Friday 14 November 2014

MAREKANI YAIPATIA TANZANIA BILIONI 16.6



SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), imetoa Sh bilioni 16.6 kwa Tanzania, zitakazotumika kujenga miundombinu ya umeme.



Mkataba wa makabidhiano ya fedha hizo, ulisainiwa jana kati ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Makamu wa Rais wa MCC, Kamran Khan. Akizungumza katika hafla hiyo, Saada alisema fedha hizo ni kwa ajili ya matayarisho ya miundombinu ya umeme.
Alisema baada ya maandalizi hayo, mradi wa umeme utasainiwa mwakani na utaondoa tatizo la umeme kwa maeneo mengi nchini.
“Fedha hizi zitasaidia kwenye maandalizi ya awali tu kama maandalizi ya ofisi, miundombinu, kutafuta mshauri mwelekezi na mradi wenyewe hasa utaanza mwakani, na lengo hasa ni kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwenye umeme,” alisema Waziri huyo.
Alisema fedha hizo zitahakikisha miundombinu ya umeme Tanzania Bara na Zanzibar inakuwa imara na zitaimarisha vyombo vinavyosimamia sekta hiyo ya nishati.
“Tunajua umuhimu wa umeme kwenye kilimo na pia viwanda, MCC wamesema watasaidia sekta hii kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hii na upatikanaji wake unakuwa imara,” alisema Saada.
Alisema mbali na kupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa umeme, pia mradi huo utalipa nguvu Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuhudumia watu wengi zaidi.
Khan alisema makubaliano hayo ni muendelezo wa ubia imara kati ya Marekani na Tanzania, ambapo kati ya mwaka 2008 na 2013 MCC ilitekeleza mkataba wa miradi mikubwa katika sekta za maji, barabara na umeme nchini kote, ambayo iligharimu dola za Marekani milioni 698.
“Chini ya mkataba huo mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya kilomita 3,000 ulijengwa, kilomita 430 za barabara pia zilijengwa, mitambo mikubwa miwili ya usafirishaji maji ilifungwa na njia ya kurukia ndege ilitengenezwa,” alisema Khan.
Alisema kwa kuzingatia mafanikio katika miradi hiyo, MCC iliichagua tena Tanzania kuingia katika mkataba wa pili katika sekta hiyo ya nishati ya umeme, ikiwa ni pamoja na kuboresha uendeshaji wa Tanesco na Zeco kiufundi, kusimamia fedha na uendeshaji na kuongeza kiwango cha upatikanaji umeme katika maeneo ya vijijini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!