Wednesday 19 November 2014

MICHEZO: KLUIVERT ATHIBITISHA UJIO WA BARCELONA DAR


MAVETERANI wa klabu ya FC Barcelona inayocheza Ligi Kuu ya Hispania La Liga, wanatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Disemba mwaka huu.



BIN ZUBEIRY imeambiwa na mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Patrick Kluivert aliyekuwa kisiwani hapa kwa mapumziko mafupi.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwepo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar wakati nyota huyo mstaafu wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi akiondoka kurejea nchini kwao, alimuuliza sababu ya ujio wake nchini Tanzania.

Akijibu suala hilo, Mholanzi huyo aliyewahi pia kuwa msaidizi kocha wa Uholanzi, alisema kilichomleta ni kukamilisha taratibu za kulieta klabu yake hiyo nchini Tanzania.

Alisema watakapokuwa nchini, wakongwe hao watacheza mechi moja ya kirafiki na timu watakayopangiwa na wenyeji wao.


Nyota wa zamani wa FC Barcelona ya Hispania na timu ya taifa ya Uholanzi Patrick Kluivert akihojiwa na mwandishi wa Zanzibar Leo Salum  Vuai katika uwanja wa ndege wa Abeid Karume Zanzibar wakati akijiandaa kuondoka nchini jana. Anayeonekana kulia ni muandaaji na mtangazaji wa kipindi cha michezo redio Coconut FM, Ali Mohammed.  


"Bado hatujajua tutacheza na timu gani, ama klabu, timu ya taifa au wachezaji wa zamani wa Tanzania, hilo tunawaachia wenyeji wetu wapange, ninachoweza kukwambia ni kwamba Barcelona ya zamani wakati mimi nikicheza itakuja Tanzania wakati wowote mwezi Disemba," alifafanua Kluivert.

Aliwaomba wapenda soka wa jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa jumla, kujiandaa kushuhudia kikosi cha maveterani hao, ambao alisema licha ya umri mkubwa, bado wanaweza kusakata kabumbu la kusisimua.

Mratibu wa ziara ya nyota huyo hapa Zanzibar Ali Khatib Dai, alisema mpango mzima wa kuileta FC Barcelona nchini, unaandaliwa na Kampuni ya Tanzania Sisi Nyumbani, (TSN) yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam, chini ya Mkurugenzi wake Farough Baghozahi.

Alipokuwa kisiwani Zanzibar, Kluivert alifikia katika hoteli ya kitalii ya La Gema iliyoko Nungwi Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja ambako alikaa kwa muda wa siku mbili na kuondoka jana Novemba 18 mchana

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!