Sunday 23 November 2014

TUNAHITAJI RAIS AJE AWE DIKTETA-WASOMI

Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu namna sakata la wizi wa fedha kwenye akaunti ya Escrow linavyoshughulikiwa, huku wengine wakisema umefika wakati sasa nchi iongozwe na rais dikteta.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kuwa uamuzi wa Naibu Spika, Job Ndugai kuwaomba wabunge kukishauri kiti chake juu ya hatua ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwa ripoti ya uchunguzi wa fedha za Escrow, umeonyesha Bunge linataka ukweli ujulikane.
Mratibu wa Umoja wa Wanawake  Wanasiasa Tanzania (ULINGO), Dk Ave Maria Semakafu alisema baadhi ya watu wanataka kupotosha ukweli kwa kuwataja viongozi wasiohusika hawahusiki moja kwa moja na ufisadi wa fedha hizo badala ya kuwanyooshea kidole majaji waliotajwa kupewa mgawo huo.
Akizungumzia suala la mahakama kuzuia jambo hilo kujadiliwa bungeni, alisema kinachofanyika ni sawa na kumpa nyani kesi ya ngedere huku ukijua kabisa haki haitotendeka.
“Hata waandishi wa habari wanakosea mahali  pa kulenga, majaji watatu ndio wametajwa kupata mgawo (anawataja), suala hapa Jaji Kiongozi atoe taarifa kuhusiana na jambo hilo,” alisema Semakafu.
Alisema kutokana na kujirudiarudia kwa matukio ya ufisadi nchini, taifa limepoteza mwelekeo hivyo linahitaji kiongozi dikteta atakayeweza kuwashughulikia wahalifu bila huruma.
“Nchi haijulikani inakwenda au inarudi. Dawa ni kupata kiongozi dikteta, nchi hii haihitaji mtu mwenye makundi, tumefika hapa kwa sababu ya urafiki,” alisema Semakafu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema kinachoonekana sasa ni matokeo ya viongozi kutokuwa na utamaduni wa kuchukua hatua kali watu wanapofanya makosa, ikiwamo kufilisi mali zao.
Profesa huyo alisema kwa hali ilipofikia nchi inahitaji kupata kiongozi dikteta ambaye atakuwa tayari kutawala kwa muda mfupi ili arudishe nidhamu iliyopotea.
“Tunahitaji dikteta atakayesema nitakaa kwa muda mfupi, asafishe uozo, kisha aondoke…, Haiwezekani tuendelee kushuhudia nchi ikizidi kufilisika,” alisema Profesa Shumbusho.
Mbunge wa Mgogoni, Kombo Khamis Kombo (CUF), alisema matukio ya ufisadi yameongezeka nchini kwa sababu kila kiongozi anayetarajiwa kuchukua hatua analalamika kuwa watendaji wake wanamwangusha.
“Viongozi wanapiga danadana, wana watu ambao hawawezi kuwakosoa…, tulipofikia tunahitaji kiongozi mwenye maadili,” alisema Kombo.
Mkuu wa Kitivo Msaidizi  (Taaluma), Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii,  Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Danford Kitwana alisema kilichotokea bungeni juzi kinaashiria Serikali kujaribu kulizima suala la Escrow ili lisijadiliwe kwa kuwa wanafahamu linaweza kuwang’oa baadhi ya viongozi madarakani.
Hata hivyo, alisema kutokana na kauli za wabunge wengi waliotoa mapendekezo yao kutaka jambo hili lijadiliwe na ukweli kufahamika, Serikali itakuwa na nafasi ndogo ya kukwepa kutekelezwa kwa maoni ya wabunge walio wengi.
Aliongeza: “Tatizo la Tanzania ni ukosefu wa maadili na uchungu wa mali ya umma, tutaendelea tu kusikia kesi kama hizi kwani bado kuna mambo mengi yaliyofanywa bado hayajafichuliwa.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!