kazi mwilini mbele ya Rais Jakaya Kikwete.
Tukio hilo lilifanyika siku kadhaa zilizopita ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa sera mpya ya elimu nchini. Shule hiyo ilichaguliwa na Rais kwa kigezo cha kutimiza ahadi ya ujenzi wa maabara zote katika muda uliopangwa.
Uso kwa uso na Rais Kikwete
Kwa lugha ya mazingira ya kishule, Juma anaweza kuambiwa kuwa siku hiyo alijizolea ‘ujiko yaani sifa . Hii siyo kwa kukutana na kiongozi wa nchi, lakini pia kwa kumvutia kutokana na maelezo fasaha aliyokuwa akimweleza kuhusu mada ya mfumo wa damu unavyofanya kazi mwilini.
Kwa hakika alimshangaza Rais na watu waliombatana naye siku hiyo, huku yeye mwenyewe akisema ujasiri wa kuzungumza mbele ya Rais na wageni wengine maarufu kwa mara ya kwanza ulitokana na kujiamini.
“Nilimwona Rais Kikwete kama mtu wa kawaida kama wengine waliokuwa kwenye tukio lile. Hali hiyo ilinisaidia kufanya vizuri, kwani kama ningemchukulia kama kiongozi wa nchi labda ningeogopa na kufanya vibaya, lakini nashukuru kazi ilifanyika vizuri tu.”
Akiwa na sura ya kinyonge na hulka ya kuzungumza taratibu, Juma anasikitika kuwa fursa aliyopata ya kukutana uso kwa uso na Rais Kikwete, hakuitumia kumweleza mambo matatu anayoamini ni muhimu hasa katika fani za uhandisi na Tehama. Ni mambo gani hayo?
Anasema: “Ningemwomba ahakikishe anaondoka madarakani akiwa ameacha shule zote za sekondari zikiwa na maabara za masomo ya sayansi, walimu wa kutosha na kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanafunzi wenye ndoto za kusoma sayansi,’
Siri za mwanafunzi kufanya vyema
Juma anasema zipo njia mbili tu zinazoweza kumsaidia mwanafunzi yeyote yule nchini kufanikiwa katika ndoto zake za kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Njia hizo anataja kuwa ni juhudi binafsi na mchango wa mazingira yanayomzunguka mwanafunzi.
“Kwanza ni kuamua kupenda somo lenyewe, hali ya kupenda inajengwa na hisia za mwanafunzi mwenyewe, hivyo unaweza kuhamishia hisia zako kwenye masomo hayo. Ukifanya hivyo itakuwa hatua ya kwanza na muhimu sana,” anasema na kuongeza:
“Najua mwanafunzi anaweza kuathiriwa na ugumu wa maisha nyumbani, lakini hali hiyo lazima aichukulie kama changamoto na pia iwe kama hasira kwake ya kujituma zaidi, kujisomea na kuwekeza nguvu na muda mwingi akifikiria masomo. Mimi kama ningefikiria sana changamoto za familia yangu nisingeweza kuwa na juhudi hizi.”
Kuhusu sababu ya pili ambayo ni mazingira yanayomzunguka mwanafunzi, anatolea mfano wa masomo ya sayansi ambayo wanafunzi hawawezi kufanya vizuri kama hakuna mazingira bora kama vile miundombinu ya maabara na ushiriki wa wazazi katika kuhamasisha watoto.
Anaongeza: “Kuna mchango mkubwa unaohitajika kutoka serikalini kuhakikisha inaandaa walimu wa kutosha katika masomo ya sayansi nchini nzima na kuweka maabara za kutosha.”
Anasema mwanafunzi anaweza kuwa na dhamira, nia ya kusoma lakini kama hakuna miundombinu mizuri ndoto zinaweza kupotea.
Wosia kwa wanafunzi
Kwa upande mwingine, Juma anasema jitihada za ujenzi wa miundombinu shuleni na uwekezaji wowote wa elimu unaofanywa na Serikali, vinaweza kukosa tija ikiwa wanafunzi hawana ari ya kujifunza.
“Huwezi kupenda sayansi halafu ukachagua rafiki anayependa michezo tu shuleni au unakuwa na rafiki asiyezingatia masomo na tabia zake ni chafu, haifai kabisa,” anaeleza.
Mchango wa familia yake
Juma anasema japo familia yao ni ya kipato cha kawaida, baba yake mlezi, aliahidi kumsaidia kielimu ili atimize ndoto yake ya kufika chuo kikuu. Anashukuru kuwa familia yake imeamua kumpa msaada wa kutimiza ndoto zake.
“Najua mama hawezi lakini baba aliniambia atanisaidia kwa nafasi yake mpaka nitakapofanikisha ndoto zangu. Ndoto zangu ni kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Bailojia ili baadaye nije kuvaa kofia ya udaktari, kwa sababu ninaliweza kwa kiwango kikubwa somo la Baiolojia.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!