Kazi ni kazi mchagua jembe si mkulima... kikubwa ni kufanya jitihada zozote ili mradi mkono uende kinywaji pata mikeka ya asili iliyo na ubora wa hali ya juu na kuhimilia matumizi mbalimbali kama kulalia, kuanikia unga na mahindi pindi yapooshwa.
Ukiwa katika Kijiji cha Ilembo Wilaya ya Mbeya Vijijini hususan katika siku maalumu za minada utawakuta kinamama wengi wajasiriamali wakiuza bidhaa mbalimbali hususan mikeka, vikapu na mahitaji mengine ya nyumbani.
Siku ya minada katika maeneo ya mengi ya vijiji ni siku maalum ya kutoa fursa kwa wafanyabishara, wakulima kuuza bidhaa zao na hata jamii kutumia siku hiyo kufurahi, kuburudika kwa vinywaji vya aina mbalimbali hususan nyama choma.
Nikiwa katika Kijiji cha Ilembo katika mnada wa siku ya Ijumaa ambayo ni mashuhuri kwa shamra shamra nilikutana na mjasiliamali wa kusuka mikeka ya asili Letisya Mwaipaso (37) ambaye anasema ameweza kuwa na mafanikio makubwa kutokana na biashara hiyo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita
Mwaipaso ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Santilya kata ya Ilembo na hakufanikiwa kupata elimu ya sekondari kutokana na hali duni ya uchumi katika familia na kusababisha kuolewa akiwa na umri mdogo na kwamba mpaka sasa ni mama wa watoto watatu
Anasema kuwa baada ya kuolewa alikutana na changamoto mbalimbali za kimaisha katika ndoa yake hali iliyomlazimu kuchanganua akiri ya kujua ataishi vipi na familia inayomtegea na hivyo kujikita katika kilimo cha zao la viazi mviringo.
Anasema alianza kwa mtaji wa Sh50,000 na kwamba mungu alimsaidia na kupata faida ya Sh60,000 na hivyo aliongeza jitihada zaidi katika kilimo hicho kwa kutambua kuwa mwanamke ndio kichwa cha nyumba
Amesema kuwa hakuishia katika kilimo cha viazi pekee bali aliendelea kujishughulisha na shughuli za ususi wa mikeka.Pia umemwongezea mwanga wa kumudu upatikanaji wa fedha na hivyo kuachana na utegemezi na kusimama mwenyewe katika kukabiliana na hali ya maisha.
Anasema mpaka sasa anawezaa kupata faida ya Sh20,000 hadi Sh30,000 kwa siku ambazo zinajitosheleza kumudu kutunza familia na kucheza michezo ya kuchangia fedha mitaani na hivyo kujikuta akiachana na utegemezi.
Anasema kuwa akiwa kama mwanamke anayejiamini amekuwa ni mtu wa kujaribu kila aina ya biashara ili afikie ndoto yake ya kujenga nyumba bora ya kisasa katika kijijini ili awe mfano wa kuigwa.
Aidha alisema biashara hiyo imempa mafanikio makubwa na kwamba anauza kwa bei ya Sh8,000 hadi Sh12,000 kulingana na ukubwa na kwamba imekuwa na wateja wengi wa kudumu kutoka katika maeneo mbalimbali hadi nchi jirani ya Zambia.
Ameweza kununua kiwanja ambacho alijenga nyumba ya kawaida ambayo mpaka sasa anaishi na familia yake na akielekeza nguvu zaidi katika mradi wake wa kufuma mikeka.
Mwaipaso anasema kuwa safari ya maisha inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kujituma na kwamba wanawake wanapaswa kujituma na kujiamini kuwa na wao ni sehemu ya jamii inayoweza kusimama yenyewe.
WITO
Wanawake huu ni wakati wa kuchangamkia fursa za kiuchumi kwa kutumia rasilimalia zilizopo kwa kujikita katika kilimo cha mazao mchanganyiko na kujihusisha katika utengenezaji wa vitu vya asili kwa kuwa na mitaji midogo isiyohitaji nguvu zaidi.
“Nchi yetu ina rasilimali nyingi za kujikwamua kiuchumi zisizotegemea mitaji na kwamba wanawake waachane na dhana za kuwa tegemezi kwa waume zao kwani hali hiyo inachangia wanaume wengi kukimbia nyumba na kutelekeza familia,” anasema.
Aidha, aliwataka wanawake vijijini kujiunga katika vikundi vya kinamama ili waweze kupatiwa elimu ya kuanzisha miradi ya ujasiriamali kwa kutumia mitaji kidogo na kuchana na dhana za kuchukua mikopo katika taasisi za kifedha ambayo kwa kiasi kikubwa udhalilishaji na kunyang’anywa mali zao.
Mwaipaso anasema kuwa fursa za kiuchumi ni nyingi na kwamba wanawake wasikubali kubweteka na kutumiwa vibaya katika familia hali inayosababisha kuonekana mizigo na kujikuta tukinyanyapaliwa na kutengwa na jamii.
OMBI
Wanaiomba Serikali kuwezesha vikundi vya wakinamama ili viweze kuimarika na kuwa endelevu na kutambulika kisheria kwani wanawake wakiwezeshwa wanaweza katika kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa hususan kuongeza ajira kwa vijana
Anasema kuwa tatizo la wanawake wengi kubweteka ni changamoto ya ukosefu wa vyanzo vya mapato na hivyo kusababisha kuwa tegemezi katika ndoa na familia zao.
Hata hivyo, anasema mikakati pekee ya kujikomboa kwa wananwake na kujikita katika shughuli zozote na si kuchagua kazi na kwamba ni wakati wa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo ili kujinasua na hali ya umaskini miongoni mwetu.
Aidha, wameiomba Serikali na wadau mbalimalimba kutumia fursa na kununua bidhaa za asili zinazotengezwa na wajasiriamali wadogo wadogo ili kutangaza soko la bidhaa hizo ndani na nje ya nchi ili kuwasaidia kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi
No comments:
Post a Comment