Wednesday 11 February 2015

AMUUA MTEJA WA GARI NA KUFUKIA MAITI UANI



Mkazi wa Ilala Sharifu Shamba, jijini Dar es Salaam, anatuhumiwa kumuua rafiki yake kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulisakafia uani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.


Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
Inadaiwa kuwa marehemu alimpa mtuhumiwa huyo fedha hizo ili akamnunulie gari na kwamba, baada ya kudaiwa muda mrefu, ndipo alipoamua kufanya ukatili huo.
Habari zilizolifikia NIPASHE, zinaeleza kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa alimpigia simu rafiki yake huyo na kumtaka aende bandarini kuchukua gari hilo kwa madai kwamba, lilikuwa limewasili. 
Kwa mujibu wa habari hizo, wakati huo mtuhumiwa alikuwa bandarini akimsubiri rafiki yake huyo. Inadaiwa rafiki yake huyo  alikwenda hadi bandarini na kuonana na mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo, kilichotokea ni mtuhumiwa kumzungusha rafiki yake huyo bila kupata gari alilomuahidi.
Hali hiyo ilimfanya rafiki yake huyo kulazimika kuondoka baada ya kushindwa kuhimili mzunguko waliokuwa wakifanyiwa na mtuhumiwa. Baada ya kushindwa kupata gari alilolitarajia, mtuhumiwa aliamua kurudi na rafiki yake huyo nyumbani kwake (mtuhumiwa), Ilala ambako alitekeleza mauaji hayo na kumzika.
Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa mpangaji wa nyumba hiyo, ambaye ni kaka wa  Sheikh Sharifu, Abubakar Matonga,  alisema walihamia kwenye nyumba hiyo Novemba 17, mwaka jana na kwamba, wamekuwa wakiitumia kwa shughuli za maombezi.
 “Jana (juzi) walikuja watu wanne waliojitambulisha kuwa ni polisi. Walituhoji na kutuomba mkataba wa nyumba tulioingia na mwenye nyumba. Baada ya kuwapa mkataba huo, walituomba namba ya simu ya mwenye nyumba. Walipompigia simu, walimtaka aje kwenye nyumba yake,” alisema Abubakar.
Aliongeza: “Alipofika, polisi walisema kuwa nyumba hii ilitumika kwa mauaji yaliyofanywa na mpangaji aliyekuwa akiishi humu kipindi cha nyuma. Alihama mwezi wa saba, mwaka jana baada ya kufanya mauaji.”
Abubakar alisema polisi walisema mpangaji aliyekuwa akiishi katika nyumba hiyo alikuwa anadaiwa na marehemu zaidi ya Sh. milioni 30 alizopewa kwa ajili ya kumuagizia gari, lakini akakaa na fedha hizo zaidi ya mwaka bila kuonyesha hilo gari wala kurejesha fedha hizo.
“Fedha hiyo ilikaa kwa muda mrefu, takribani mwaka. Kutokana na kero za kumdai, siku moja mdaiwa akampigia simu mdeni wake na kumwambia gari limekuja bandarini, aende akamkabidhi pamoja na nyaraka muhimu,” alisema  Abubakar. Alisema polisi waliwaeleza kuwa, alipopigiwa simu, alimwambia rafiki yake waende wote ili akamsaidie kuendesha gari hilo. 
Abubakar alisema alipofika bandarini,  alizungushwa bila mafanikio yoyote.  Alisema rafiki ya marehemu alipoona mizunguko imezidi, alimuaga akamwambia akishapokea gari amjulishe ili amfuate.
Mmoja wa majirani, ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini, alisema polisi walifika jana (juzi)  eneo la tukio na kuwakusanya wananchi, wakiwamo wajumbe wa nyumba kumi, viongozi wa serikali za mitaa na kuwapa taarifa za mtu kuuawa na kufukiwa kwenye nyumba hiyo.
“Baada ya kutueleza, walianza kuchimba mlangoni ambako mwili huo ulifukiwa na kuutoa. Lakini mwili huo ulionekana ukiwa umefungwa fungwa na mito ya godoro  ambapo ilionekana miguu, mikono na fuvu,” alisema. 
Mjumbe wa nyumba kumi na Serikali za Mtaa Tawi la Amana, Kitongoji cha Sharifu Shamba, Christina Msala, aliwashauri wenye nyumba kwamba, wanapopangisha nyumba watoe taarifa kwa wajumbe wa eneo husika ili likitokea tatizo mtu afahamike hata kwa jina.
Juzi polisi Mkoa wa Ilala walifukua mwili huo baada ya kumkamata mtuhumiwa ambaye jina lake halijafahamika na kumhoji muda mrefu na baadaye waliuchukua mwili kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mary Nzuki, alipopigiwa simu jana, ilipokelewa na mtu alijitambulisha kuwa msaidizi wake, ambaye alisema bosi wake yuko kwenye mazishi ya watu sita walioteketea kwa moto wiki iliyopita katika maeneo ya Kipunguni.
Hadi tunakwenda mitamboni NIPASHE liliendelea kumtafuta Kamanda Nzuki, lakini simu yake haikupatikana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!