Sunday 23 November 2014

MIKATABA YA GESI, MAFUTA SASA YATAKIWA BUNGENI


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, imeshauri kuwa wakati umefika sasa kwa mikataba mikubwa ya uwekezaji wa rasimali za Taifa kuridhiwa na Bunge.



Aidha, imeshauri kuwa lazima kuwe na chombo maalumu kinachosimamia uwekezaji wa hisa za Serikali katika sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliyasema hayo bungeni jana wakati akitoa maoni ya Kamati yake katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa 2014.
Mpina alisema: “Kamati inashauri kuwa umefika wakati sasa mikataba mikubwa ya uwekezaji wa rasilimali za Taifa, mfano ardhi, madini, mafuta, gesi, misitu na kadhalika, kuridhiwa na Bunge.”
Aliwashauri pia sheria itamke wazi sharti la mikataba ya ubia kuwa na kipengele kitakachosimamia ubora wa miradi kwa kipindi chote cha mkataba hadi mradi utakaporejeshwa serikalini ili kulinda maslahi ya umma.
Alisema kwa kuzingatia maudhui ya muswada huo, Kamati imeridhika kuwa mapungufu yaliyopo katika sheria hiyo yakifanyiwa marekebisho, sheria itasaidia kuboresha usimamizi na uratibu wa masuala ya ubia huo na kuongeza ufanisi katika uidhinishaji wa miradi ya ubia.
“Pia ni muhimu Watanzania wafaidike moja kwa moja na rasilimali za nchi, hii inafanyika katika nchi nyingi na inawezekana hata hapa kwetu Tanzania,” alisema Mpina.
“Tunataka ununuzi wa umma uwe chombo cha kuwawezesha Watanzania kiuchumi kwani sio kwamba Watanzania hawawezi, wanaweza sana suala ni kuwawezesha na siyo kuwabeza.”
Katika mchango wake, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema vigezo viwili ni muhimu katika suala hili la ubia, kuaminika na ufanisi.
Naye Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM), alisema mabadiliko ni mazuri na kutaka uwepo uwazi katika sheria ya ununuzi wa umma.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!