skip to main |
skip to sidebar
MIKINDANI ULIVYOSAHAULIKA NA VIVUTIO VYA KIKOLONI
‘ Wito wangu kwa serikali ya Mkoa wa Mtwara ni kwamba wawahimize wafanyabiashara kujenga mahoteli yenye hadhi ya kitalii ili kuweza kuwalaza watalii watakaokuja kutembelea vivutio vya Mkoa wao.
UFAHAMU mdogo wa Watanzania katika kutambua kuwa Mtwara kuna vivutio vya utalii ndiyo unanifanya kuweza kuandika makala haya kwamba sasa wanaweza kufanya utalii katika mkoa huo.
Ukivuta fikra na mtazamo na kurudi nyuma zaidi ya miaka 50 wakati wakoloni wakiwa hapa nchini, mji wa Mikindani ulikuwa na sifa ya kihistoria uliojiwekea ambao una barabara nyembamba ambapo pembeni yake kuna nyumba za ghorofa mbilimbili mwonekano wake ni kama mji wa Zanzibar na upo kilometa 10 kutoka Mtwara mjini.
Mji huo uko kando kando ya ghuba ya Mikindani ambapo kuna utulivu katika ukanda wa kusini ya bandari ya Mtwara, umepambwa katika vilima ambavyo vimesheheni nyumba za kienyeji za makuti na baadhi yake zimeezekwa kwa bati. Na wakati ukielekea makao makuu ya mkoa utakutana na vitalu vya mashamba ya chumvi.
Kuna usemi unaosemwa maana ya neno, Mikindani kulikuwa na gereza kubwa katika eneo hilo ambapo kulikuwa na Watanganyika ambao walikuwa na asili ya kiasia ambao walikuwa wanashindwa kutamka Muweke ndani mhalifu na badala yake walitamka 'Mekendani,' wazungu wakashindwa nao kuita hivyo wakaita 'Mikindani.'
Hata hivyo wenyeji wengine wanasema kuwa neno hilo lina maana ya mchikichi mchanga yaani 'mkinda' ukiwa mmoja na katika eneo hilo ilikuwepo mingi na mtu alipokuwa anatoka eneo jingine na kuelekea huko alisema kuwa anakwenda 'Mikindani' yaani katika eneo lenye Mikinda mingi hatimaye jina likapatikana mpaka leo.
Mji huu umekuwa ukifahamika kidogo kwa watu walio wengi wa ndani ya nchi hata nje ukizingatia historia uliokuwa nao kama kuwa bandari ya kwanza ya mwambao wa kusini mwa Tanzania na kuwa mji mkongwe kabisa kama ilivyo Kilwa, Bagamoyo, Pangani, Lindi na Mafia.
Bodi ya Utalii Tanzania ndiyo yenye jukumu la kutangaza na kuwaelekeza wananchi juu ya vivutio vilivyopo nchini lakini pia watalii kutoka nje kuwapa taarifa kama hizo, hata hivyo tayari wameshaanza kutangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi yetu.
Aidha nilibahatika kuongea na afisa husiano Bw.Geofrey Tengeneza, ambapo alithibitisha kuwa kutokana na kukua kwa mji wa Mtwara na uwekezaji wa gesi na mafuta unaokuwa kwa kasi wameshaanza kuwaonyesha na kuwaeleza watalii wa ndani na nje kuwa Mtwara pia kuna vivutio vya kitalii ambavyo watu wanaweza kutembelea.
"Tulianza na kufufua jengo la Wajerumani yaani lililokuwa boma na vivutio vingine vya kitalii Mikindani na Mtwara yote...kuna vivutio vingi katika Mkoa huu wa Mtwara ambavyo tunatakiwa kuvitangaza ili wananchi wavifahamu na kufanya utalii wa ndani," anasema Bw.Tengeneza.
Anasema kuwa Bodi ya utalii Tanzania imekuwa ikijitahidi kuandika habari za vivutio vya utalii vilivyoko hapo Mtwara katika majarida ya Tantravel, Tanzania Asilia na lingine jipya la Hardventure Tourism ambapo yanasomwa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia watalii wa ndani na nje pia.
"Tumekuwa tukiandika habari za vivutio vya utalii hapo Mtwara na mimi mwenyewe mwaka jana nilithubutu kuja hapo Mikindani na nikaandika habari za vivutio vya utalii kwa ujumla ili kuwajulisha wananchi sehemu za kutembelea," anasema Tengeneza na kuongeza kuwa,
"Wameweza kutangaza katika vyombo vya habari vya nje kama CNN Domestic, CNN Internatinal, lakini pia katika ligi ya mpira wa miguu ya Uingereza katika viwanja mbalimbali matangazo ya utalii wa Tanzania yanaendelea kutangazwa," anasema.
Aidha, anatanabaisha kuwa wameweza kutangaza hata katika treni, teksi, mabasi na maonyesho mbalimbali yanayofanyika katika nchi za kigeni kama Uingereza na Marekani kwa lengo la kuvutia watalii wengi kuja Tanzania lakini pia wenyeji wa Tanzania walioko katika nchi hizo kuona sehemu za kuja kutembelea wawapo nchini kwao.
"Inafurahisha kuona fukwe nzuri pamoja na nyumba zilizojengwa na mawe ya baharini na hii ni ishara tosha ya kuona utamaduni wa ujenzi wa kiarabu, anasema Bw.Simon Matekete mkazi wa Mtwara katika eneo hilo la Mikindani.
Anasema kuwa hapo ndipo palipofufuliwa lile boma lililokuwa ngome ya Wajerumani na sasa inajulikana kama Hoteli ya Old Boma, kwa ujumla ghuba ya Mikindani ni kubwa ambapo ni bandari ambayo imetunzwa vizuri katika ukanda wa kusini mwa Tanzania inayosheheni na ni rahisi kuzifikia fukwe bora na hifadhi za viumbe wa baharini.
Anasema kuwa Mikindani ni mji mkongwe unaofurahisha kwa mitaa yenye kona kona na mandhari ya kiafrika iliyojengwa kwa ujenzi wa Kiarabu na Kiingereza.
Akizungumzia mandhari ya eneo hilo anasema kuwa ni mwendo wa nusu siku kutoka Mikindani kwenda kutembelea hifadhi ya Lukwika Lumesule ambayo imetembelewa mara chache barani Afrika kwa taarifa za kitalii kutoka bodi ya utalii Tanzania;kuna makundi ya tembo wakihama kutoka mto Ruvuma.
Lakini pia ni nyumba ya simba, chui, viboko, mamba, swala na wanyama wengine wengi ambao wanapatikana katika hifadhi na mbuga za taifa zilizoko upande wa kaskazini ya nchi yetu; kuna michezo ya kuogelea kwa kutumia vifaa vya kutembea juu ya maji kutoka ghuba hiyo ya Mikindani mpaka kijiji cha kihistoria cha Pemba na zaidi ya hapo.
Michezo hiyo imekuwa ikichezwa zaidi ya miaka 100, kwa hiyo ni nafasi yako ya kucheza juu ya maji kwa kutumia vifaa hivyo vya kitamaduni.
Mbali na vivutio hivyo, Mikindani ulikuwa mji muhimu wa kibiashara kuanzia karne ya 15 na Dkt.David Livingstone aliwahi kunukuu katika kumbukumbu zake kuwa ni moja ya bandari nzuri katika mwambao wa pwani; baada ya hapo kwa bahati mbaya ikajawa na mchanga hivyo kushindwa kutumika kwa shughuli za kibandari.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bi.Jamadi Abdallah anasema kuwa halmashauri ina mfano kabambe wa kuweza kuutangaza mji wa Mikindani kama mji wa kitalii ambao umesheheni vivutio mbalimbali na historia ya mwambao wa maisha ya watu wa pwani.
Anasema kuwa wana mpango wa kuyafanyia ukarabati majengo ya kihistoria ya kale yaliyopo katika maeneo hayo lakini pia wana mpango wa kutafuta mwekezaji wa ndani ili kuweza kuuendeleza mji huo wa kale.
"Tuna mpango wa kuutangaza mji huu wa Mikindani lakini tunaanza kwa kufanya ukarabati wa majengo ya kihistoria ya kale na kuweka kumbukumbu zingine za kale," anasema Bi. Abdallah.
Anatoa wito kwa wananchi kutembelea Mkoa wa Mtwara na kuona hali halisi ya utalii na mazingira ya uwekezaji unaoendelea kwani baaadaye wanategemea kupokea watalii wengi wa ndani na nje kwa lengo la kuona vivutio lakini pia shughuli za gesi.
Anashauri viongozi wa Mkoa kuhimiza wafanyabiashara kuwekeza katika kujenga hoteli za kitalii na kuanzisha makampuni ya kusafirisha watalii kuingia Mtwara na kuwatembeza maeneo ya vivutio na hata kuwapeleka mikoa jirani.
"Wito wangu kwa serikali ya Mkoa wa Mtwara ni kwamba wawahimize wafanyabiashara kujenga mahoteli yenye hadhi ya kitalii ili kuweza kuwalaza watalii watakaokuja kutembelea vivutio vya Mkoa wao," anasema Bw.Tengeneza.
Ningependa kuwashauri Watanzania kuwa siyo gharama kubwa kufanya utalii wa ndani, kwani kwa kufanya hivyo utaweza kuwa balozi wa vivutio ambavyo vipo ndani ya nchi yetu popote pale uendako, isije ikawa
kichekesho pindi Mtanzania anapokwenda Kenya au Uganda na kuulizwa habari za utalii wa Mtwara na kutofahamu wakati wao walishafika nchini.
No comments:
Post a Comment