Friday, 14 November 2014
MUHIMBILI YASITISHA GHARAMA MPYA
SERIKALI imesitisha ongezeko la tozo zilizoanza kutumika hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo ndiyo yenye vifaa tiba na madaktari wenye uwezo mkubwa kuliko hospitali yoyote nchini.
Hatua hiyo ya Serikali, ipo katika kauli ya Serikali bungeni, iliyotolewa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, ambapo pia Bohari ya Dawa (MSD) iliagizwa kupeleka dawa muhimu zenye thamani ya Sh milioni 200 katika hospitali hiyo.
Hivi karibuni hospitali hiyo ilipandisha gharama za huduma hospitalini hapo, ambapo mgonjwa aliyetakiwa kulazwa baada ya kupatiwa rufaa kutibiwa katika hospitali hiyo, alipaswa kulipa Sh 5,000 kwa siku na Sh 2,000 za chakula, ambazo hazikuwepo hapo awali.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, , ilikaririwa na vyombo vya habari, ikieleza kuwa gharama mpya zilianza kutumika Oktoba 17, mwaka huu.
Kutokana na gharama hizo, baadhi ya wahudumu hospitalini hapo walikaririwa wakisema idadi ya wagonjwa imepungua wodini kutokana na wengi wao kushindwa kumudu gharama.
Wagonjwa kutoka mikoani waliathirika zaidi, kwa kulazimika kutafuta malazi nje ya hospitali hiyo, hata kama hali zao ni mbaya. Aidha, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiuguza ndugu zao, walikaririwa kuchukua uamuzi wa kuwarejesha nyumbani ili kukwepa gharama hizo.
Miundombinu
Mbali na kusitisha ongezeko hilo la tozo, Dk Seif pia ameagiza uongozi wa hospitali hiyo kurekebisha mara moja mazingira na miundombinu ya hospitali hiyo, ambayo yapo ndani ya uwezo wao.
Ingawa tamko hilo halikufafanua, lakini taarifa zinaonesha kuwa hospitali hiyo ilikuwa ikizidiwa na wagonjwa, kiasi cha baadhi kulazimika kulala sakafuni.
Vyombo vya habari viliripoti kuhusu hali ya usafi wa vyoo vya wodi ya Sewa Haji kuwa mbaya, licha ya kuwapo taarifa za kutolewa kwa zabuni kwa kampuni kadhaa kufanya usafi, unaokidhi viwango na kanuni za afya bora.
Baadhi ya vyoo havikuwa na maji na vifaa vya kusukuma maji havikuwa vikifanya kazi, huku baadhi ya mabomba yakiwa na kutu. Kutokana na ukosefu wa maji, wagonjwa na watu wanaowatembelea, walilazimika kutumia maji yaliyopo kwenye mapipa nje ya vyoo na yalipokosekana, walitafuta mahali kwingine ikiwamo nje ya jengo hilo.
Baadhi ya vyombo vya habari, viliripoti kushuhudia baadhi ya vyoo vikiwa vimejaa uchafu katika majengo ya Sewa Haji, Kibasila na Mwaisela huku vingi vikiwa katika hali mbaya ya uchakavu, kutokana na kutumika muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati.
Deni MSD
Kuhusu deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Dk Rashid alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ilifanya uhakiki wa deni la MSD la Sh bilioni 41.5.
Baada ya deni hilo kuhakikiwa, alisema Serikali ilianza kulipa kwa awamu ambapo Sh bilioni 8 zililipwa Juni 14, Sh bilioni 2 Agosti na Sh bilioni 20 zimelipwa mwezi huu. Alisema kiasi kilichobaki cha Sh bilioni 11.5, kitalipwa mwezi ujao.
Kuhusu kutenga fedha za kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kupitia MSD ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata dawa na vifaa tiba kwa wakati, alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Bunge liliidhinisha Sh bilioni 70.5 kwa ajili ya kazi hiyo. Ocean Road
Akizungumzia huduma za afya katika Hospitali ya Ocean Road, alisema huduma za matibabu ya saratani inaendelea kutolewa, kutokana na mashine ya E80 kuendelea kufanya kazi na kwa sasa ndiyo inayotibu wagonjwa wote wa saratani katika taasisi hiyo.
“Kutokana na kuwepo kwa mashine moja tu ya mionzi inayofanya kazi, kwa sasa hivi mashine inafanya kazi kwa saa 18 kwa siku ili kupunguza mlundikano wa wagonjwa. “Mashine ya intra cavitary ambayo ilikuwa imesimama kufanya kazi kutokana na ubovu na kukosekana kwa vifaa muhimu, imetengenezwa na sasa imeanza kufanya kazi hivyo kuwezesha matibabu ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Waziri.
Nafasi ya Njelekela yatangazwa
Wakati hali ikiwa hivyo, nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, ilitangazwa jana kuwa iko wazi. Sifa za mtu anayetakiwa kujaza nafasi hiyo ni pamoja na Shahada ya Uzamili katika Udaktari wa Binadamu; au sifa inayolingana na hiyo katika masuala ya udaktari na upasuaji, pamoja na uzoefu wa zaidi ya miaka kumi katika uongozi wa hospitali.
Tangazo hilo lilitolewa na hospitali hiyo na lilikuwa katika gazeti la Daily News la jana, Ukurasa wa Nne. Waombaji wenye vigezo vinavyotakiwa, wanatakiwa watume maombi ya kazi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo nyeti nchini huripoti kwa Bodi hiyo ya Wadhamini. Mwisho wa kupokea maombi ya kazi hiyo ni Desemba 5, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment