Saturday 21 February 2015

SERIKALI KUAJIRI WALIMU WA SEKONDARI 35 000

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini.

Pinda alisema hayo juzi mjini Iringa alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa Kata ya Kiwere, Tarafa ya Kalenga, baada ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu wa shule hiyo.

Alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji yaliyowasilishwa kuwataka wahusika kuzipa kipaumbele shule ambazo miundombinu yake imekamilika, ikiwamo vyumba vya maabara.
Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara, Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo tayari ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika.
“Mkuu wa mkoa inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo bado hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni, mwaka huu, kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Alisema hataongeza tena muda
wa ujenzi,” alisema Pinda.
Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Leonard Msigwa alisema ujenzi wa nyumba nne za walimu zitakazokaliwa na familia nne kila moja, umegharimu Sh323.2 milioni.
Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko,
Msigwa alisema nyumba hizo zimejengwa na Shirika la DESWOS la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na wananchi.
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Ofisa Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya masomo ua kemia na baiolojia na tayari mfumo wa gesi na maji umekwishafungwa ndani ya vyumba hivyo.
“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwishagharimu Sh52.8 milioni na mwezi huu tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya samani za maabara zikiwamo meza 24 na stuli 96,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!