Maisha ya maelfu ya Watanzania yapo hatarini baada ya kubainika kuwa kwenye magari ya abiria maarufu daladala ya jijini humo, yanayotoa huduma za usiku kwa safari za kwenda na kutoka maeneo mbalimbali yamekuwa yakihusishwa na mtandao wa vibaka unaoendesha vitendo vya uporaji na ukabaji.
Mtandao huo unaelezwa kufanya vitendo hivyo kwa kutumia silaha mbalimbali ikiwamo visu na bastola, huku baadhi ya vibaka hao wakitumia magari hayo kujificha kwa kujifanya ni abiria.
Mbali na uhalifu huo unaoendelea kufanyika kwenye daladala nyakati hizo za usiku, magari mengi yanayotoa huduma za usafiri nyakati hizo hadi alfajiri ni mabovu yakiwa pia hayana vibali vya kutoa huduma hizo.
Magari hayo yanayofahamika kwa jina la ‘daladala bubu’ au ‘ya kuwanga’ madereva wake pia hufanya kazi hiyo bila ya kuwa na leseni za udereva, jambo linalohatarisha zaidi maisha ya abiria.
Uchunguzi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ikiwamo Sinza, Ubungo, Kariakoo, Faya, Buguruni, Gongo la Mboto Machinjioni, Kimara, Mbezi, Magomeni, Kinondoni, Tandika, Temeke, Yombo Dovya, Vingunguti, Bom Bom na Machimbo, umebaini kuwa magari hayo hufanya kazi nyakati za usiku pekee kutokana na kutokuwapo askari ama kuwapo askari wachache wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Gazeti hili limebaini kuwa wizi kwenye daladala hizo, madereva wa daladala kuwapa makondakta au wapiga debe kuendesha magari ya abiria vinaendelea kushamiri, huku nyakati za hatari zaidi kwa daladala hizo ni kuanzia saa 6 usiku hadi alfajiri.
Uhalifu unaofanywa
Uhalifu unaofanywa kwenye magari hayo unahusisha vibaka wanaokuwa ndani ya gari ambao hujifanya kuwa miongoni mwa abiria.
Imebainika kuwa abiria akikaa vibaya ndani ya daladala, vibaka hao hutumia nafasi hiyo na kujihalalishia chochote watakachoweza kuibia.
Aina nyingine ya vibaka ni wale wanaokula njama na madereva na kondakta wa daladala. Vibaka hao pia hujifanya abiria kwenye daladala bubu husika ambapo wakifika kituoni hujihusisha na kupiga debe kuita abiria, lakini mbele ya safari dereva hubadili njia, akiweza kwenda vichochoroni ndipo abiria huvamiwa na kuporwa mali zao huku wakitishiwa kwa silaha.
Uchunguzi unaonyesha kuwa aina nyingine ya wizi huo hufanywa na kundi la vibaka ambalo hujifanya ni abiria ambapo kila mmoja hulenga kumfanyia uhalifu abiria mmoja.
“Abiria akishuka tu na yeye anashuka, humfuata na kumwibia, halafu anakwambia utembee bila kugeuka. Ukigeuka tu wanakuchoma na kisu au silaha yoyote wanayokuwa wamejihami nayo,” alieleza mmoja wa madereva wa daladala aliyeomba jina lihifadhiwe kwa kuwaogopa vibaka hao.
Aina nyingine ya uhalifu ni ule unaofanywa na vibaka wanaokuwa katika vituo vya daladala. Maskani yao ni kwenye vituo hivyo ambapo abiria akishuka huweza kumkwapua hata wakati mwingine kumfuatilia hadi eneo watakaloona hakuna watu na kumpora.
Uchunguzi
Zaidi ya mara tatu, mwandishi wa gazeti hili alipanda gari na kukutana na masaibu hayo. Mara ya kwanza alipanda gari kutoka kituo cha Tabata Relini kwenda Temeke.
Hata hivyo, gari lilipofika Tabata-mataa abiria walitangaziwa kuwa ndiyo mwisho wa safari kutokana na gari hilo kushindwa kuendelea na safari kwa kilichoelezwa kuwa ni ubovu. Gari hilo lilikuwa limeandikwa M- Sita-Segerea.
Katika kituo cha Tabata Segerea, mwandishi alijifanya kama askari na kuanza kumuhoji kijana mdogo aliyeonekana mwenye umri wa chini miaka 18. Kijana huyo ndiye aliyekuwa dereva wa gari hilo ambapo alikuwa akisubiri abiria wa kwenda Kinyerezi.
Baada ya kumuhoji kijana huyo na kumtaka aonyeshe leseni yake ya udereva alisema kuwa ipo kwa bosi wake huku akitetemeka. Kijana huyo alikiri baadhi yao kufanya matendo hayo, lakini akasema binafsi hajawahi kufikiria kufanya uhalifu.
Madereva daladala wazungumza
Mmoja wa madereva daladala zinazofanya safari zake Mbagala- Ubungo aliyejitambulisha kwa jina la Saidi Omari aliliambia gazeti hili kuwa, mara nyingi huwaachia magari watu wengine wasio na uzoefu hata leseni hawana ili kuwasaidia wapate uzoefu wa udereva hasa nyakati za usiku kwani hakuna askari.
“Unajua maisha ni kusaidiana. Anakuja jamaa anakuambia ajifunze kuendesha angalau apate uzoefu. Kutokana na hali ya maisha, unashindwa kumnyima. Siyo kila mtu anaweza kumudu gharama za mafunzo ya udereva zinazotolewa vyuoni. Akijifunza, baadaye akifahamu vizuri leseni anapambana tu hadi anapata,”alisema Omari.
Dereva mwingine anayefanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Buguruni, Mathew Saimon, alibainisha kuwa kabla ya kumpa mtu anaendeshe daladala yenye abiria humpa kwanza ajifunze. Akishafahamu kuendesha vizuri, ndiyo wanamruhusu aendeshe likiwa na abiria.
“Tunampa aendeshe barabarani akiwa na abiria apate uzoefu na kumjenga hali ya kujiamini akiwa barabarani kwani tunafahamu kuwa ndani ya gari tumebeba roho za watu zaidi ya 30. Akiwa mzoefu ina maana kuwa sheria za barabarani atakuwa anazifahamu vizuri,”alisema Saimon.
Kuhusu kujihusisha na wizi, dereva huyo alisema kuwa huwa anasikia habari hizo kwa wenzake kuhusu hali hiyo huku akieleza kuwa kuna wakati hata wao wanakumbana na vibaka.
“Lakini katika suala la udereva huwa hatumpi gari mtu tusiyemfahamu. Pia, hatujihusishi na wizi kwani tukifanya hivyo tutaleta dosari katika utoaji wa huduma zetu,”alisema.
Abiria wazungumza
Lilian Laurent, mkazi wa Kinondoni Mkwajuni ambaye ni mmoja wasafiri aliyewahi kukumbana na masaibu hayo, alisimulia kuwa aliwahi kupanda daladala akidhani yupo na abiria wenzake kumbe walikuwa vibaka.
“Ulikuwa usiku wa saa 5 hivi. Nilipanda mimi pamoja na mwenzangu kwenye Kituo cha Faya kuelekea Kariakoo. Ndani ya gari walikuwa vijana wanne na mwanamke mmoja.Tulienda vizuri. Kufika mbele kidogo, dereva aliongeza mwendo, akabadili na njia.
Tukaanza kupiga kelele. Wale vijana walishika visu wakatutishia kwamba, tukipiga kelele tu wanatuchoma. Tulinyamaza wakaingia uchochoroni, wakatusachi na kuchukua kila kitu, halafu wakatushusha na kutuambia tupotee,”anasimulia Laurent na kuongeza kuwa daladala hiyo haikuwa imeandikwa jina wala inapokwenda.
Naye Amir Salumu alisema kuwa aliwahi kupanda gari usiku kutoka Ubungo kuelekea Gongo la Mboto. Lakini walipofika Tazara lilizima wakalazimika kushuka bila ya kurudishiwa nauli.
Wakati yeye akikumbana na hilo, Husna Khalid anasimulia kuwa, mwezi uliopita alipanda daladala ya Kariakoo-Vingunguti na kuibiwa.
“Daladala ilikuwa imejaa sana hivyo nililazimika kusimama. Wakati ninakaribia kushuka, kijana aliyekuwa amesimama pembeni yangu alianza kunisukuma kwa nguvu. Sikujisumbua kwa sababu nilijua nashuka kituo kinachofuata. Sikufahamu kwamba alikuwa ananiibia. Nilifika nyumbani nikagundua zipu ya pochi imefunguliwa. Hakuna simu wala pochi ndogo (walet),”alisema Khalid.
Kwa upande wake Victoria Kagasheki mkazi wa Kinondoni, alisimulia jinsi alivyoponea chupuchupu kuchomwa na kisu akisema kuwa alipanda daladala usiku akielekea Kinondoni Mkwajuni.
“Nilifika kituoni vizuri. Baada ya kushuka wakati natembea kuelekea nyumbani walitokea vijana watatu. Wawili walinishika huku na huku wakiwa na visu, mwingine akaingiza mikono mfukoni mwangu, wachukua pochi, wakanivua kila kitu, kasoro nguo ya ndani huku wakinitisha kuwa nikipiga kelele tu nimepoteza maisha. Walivyomaliza wakaniambia nipotee na nisigeuke nyuma,”anaeleza Kagasheki.
Sumatra
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Kanda ya Mashariki, Konrad Shio alisema kuwa mamlaka yake inafahamu kuwapo kwa tatizo hilo.
“Suala la kuwa na wapigadebe kuendesha daladala tunalifahamu…na wala halifanyiki usiku tu. Hata mchana hufanyika kwa kisingizio kwamba dereva mhusika anaumwa au ana dharura.
“Nakumbuka kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu, tulifanya operesheni za kawaida za makosa mbalimbali barabarani hapa jijini. Tulikusanya leseni za madereva 30 na kuzifanyia uchunguzi wa kina. Tulibaini kuwa kati ya hao ni mmoja pekee aliyekuwa na mkataba wa kuendesha daladala,”alibainisha Shio.
Aliongeza kuwa, licha ya kwamba walikuwa na leseni za udereva, lakini hawakuwa na kibali cha kuendesha usafiri wa abiria.
Kuhusu daladala zisizo na kibali saa za usiku, Shio alieleza kuwa madereva wengi hawana leseni na ndiyo vinara wa kuendesha magari mabovu.
Ofisa huyo alieleza kuwa karibu nusu ya madereva waliokuwa wanaendesha magari hayo hawakuwa na leseni, jambo ambalo linahararisha usalama wa abiria.
Kuhusu wizi wa kwenye daladala, Shio alikiri uhalifu huo kufanyika, lakini akaeleza kwamba watu wanaojihusisha na uhalifu huo ni wale wanaotumia mwanya wa daladala ambazo hazijasajiliwa.
Ili kuhakikisha suala hilo linapatiwa mwarobaini, Shio alisema kuwa Sumatra inajipanga kufanya operesheni maalumu usiku jijini humo itakayolenga kukagua magari mabovu na yasiyokuwa na leseni.
Wizara ya Uchukuzi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Uchukuzi, William Budoya alisema kuwa Sumatra, ambayo ni mamlaka husika katika suala hilo inatakiwa kuongeza nguvu kazi.
“Wanatakiwa kusimamia kikamilifu shughuli za usafiri nchini. Tena ikiwezekana waongeze operesheni za usiku. Kwa kufanya hivyo wataweza kusaidia kutokomeza hili,”alisema Budoya.
Alisema kuwa ajali zinaweza kuepukika kwa kuongeza umakini kwa madereva, ikiwa pamoja na ukaguzi wa madereva wanaoongoza vyombo hivyo.
Jeshi la Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya analizungumzia hilo na kusema kuwa, ofisi yake imekuwa ikifikiwa na ripoti mbalimbali za uhalifu, ingawa hana uhakika kama hizo ni miongoni mwao, huku akiahidi kwamba kama lipo jambo kama hilo watalifanyia kazi.
Hata hivyo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga amekiri kuwapo kwa tatizo hilo la ukiukwaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani kunakofanywa na baadhi ya madereva.
“Ilo tuna taarifa nalo na tunalifanyia kazi kwa maana ya kuongeza operesheni za barabarani. Nimeshaagiza wakuu wa usalama barabarani wa mikoa mitatu ya hapa Dar es Salaam kwa maana ya Temeke, Ilala na Kinondoni pamoja na yule anayesimamia Kanda Maalumu, kuendeleza operesheni ambayo tumeianza kwa mabasi makubwa kwa kukagua leseni na vyeti vya vyuo walivyosomea udereva.
“Kwa daladala wanaweza kuendesha kwa daraja la C1 na C3. Kwa hiyo zoezi hilo tutafuatilia kujua linaendeleje, lakini ninatoa maelezo kwamba wafanye ukaguzi kwa madereva wote wa daladala nchini
Ni kweli na mimi nimekuwa nikipata taarifa kwa wananchi wengi wakisema kwamba kuna baadhi ya maderava wa daladala wengine hawana leseni na wengine ndiyo wale wanaowaita deiwaka. Kwa hiyo hilo nalichukulia kwa uzito na kuhakikisha linafanyiwa kazi.
Nimeshaagiza lianze mara moja kama ilivyo kwa mabasi yaendayo mikoani na kwa daladala. Nimeagiza lianze mara moja. Suala la usiku ni changamoto. Usiku ni giza, dereva daladala anaweza kumgonga askari, lakini nalo tutaona namna ya kulishungulikia,”alisema Mpinga.
Aliongeza: “Tunaweza kuweka vizuizi barabarani au kuweka kambi katika vituo, ambapo daladala zinaanzia safari, kuweka askari ambaye atakuwa anakagua leseni. Japokuwa madereva wanaweza kuwa wajanja na kubadilishana sehemu ambapo hakuka trafiki, lakini hapo ningewaomba wananchi wajitahidi kutoa taarifa polisi. Waseme, gari namba fulani linaendeshwa na dereva ambaye hana sifa.”
Alisema kuwa operesheni hiyo itafanywa nchi nzima, kwani madereva wanaoendesha magari yanayotoa huduma kwa wananchi hawapo Dar pekee.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment