Sunday 1 February 2015

BI KIDUDE HAKUKUBALI KUOZESHWA AKIWA NA UMRI MDOGO


NI miaka miwili sasa tangu, Fatma binti Baraka maarufu kwa jina la ‘Bi Kidude’ alipoaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye kongosho.
Msanii huyo alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo visiwani Zanzibar katika familia ya watoto saba, baba yake mzazi, mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi.


Hadi anaaga dunia Aprili 16, 2013, Bi Kidude alikuwa hafahamu umri wake lakini kutokana na matukio ya kihistoria amewahi kukaririwa akisema kuwa, alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ni kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia iliyoanza mwaka 1914 hadi 1918.
Kabla ya msanii huyo kufariki dunia mara kadhaa mitandao ya kijamii ilikuwa ikimtangaza kwamba amefariki dunia kitu ambacho hakikuwa cha kweli. Bi Kidude ni miongoni mwa wasanii wakongwe nchini wenye historia ya kipekee na watakaokumbukwa kwa nyimbo zake na kwa namna alivyokuwa akiimba.
Bi kidude anaaminika kwamba ndiye msanii mkongwe kuliko msanii mwingine yeyote wa kike hapa nchini. Kupitia kazi zake za sanaa, aliwahi kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Asia kwa ajili ya kufanya kazi zake za muziki na kuitangaza nchi kwenye jumuiya ya kimataifa.
Katika moja ya matukio ambayo naweza kusema kwamba yalinivutia sana katika historia ya Bi Kidude ni ile ya kutoroka kuolewa akiwa na umri wa miaka 13. Alilazimishwa kuolewa akaamua kutoroka nyumbani kwao Zanzibar na kuamua kwenda Tanzania Bara. Uamuzi wa mwanamke huyo unatoa funzo kwa watoto waliopo shuleni kuiga mfano wake, wasikubali kuolewa, wazingatie masomo ili watimize ndoto zao.
Wapo watoto wanaokataa na kutoroka kama bibi huyo alivyofanya lakini wengine wanazidiwa na maamuzi ya wazazi wao hali inayochangia ongezeko la ndoa chini ya miaka 18 na mimba za utotoni. Historia inaonesha kwamba, Bi Kidude aliangaliwa kama malkia wa muziki wa taarab nchini ambaye kipaji chake kiligunduliwa na kuimarishwa na mkongwe wa muziki wa aina hiyo Siti binti Saad kati ya miaka ya 1880 mpaka 1950.
Bi Kidude alianza kupenda kuimba akiwa na miaka 10, alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba enzi hizo Sitti binti Saad ambaye alikuwa akiimba nyimbo zenye mahadhi ya taarabu. Inadaiwa kuwa wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa na uhusiano wa karibu yeye (Bi Kidude) alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti.
Wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani, yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wageni. Kwa kuwa Bi Kidude alibaki nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumuiga namna alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri katika uimbaji. Alisifiwa kutokana na sauti yake, katika miaka ya 1920 alianza kuimba na vikundi vya kiutamaduni.
Bi Kidude ni mmoja ya waimbaji wakongwe waliozunguka nchi zote za Afrika Mashariki akiimba taarab. Msanii huyo alitembelea miji mikubwa ya ukanda wa pwani pamoja na bara upande wa Ziwa Victoria na Tanganyika. Mwaka 1930, alirejea Dar es Salaam kutoka Kaskazini mwa Misri huko alipoenda baada ya ndoa yake kuvunjika hivyo alikwenda huko kupumzika.
Inadaiwa kuwa moja ya sababu ziliyochangia ndoa yake kuvunjika ni unyanyasaji wa kimapenzi aliokuwa akifanyiwa na mumewe. Baada ya kurudi Tanzania alijiunga na kikundi cha Egyptian Taarab alichodumu nacho kwa miaka mingi. Katika miaka ya 1940 alirudi Zanzibar na kujenga nyumba iliyokuwa ya matope na kuanza maisha mapya hapo.
Alikuwa maarufu kwa shughuli za unyago ambazo ziliwaandaa wasichana kuelekea katika maisha ya utu uzima. Ni mtaalamu wa mambo hayo ya mila kongwe akifanya hivyo kwa wasichana akitumia mafunzo ya kitamaduni kuwaelekeza wasichana namna ya kuishi na waume zao na kuepuka migongano ya kifamilia na unyanyasaji wa mapenzi.
Jina la Bi Kidude lilikuwa likisifika katika jamii yote ya Zanzibar na kuwa kielelezo cha utalii wa visiwa hivyo vya karafuu. Hoteli mbalimbali kubwa na zenye hadhi ya juu visiwani humo zimekuwa zikizipa majina migahawa na hoteli jina la Bi Kidude.
Bi Kidude alikuwa na upeo mkubwa wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za Kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, aliliona hilo katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni kutoka Arabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo kwa kutovaa hijabu, akaishi kama Mtanzania na si kama Mwarabu.
Si hivyo tu, msanii huyo pia alivunja miiko mingine zaidi ya kutokunywa pombe na kuvuta sigara. Bi Kidude alikuwa anakunywa pombe na alivuta sigara. Moja ya nyimbo zake ambazo zilitamba na kumpatia umaarufu mkubwa mkongwe huyo ni Muhogo wa Jang’ombe, aliuimba kwa Kiswahili na Kiarabu.
Bi Kidude ni hazina kubwa na mwalimu mzuri kwani inadhihirika kwamba wasanii wengi wamepata mafunzo kutoka kwake. Pamoja na umahiri umaarufu wake na kuwa kwenye sanaa kwa muda mrefu Bi Kidude hajawahi kukumbwa na kashfa yoyote hivyo amekuwa na historia ya kipekee tofauti na wasanii wa sasa.
Mwaka 1999 alipata tuzo ya Tamasha la filamu la nchi za Jahazi (ZIFF) ambayo ni tuzo ya maisha na Mwaka 2005. Bi Kidude alipewa tuzo ya heshima ya dunia WOMEX zilizobuniwa mwaka 1999 na ambazo wanazawadiwa watu ambao wamepata mafanikio makubwa katika muziki au wametoa mchango mkubwa katika muziki, umuhimu wa mtu katika jamii na hata, mafanikio ya kibiashara.
Kutokana na kazi zake za sanaa, Tanzania Bara na Zanzibar, Rais Jakaya Kikwete alitambua umuhimu wa mzee huyo na wasanii wengine kwa kuwatunukia nishani ya sanaa na michezo ambayo hutolewa kwa wasanii na wanamichezo mashuhuri, ambao kazi zao za sanaa au michezo zimeipatia sifa kubwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wasanii wengine waliopewa nishani hiyo ni pamoja na kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo ambaye naye ni marehemu, kiongozi wa zamani wa bendi ya Dar es Salaam International, marehemu Marijani Rajabu, aliyekuwa msanii maarufu wa maigizo na filamu nchini, marehemu Fundi Saidi ‘Mzee Kipara’ na mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.
Gurumo, Bi Kidude na Akwari walihudhuria hafla hiyo ya kuvishwa nishani zao na Rais Kikwete wakati nishani za Marijani na Mzee Kipara zilipokelewa na watoto wao. Bi Kidude hakuweza kwenda eneo la kupokea nishani kutokana na hali ya afya yake kutokuwa nzuri. Ilibidi Rais Kikwete amfuate mahali alipokuwa ameketi na kumtunukia nishani yake.
Bi Kidude amedumu kwenye fani ya uimbaji kwa zaidi ya nusu karne na kwa sasa ni msanii pekee wa taarabu mwenye sifa zilizotukuka kutokana na ukongwe wake na umahiri wake katika kuimba taarab. Kwa mujibu wa historia ya Gurumo, alianza muziki 1960 na kushiriki katika bendi mbalimbali kama vile Nuta, Atomic Jazz, Kiko Kids, Jamhuri Jazz, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, Mlimani Park, Juwata, Ottu na Msondo Ngoma.
Alitunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kuheshimu na kufanyakazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani na kuwaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kulea watoto na vijana kutimiza wajibu wao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!