KATIKA hatua inayoonesha utendaji usiozingatia maadili ya utumishi wa Umma, Hospitali ya Wilaya ya Magu jijini Mwanza, inatuhumiwa kumuuzia damu, mlemavu wa ngozi (Albino), Selina Magida, mkazi wa Kata ya Kahangara, Kijiji cha Shinembo, Kitongoji cha Deke.
Licha ya huduma hiyo kutolewa bure nchi nzima, Magida ambaye ni mjamzito kwa sasa akiwa amelazwa chumba cha upasuaji, alifikishwa hospitalini hapo Juni 16 mwaka huu, saa moja jioni akiwa hajitambui na baada ya vipimo akaonekana kuwa na upungufu wa damu, ndipo akakumbana na kadhia hiyo ya kutozwa fedha.
Inadaiwa kuwa baada ya kugundulika kuwa na upungufu wa damu, ndugu zake walitakiwa watoe kiasi cha sh. 25,000 ili awekewe damu hiyo kwa maelezo kwamba bila kiasi hicho damu haiwezi kupatikana.
Chanzo chetu ndani ya hospitali ya Magu, kilieleza kuwa baada ya wanandugu kuchangishana, walifanikiwa kufikisha kiasi hicho cha na hatimayeMagida akawekewa damu saa tano usiku.
“Walichangishana huku wakihoji dhana nzima ya kina mama wajawazito kupata huduma bure iko wapi, lakini pia suala la kuuzwa kwa damu limeanza lini wakati kila siku wanahimizwa kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wengine,”kilisema chanzo chetu kikiwanukuu ndugu wa Magida.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ndugu wa Magida waliambiwa kuwa sh. 5,000 ni kwa ajili ya huduma ya maabara na kiasi kilichosalia ni kwa ajili ya damu atakayowekewa mgonjwa.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Magu, Dk. Athuman Pembe, alipoulizwa juu ya ukweli wa tukio hilo, alikataa kuliongelea na kudai mpaka apewe ruhusa na mkurugenzi wa wilaya.
“Sitoi taarifa yoyote mpaka niagizwe na mkurugenzi, hivyo ndivyo ninavyoweza kukuambia, mtafute mkurugenzi,”alisema Dk. Pembe.
Mkurugenzi wa wilaya ya Magu, Naomi Nnko, alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema yupo kwenye kikao na kutaka mwandishi amfikishie taarifa kwa maandishi. Alipoelezwa kuwa suala hilo halihitaji kufikishwa kwa maandishi, Nnko, alisema hana taarifa hizo kisha akakata simu.
Takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai 100,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu.
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment