Wednesday 11 February 2015

HATUA YA KENYA YA KUZUIA MAGARI YA TANZANIA IMETUSIKITISHA-MWAKYEMBE


Serikali ya Tanzania imesema itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wanaokuja  kutembelea vivutio vya kitalii kutumia viwanja vya ndege vilivyopo nchini ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia Kenya kuendelea kuzuia magari ya kitalii yaliyosajiliwa Tanzania kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa ajili ya kuchukua na kushusha watalii.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe (pichani), alisema  jana kuwa serikali imesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na  Kenya kwani uamuzi wake hauendani na dhamira njema ya mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dk. Mwakyembe alisema mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa ushirikiano katika sekta ya utalii kati ya nchi hizo na makubaliano yalielekeza katika kubadilishana watalii kwa lengo la kuondoa bugudha kwa watalii.
Alisema pamoja na kwamba Kenya inakwenda nje ya mkataba wa mwaka 1985, viwanja vya ndege vya Tanzania hasa vya kimataifa vitaendelea kuwa sehemu za kuingilia na kutokea kwenda kokote ndani au nje ya jumuiya na havitachukuliwa kama vivutio vya utalii.
 “Tanzania haitazuia magari ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi hizo,” alisema.
Alisema Tanzania itaheshimu na kuzingatia mkataba huo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi hizo wakati ikiendelea kutafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wanaopitia uwanja wa Jomo Kenyatta.
Aliongeza kuwa kutokana na uzito wa suala hilo, wizara yake iliona umuhimu wa kuhusisha Wizara za Uchukuzi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maliasili na Italii, Viwanda na Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ili kupata msimamo wa nchi wa pamoja kabla ya mkutano na Kenya. Alisema tatizo lililopo ni kwamba miaka 10 iliyopita Kenya walikuwa wanaipita Tanzania katika sekta ya utalii, lakini hivi sasa imekuwa ni karibu nusu kwa nusu na kwa Tanzania vivutio vya utalii vipo eneo moja, hivyo imekuwa utamaduni watalii kupitia Kenya kabla ya kuja Tanzania.
“Magari kuzuiwa hayatupi tumbo joto, wala halina impact (athari) kiuchumi, watalii wanapata usumbufu kidogo, tutaboresha viwanja vyetu vya ndege watakuwa wanapitia viwanja vyetu,” alisema.
Desemba 22 mwaka jana Kenya ilizuia magari ya kitalii yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!