Thursday, 20 November 2014
BARABARA JUU YA BAHARI KUPUNGUZA FOLENI DAR
JUHUDI za Serikali za kukabiliana na foleni katika jiji la Dar es Salaam zimeendelea kushika kasi, ambapo siku moja baada ya kupokea kivuko cha kisasa kitakachofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, jana imetangaza mpango wa kujenga barabara ya juu itakayopita juu ya bahari ya Hindi kati ya ufukwe wa Coco, Oysterbay na Aga Khan, Upanga.
Tayari makubaliano ya ujenzi wa barabara hiyo umefikiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini. Barabara hiyo itakuwa na urefu wa kilometa 7.1 huku daraja litakalounganisha barabara hiyo kupita juu ya bahari litakuwa na kilometa 1.2 na litakuwa na njia nne pamoja na njia za waenda kwa miguu.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa za kubomolewa kwa daraja la Selander ambapo alisema, taarifa hizo ni upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu.
Alisema daraja la Selander lilijengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan na haliwezi kubomolewa kwa kuwa Serikali ina historia kubwa na Japan, hivyo si jambo la busara kubomoa daraja hilo ambalo linapitisha magari 51,000 kwa siku moja.
“Serikali ya Korea Kusini imekubali kujenga flyover yenye urefu wa kilometa 7.1 ambayo itaanzia Coco Beach na kuja kutokea Aga Khan na kuungana na barabara ya Ali Hassan Mwinyi,” alisema Magufuli.
Alisema barabara hiyo itakuwa ina uwezo wa kupitisha magari 61,000 kwa siku hivyo kufanya kupunguza msongamano kwa kiasi kikubwa sana na hilo hasa ndiyo lengo la Serikali.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale alisema, ujenzi wa barabara na daraja hilo unatarajiwa kuanza mwakani kwani tayari asilimia 99 ya mazungumzo yameshakamilika na bado asilimia moja ili ujenzi uanze.
Alisema michoro ya ujenzi wa daraja hilo umekamilika na hivyo kazi iliyobaki ni kutolewa kwa pesa ili ujenzi uanze mara moja, ujenzi ambao unatarajiwa kufanyika katika miezi 24.
Aidha, alisema daraja hilo litagharimu Sh bilioni 110 litakuwa likipakana na daraja la Selander na si kubomolewa kama taarifa za upotoshwaji zinavyosambazwa kwenye mitandao.
“Litasaidia kupunguza tatizo la foleni kwa sababu kutakuwa na barabara ambazo pia zitaunganisha na barabara ya Chole na kuja hadi Coco Beach na itakwenda hadi Agha Khan na kuungana na Ali Hassan Mwinyi, hivyo foleni hapa katikati haitakuwepo,” alisema.
Wakati safari za kivuko kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo zikisubiriwa kwa hamu, sambamba na ujenzi wa barabara za juu kupitia bahari ya Hindi katika eneo la ufukwe wa Coco na Aga Khan, ujenzi mwingine wa daraja kati ya katikati ya Jiji hadi Kigamboni kupitia baharini, unaofanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi la Jamii (NSSF) na Serikali, unaendelea.
Aidha, Serikali imeendelea kujenga kwa kasi barabara za mradi wa mabasi yaendayo kasi, kujenga barabara za pembezoni mwa jiji kwa kiwango cha lami, dhamira ikiwa kuifanya kero ya msongamano na foleni wa magari jijini Dar es Salaam kuwa historia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment