Wednesday, 5 November 2014

WALEMAVU WANABAGULIWA KATIKA AJIRA


UTAFITI nchini umeonyesha nusu ya Watanzania wameshuhudia ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu katika ajira.

Utafiti huo ulifanywa na Taasisi ya Twaweza ni Sisi na kuonesha kuwa wananchi hao wameripoti kuwahi kushuhudia ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi alisema ni wananchi wawili kati ya 10 waliokiri kufahamu asasi na mashirika yanayotoa upendeleo katika suala la kuwaajiri watu wenye ulemavu.
“Wananchi waliripoti kuwa miongoni mwa mashirika haya asilimia 38 ni taasisi za kiserikali, lakini pia utafiti umeonesha kuwa watoto wenye umri wa kwenda shule ambao ni walemavu ila hawakuwa shuleni bado wapo wengi,” alisema Mushi.
“Vile vile asilimia 33 ya wananchi walionesha kuwaona watu wenye ulemavu kama siyo watu kamili au kuwa kikwazo kwao karibu nusu ya wahojiwa walionesha kuwaona watu wenye ulemavu kama mzigo kiuchumi kwa familia zao na wenye uzalishaji mdogo kuliko watu wasio na ulemavu,” alisema.
Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani alisema baadhi ya wananchi wamependekeza viti vilivyotengwa bungeni kwa ajili ya watu wenye ulemavu idadi yake iongezwe.
“Tunahitaji kuondokana na mtazamo huu wa kuwaona watu wenye ulemavu kama waathirika au mizigo na badala yake tuwaone kama watu wenye uwezo tofauti, wanaostahili heshima na haki ya kupata fursa sawa kama raia wengine,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!