Sunday, 15 March 2015

DUNIA HAIISHI VITUKO NYUMBA YAUZWA OFA MKE WA BURE!



UKISTAAJABU ya Musa utayaona ya firauni. Ni msemo ambao leo umedhihirika huko Indonesia.
Msemo huo umedhihirika, baada ya mwanamke mmoja ambaye ni mjane, kutangaza kuuza nyumba yake na kumpa ofa mnunuzi wa kupata mke bure kama atahitaji ‘huduma’ hiyo. Mwanamke huyo, Wina Lia mwenye miaka 40 ametangaza kuuza nyumba yake iliyopo Sleman, katika kisiwa cha Java, Indonesia.



Ameweka wazi kuwa mnunuzi wa nyumba hiyo, mbali ya kupata nyumba, pia anatoa ofa ya kukubali kuolewa naye. Hata hivyo, ofa hiyo sio ya lazima na mnunuzi anaweza kuikataa.
Tangazo hilo limesambazwa kwenye mtandao wa intaneti na kusababisha watu wengi kushangazwa. Kwenye tangazo hilo limeanza kama matangazo mengine ya kuuza nyumba, na kueleza sifa ya nyumba hiyo kuwa ni yenye ghorofa moja, vyumba viwili vya kulala, vyoo viwili, sehemu ya kusafisha gari na bwawa la samaki.
Tangazo hilo likaongeza kuwa ipo ofa maalumu kwa mnunuzi iliyoelezwa: “Ukinunua nyumba hii, unaweza kuomba muuzaji wa nyumba akubali kuolewa na wewe.” Pia tangazo hilo limewekwa na picha ya Wina ambaye ni mrembo. Mbali na nyumba, Wina pia anamiliki saluni ya kike na katika picha hiyo, amependeza akiwa ameegemea gari mbele ya nyumba yake.
Nyumba hiyo ipo kwenye kisiwa cha Java na inauzwa dola za Kimarekani 75,000. Tangazo limeweka wazi kuwa bei haipungui na wanatakiwa wanunuzi wenye nia ya kweli. Mmiliki wa mtandao wa intaneti wa Kaskus, anasema Wina ana akili na ni mjanja kwani anajua akiolewa na mnunuzi wa nyumba hiyo, ataendelea kuwa mmiliki.
Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, Wina amesema kuwa; “nimeshtushwa na jinsi watu walivyochukulia tangazo langu. “Nimeshangazwa na jinsi waandishi wa habari wanavyokuja kunihoji na hata polisi wamekuwa wakiniuliza maswali na wameniambia niende kuhakikisha habari hiyo wakidhani si sahihi, lakini nimewaambia sio kusudio langu kutoa tangazo hilo kama habari”.
Wina mwenye watoto wawili anasema alimuomba rafiki yake ambaye ni dalali la nyumba, amsaidie kutafuta mnunuzi na kwenye hatua hiyo pia amtafutie mume hivyo alitarajia tangazo hilo angelituma kwa watu wachache na si kuliweka kwenye mtandao wa intaneti.
“Nilimwambia rafiki yangu kuwa kama kuna mnunuzi wa nyumba ambaye hajaoa au amefiwa na mke na anataka nyumba na wakati huohuo anataka mke, anijulishe kwani mimi pia ni mjane,” anasema.
Anasema hadi sasa amejitokeza mnunuzi mmoja aliyetembelea nyumba hiyo. Hata hivyo Wina amekataa kutoa taarifa zaidi kama mnunuzi huyo kakubali na ofa hiyo ya ziada au la.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!