KIONGOZI wa Chama cha Kisoshalisti kilichojulikana kama “NAZI” Adolf Hitler (1889-1945) alikuwa mmoja kati ya Madikteta dhalimu na mwenye nguvu kuwahi kutokea katika karne ya 20.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, mbabe huyo aliamka kwa nguvu kupitia chama hicho cha Wafanyakazi wa Ujerumani na kuchukua udhibiti wa serikali ya Ujerumani mwaka 1933.
Hitler aliamuru uanzishwaji wa kambi za mateso dhidi ya Wayahudi na makundi ya watu wengine huku akiamini kuwa kufanya hivyo ilikuwa chachu na tishio tosha dhidi ya ukuu wa himaya ya Aryani na hatimaye kusababisha vifo vya zaidi ya Wayahudi wapatao milioni sita.
Mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya nchi ya Poland mwaka 1939 ndiyo yaliyoanzisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambapo mpaka kufikia mwaka 1941 Ujerumani iliteka sehemu kubwa ya ardhi ya Ulaya na Afrika Kaskazini.
Ili kuepuka kukamatwa kwa kukwepa utumishi katika jeshi la Austria-Hungary, Hitler aliondoka toka Vienna na kuelekea Munich Mei 1913, lakini baadaye alilazimika kurudi.
Taarifa za kihistoria zinasema Kiongozi huyo wa Nazi alijiunga na jeshi la Bavaria na kuanza kufanya kazi za kujitolea ambapo mwaka uliofuata alishiriki kikamilifu katika vita ya Kwanza ya Dunia akiwa mstari wa mbele upande wa Magharibi ambapo uzoefu wake katika vita na mapambano uliathiri mawazo, fikra na mitazamo yake yote baada ya hapo.
Baada ya Vita Kuu ya kwanza ya Dunia, Hitler alichukua udhibiti wa chama hicho cha wafanyakazi wa Ujerumani kama kiongozi, hivyo aliamini kingemwezesha kushika dola ya Ujerumani.
Aliposhindwa kwenye jaribio la Mapinduzi la mwaka 1923 yeye na wenzake walikamatwa na kufungwa jela na baada ya kutoka jela alijitahidi kukijenga chama hicho na kuanza mikakati ya kukamata dola kwa njia zilizo halali.
Hitler alikusudia kufanya mageuzi na kuendesha sera za kibaguzi ambazo zingetoa nafasi ya kutosha kwa Wajerumani kuweza kuishi katika himaya kubwa duniani.
Kwanza alitabiri ingekuwa rahisi kuiteka Czechoslovakia, na kufuatiwa na Ufaransa ambayo ilikuwa kizingiti kigumu kwa wakati huo hatimaye kumalizia na nchi ya Uingereza.
Kwa mujibu wa mikakati ya Adolf Hitler, vita ya tatu ingefuata juu ya uvamizi dhidi ya Jumuiya ya Kisovieti ambayo kwake ulikuwa ni mtihani ambao alipanga afaulu kwa kufikiri vita ingepiganwa kwa haraka na kwa urahisi.
Kwa mujibu wa fikra zake za kuipiga Urusi, hii ingempa utajiri wa malighafi za kutosha hususan mafuta ambayo yangemwezesha kuandaa mkakati wa maandalizi ya vita ya nne dhidi ya Marekani.
Vita hiyo ingekuwa rahisi tu kwake endapo Ujerumani ingeweza kuwa na ndege ziwezazo kusafiri masafa marefu pamoja na meli za kivita na kwa upande mwingine ndege za kutosha na jeshi la maji kubwa na imara lingemwezesha kumkabili adui kokote aliko bila umbali kuwa kikwazo.
Baada ya Hitler kuingia madarakani mwaka 1933, maandalizi ya Ujerumani kijeshi yalianza kufanyika, hivyo mkazo na mkakati wa muda mfupi ulikuwa kutengeneza silaha kwa ajili ya vita dhidi ya mataifa ya Magharibi na mkakati wa muda mrefu ulikuwa juu ya uzalishaji wa silaha nzito kwa ajili ya vita dhidi ya Marekani.
Mwaka 1938 Hitler aliachana na mpango wa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Czechoslovakia na kuangalia zaidi makubaliano ya amani na kiongozi wa nchi hiyo ambayo yalifanyika mjini Munich na hilo lilikuwa kosa lake baya na kubwa kuwahi kulifanya.
Alipoamua kuigeukia Ufaransa na Uingereza, Hitler hakuweza kuishawishi Serikali ya Poland kujiunga na kuwa sehemu ya himaya ya Ujerumani kwa njia za amani, ili kuhakikisha hali ya utulivu inakuwepo katika Mashariki ya Ulaya, hivyo alichukua maamuzi ya kuivamia na kuiharibu Poland kabla ya kuanza kuzikabili nchi za Magharibi.
Uvamizi wa nchi ya Poland ulikusudiwa kufanyika ifikapo Septemba Mosi, 1939 lakini, ili kufanikisha azma yake hiyo na ushindi wa haraka juu ya Poland kwa kuvunja kila aina ya kikwazo mbele yake, alikusudia kuiingiza Ujerumani katika makubaliano na Urusi, ili mwisho wa siku iwe rahisi kwake kuzivamia nchi za Magharibi bila pingamizi lolote.
Pia Hitler alikusudia kufanya uvamizi dhidi ya Mataifa ya Magharibi katika msimu wa baridi mwishoni mwa mwaka 1939, lakini hali mbaya ya hewa ilikuwa ni kikwazo kikubwa ambacho kingeathiri jeshi lake la anga, kwa hiyo aliamua kuhairisha mpango huo na kuhamishia uvamizi huo ifikapo mwanzoni mwa mwaka 1940 katika majira ya joto.
Kutokana na ushauri alioupata toka kwa Admiral Erich Raeder juu ya kuivamia na kuiteka Norway, ili kuwezesha upatikanaji wa njia rahisi kwa jeshi lake la maji katika bahari ya Atlantiki kuelekea Kaskazini, aliivamia Norway mwaka Aprili, 1940.
Baada ya kupokea ushauri tena toka kwa Kamanda Mkuu Erich Von Manstein lengo la uvamizi kuanzia Kaskazini lilibadilishwa na kuamua kupanga mashambulizi kuelekea nchi zilizoko Kusini mwa Ulaya kwa lengo la kuzuia misaada ya kijeshi toka jeshi la Washirika (Allied force) kuelekea nchi za Ubelgiji na Uholanzi.
Mkakati mpya wa Hitler kwa mara ya kwanza ulionekana kufanya kazi wakati jeshi la Ujerumani lilipofanikiwa kuvunja mstari wa ulinzi wa jeshi la Kifaransa na kufanikiwa ndani ya siku kumi kufika kwenye mkondo wa Pwani nyuma ya vikosi vya majeshi ya Muungano.
Baada ya kuonekana wazi kuwa majeshi ya Washirika yaliyokwama yanaweza kutotoroka kipigo cha jeshi la Ujerumani, mwelekeo wa silaha na jeshi la Ujerumani ulibadilika tena, lakini jeshi hilo lilishachelewa kuweza kuzuia na kufanya mashambulizi dhidi ya askari wa jeshi la Muungano kwa sababu kikosi maalumu cha jeshi la Uingereza na wanajeshi wa Ufaransa walifanikiwa kuokolewa na kutoroka.
Pigo lililotokea mapema mwa mwezi Juni 1940 lililopelekea anguko kwa mstari wa mwisho wa ulinzi wa jeshi la Ufaransa ulikuwa ni ushindi kamili uliompa Hitler furaha na shangwe huku akijua anapata msaada wa kutosha toka kwa Makamanda na Majemedali wake wa kivita, ambao kila mara alikuwa akiwapandisha vyeo na kuwapa namna nyingine za rushwa kama sehemu ya kuwapa motisha ya kuendelea na mapambano.
Taarifa zinasema kwa sababu ilionekana kama vita hii ilikuwa imeisha baada ya Ujerumani kuiteka Ufaransa, Hitler alianza kupanga mipango mingine kwa ajili ya vita dhidi ya Marekani na Umoja wa Kisovieti.
Julai 11, 1940 Hitler alitoa amri kuanza kwa ujenzi wa jeshi la maji ikiwemo ujenzi wa meli za kivita na ilipofika Julai 31, 1940 baada ya mkakati wa kutaka kuvamia Umoja wa Kisovieti katika msimu wa baridi wa 1940, Hitler kutokana na ushauri wa wafanyakazi wake wa kijeshi aliamua kuishambulia Urusi katika majira ya joto mwishoni mwa mwaka1941.
Hitler alifikiri kwamba kushindwa kwa Ujerumani katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kulitokana na anguko lililotokea katika ardhi ya nyumbani, hivyo kudhani kuwa uanzishwaji wa sera za kidikteta na mauaji ya kukusudiwa ya Wayahudi ulikuwa uhakika wa ushindi wa vita dhidi ya majeshi washirika.
Safari hii Hitler alipoona hana jinsi na majeshi washirika yameshaingia mjini Berlin huku yakiongozwa na Jeshi Jekundu la Urusi, Hitler alijawa na hofu ya kisasi ambacho Warusi wangetoa dhidi ya Wajerumani, hivyo aliamua kumuoa mke wake na wote kwa pamoja kuamua kujiua muda mfupi kabla ya jeshi la Urusi kuwasili.
No comments:
Post a Comment