WAKATI jamii ikipambana kuzuia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), imebainika kuwa licha ya tishio hilo la kuawa lakini pia wamekuwa wakifanyiwa vitendo wa ukatili ikiwemo kubakwa.
Mwandishi wa gazeti hili, Machi 10, mwaka huu alitembelea kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu wa ngozi cha Buhangija Jumuishi kilichopo Manispaa ya Shinyanga na kukutana na binti mwenye umri chini ya miaka 18 ambaye alifanyiwa ukatili kwa kubakwa na wanamume watano.
Binti huyo Lucy Mahona (17), (si jina lake halisi) ambaye pia ni mlemavu wa kusikia na kuongea alibakwa na wanamume watano akiwa kijijini kwao, wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Mmoja wa walezi wa kituo hicho, Maisara Adinani anasema alipofikishwa kituoni hapo mwaka jana mwezi wa sita walimkadiria kuwa na miaka 16 kutokana na mama yake kushindwa kujua umri sahihi wa mtoto huyo .
“Tulimpokea mwaka jana mwezi wa sita ambapo aliletwa na mama yake mzazi akiwa pamoja na kaka zake watatu ambao pia wana ulemavu wa ngozi. Pamoja na kwamba ana ulemavu wa ngozi lakini pia hasikii wala hazungumzi, ndiyo ameanza kujifunza lugha ya alama.
“Tulipompokea hatukujua kama ni mjamzito ndiyo baadaye tukashituka, tulipodadisi vyema kwa mama yake akatusimulia jinsi mtoto wake huyo alivyofanyiwa ukatili na wakati huo alikuwa na ujauzito wa takribani miezi mitano,” anasema Maisara.
Maisara anasema kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo ni kwamba mwanaye alibakwa wakati yeye na baba yake wakiwa shamba ambalo liko mbali.
Anasema walipopata maelezo hayo walimfikisha kituo cha afya ambako alifanyiwa uchunguzi na kukutwa na magonjwa ya ngono na vipimo hivyo havikumkuta na maambukizi ya Ukimwi.
Maisara anasema mama wa binti huyo aliwaeleza namna alivyotoa taarifa za kufanyiwa ukatili huo Polisi wilayani ambapo hata hivyo hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa kutokana na unyama huo.
Anasema baada ya kuona hali si salama kwa watoto wake hao ndipo aliamua kuwafikisha kituo hicho cha Buhangija Jumuishi kwa ajili ya kupata ulinzi wa kutosha na wenye uhakika.
Mwandishi hakufanikiwa kupata jina la kituo cha polisi, mama huyo alipotoa taarifa za kubakwa mtoto wake kutokana na mlezi huyo kushindwa kuelewa pamoja na ufinyu wa mawasiliano uliopo kwa mzazi huyo.
Hivi sasa binti huyo ana mtoto asiyekuwa na ulemavu mwenye miezi mitano ambaye alijifungua Oktoba, mwaka jana.
Mwandishi alimshuhudia Lucy akizungumza kwa lugha ya alama ambayo hata hivyo bado hajaijua vyema, akielezea namna alivyobakwa na wanaume hao watano.
Pamoja na kulelewa katika kituo hicho akipatiwa mahitaji mbalimbali ya mama na mtoto, mlezi wa kituo anasema bado hakuna mazingira bora ya kumlea mtoto huyo akiwa hapo.
“Kama kuna mwenye uwezo ajitokeze kumsaidia kwani mazingira ya hapa si rafiki kwa mtoto, ajitokeze afuate utaratibu kwa ajili ya kumtoa hapa,” anasema Maisara.
Mbali na changamoto zinazomkabili Lucy pamoja na kulea mtoto mdogo akiwa hapo, Mwalimu Msimamizi wa Kitengo cha Watoto Wenye Ulemavu kituoni hapo Donald Nyanga anasema wapo watoto wengine wakiwa na umri wa miaka miwili.
“Ni changamoto kubwa mfano yule mtoto pale, (anaonesha mwanamke ambaye amekaa kwenye benchi akibembeleza mtoto) ameshindwa kumwacha mtoto kwani ni mdogo na anahitaji mapenzi ya mama yake, hivyo alipomleta jana tulimweleza kuwa akae hadi mtoto azoee sababu ni mdogo sana, hata hajui kuzungumza lolote,” anasema Mwalimu Nyanga.
Tunatembea kumfuata mama huyo ambaye anajitambulisha kama Kwangu Kulwa ambaye ni mama wa mtoto aliyembeba anayejulikana kama Itofali Emmanuel.
Anasema alilazimika kufunga safari ya kutoka katika kijiji cha Ikwililo, wilayani Maswa mkoani Simiyu kwa ajili ya usalama wa mwanaye huyo na kwenda kituoni hapo.
Anasema kila alipokuwa akisikiliza taarifa za habari aliingiwa hofu kuhusu mtoto wake huyo ingawa hakuwahi kupata tishio awali hivyo alifunga safari hadi kituoni hapo.
“Huyu ni mtoto wangu wa tano, hao wengine hawana ulemavu wa ngozi, nilivyosikia redioni na tayari hivi sasa kijijini kwetu watoto wengi wa namna hii wameondolewa na wazazi wao huku wengine wakihama, niliogopa na kumleta hapa mtoto wangu. Nimewakuta hapa hata majirani zangu huko,” anasema Kwangu.
Anasema roho inamuuma kwa kuwa analazimika kumwacha mwanaye mdogo kituoni hapo huku akiwa anahitaji uangalizi wa karibu wa mzazi.
“Kituoni hapa watoto ni wengi, serikali isaidie jambo hili ili tuweze kukaa na watoto wetu, tunaumia lakini kwa kuwa tunajali maisha yao inabidi iwe hivyo,” anasema Kwangu.
Baada ya maelezo hayo ya Kwangu, Mwalimu Nyanga anasema kituo hicho ambacho kina watoto zaidi ya 300 wakiwemo wasioona na wasioosikia huku wengi wakiwa na umri wa chini ya miaka 10 kina changamoto nyingi za kukiendesha.
Anasema tangu mauaji yaibuke tena wanapokea watoto kuanzia watatu hadi watano kwa siku huku kukiwa hakuna majengo ya kutosha kwa ajili ya watoto hao wanaolazimika kuishi kwenye majengo ambayo hayajakamilika vyema ujenzi wake likiwemo lililojengwa chini ya ufadhili wa aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2012, Brigitte Alfred ambalo halijakamilika.
“Mabweni yapo manne kati ya hayo yaliyokamilika ni mawili, kuna uhaba wa vitanda kwani kimoja wanalala watoto kati ya watatu hadi watano kama ni wadogo, upungufu wa vitanda, mashuka, neti na magodoro,” anasema Mwalimu Nyanga.
Chanzo:Mtanzania
No comments:
Post a Comment