Wednesday, 5 November 2014

Republican Walidhibiti Baraza la Seneti Marekani

Image
Sio tu kwamba chama cha Republican kimepata ushindi katika majimbo ambayo kijadi ni ngome zake, bali pia katika yale ambayo yalimchagua rais Barack Obama wa chama cha Democratic hata katika uchaguzi wa rais uliopita, likiwemo la Iowa ambalo lilimpa ushindi wa mhula wa kwanza mwaka 2008.
Mbali na kuchukua Baraza la Seneti, warepublican pia wameimarisha udhibiti wao wa Baraza la wawakilishi, na kujishindia viti kadhaa vya ugavana wa majimbo ambayo hadi sasa yalikuwa yakiongozwa na watu wa chama cha Democratic.
Kushuka kwa umaarufu wa rais Obama ambaye mwenyewe alikiri kuwa uchaguzi huu ungekuwa kipimo cha uungwaji mkono wa sera zake, kumewaponza wagombea wa chama chake, ambao licha ya baadhi yao kujitenga naye wakati wa kampeni, hawakuweza kuwashawishi wapiga kura.
Onyo kwa viongozi wazembe
Katika hotuba yake ya ushindi wa useneta wa jimbo la Colorado, Cory Gardner wa chama cha Republican amesema matokeo ya uchaguzi huu ni hukumu kwa viongozi wasiowajibika.
''Usiku wa leo, wananchi wa Colorado wametuma ujumbe mjini Washington, kwamba wanachokifanya sio sahihi na cha paswa kusimamishwa. Ujumbe kwamba viongozi wanaoshindwa kuleta mabadiliko, wasitegemee shukrani. Haukuwa ujumbe kwa wa-Republican, au dhidi ya chama cha Democratic, bali onyo kwa wale wanaoshindwa kuchukua hatua za kijasiri, wakati taifa likikabiliwa na changamoto kubwa.'' Alisema Gardner.
Naye Mitch McConnell kutoka jimbo la Kentucky ambaye anatarajiwa kuwa kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Senate mjini Washington, amesema wapiga kura wamedhihirisha kukosa imani katika serikali ambayo haiwezi kutekeleza majukumu yake ya msingi. Hata hivyo ameashiria uwezekano wa kushirikiana na rais Obama mnamo miaka miwili ya uongozi wake iliyosalia. Kiongozi wa Democratic Harry Reid amesema yuko tayari kushirikiana.
Obama tayari kushirikiana
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House Josh Earnest alisema jana kuwa rais Obama alikuwa na utashi wa kufanya kazi bega kwa bega na warepublican katika kile alichokiita ''kuendeleza maslahi ya familia za tabaka la kati kote nchini''.
Hata hivyo, licha ya ahadi hizo za ushirikiano, warepublican wanatarajiwa kutumia udhibiti wa bunge kufufua miswada yao kuhusu ajira, kuangaliwa upya kwa baadhi ya sheria za kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa ya Ukaa, na bila shaka mpango wa bima ya afya wa rais Obama, maarufu kama Obamacare.
Utafiti uliofanywa na kituo cha Televisheni cha CNN cha huko Marekani miongoni wa watu waliomaliza kupiga kura zao jana, umedhihirisha kuwa asilimia 60 ya wapiga kura hawaridhishwi na kazi inayofanywa na vyama vyote viwili, Republican na Democratic, lakini idadi kubwa zaidi ilikikosoa chama cha Democratic kilichoko madarakani
CHANZO. DW

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!