Tuesday 21 October 2014

TBCF NA MKAKATI WA MAPAMBANO YA KUZUIA SARATANI YA MATITI NA MLANGO WA KIZAZI NCHINI


Takribani watu 40,000 nchini wakiwemo wanawake na wanaume wanapata ugonjwa wa saratani kila mwaka, ambapo asilimia 12 kati yao wana saratani ya matiti huku wengine wakiwa na saratani ya mlango wa kizazi.


Takwimu toka Hospitali ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa hao, idadi ya wanawake wanaopata ugonjwa huo kila mwaka ni zaidi ya 3,000 ambapo idadi hiyo ni sawa na asilimia 10 ya wanaofika kwa ajili ya matibabu hospitalini huku wengi wao wakiwa wamechelewa.
Hivi karibuni Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (TBCF) ilizindua kampeni ya uchangiaji wa fedha kupitia mitandao ya simu za mikononi ikiwa ni jitihada mojawapo ya kusaidia mapambano dhidi ya ueneaji wa magonjwa ya saratani ya matiti na ya mlango wa kizazi.
Katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Jamii imetakiwa kuiunga mkono asasi hiyo kwa kuchangia kiasi cha shilingi 1,000 kupitia mitandao ya simu ikiwemo ya Vodacom (M-PESA namba 110011) na Tigo (TIGO PESA 0658-955-554).
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba alisema kuwa takwimu za kuenea kwa magonjwa hayo nchini ni za kutisha hatua inayotokana na uelewa mdogo wa jamii pamoja na ufinyu wa hospitali za kutosha za kutibu magonjwa hayo.
Mhe. Simba alisema kwamba, kiasi cha fedha zitazokusanywa kutoka kwa wananchi zitatumika katika kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo ya kusomesha wasichana wapatao 12 katika fani ya Onkolojia yenye lengo la kuendesha programu ya upimaji na utoaji wa huduma nchini.
“Tunaomba utoe elfu moja kwa ajili yako wewe mwenyewe, mtolee mwanao, mama yako, dada yako, baba yako, mke wako na jirani, sote tuunganishe nguvu zetu ili kupunguza ukubwa wa mateso wanayoyapata wale wote waliogundulika na matatizo haya.
Asasi hii ilianzishwa na inaendeshwa na wahanga wa saratani, na pia imekuwa inasaidia watu wanaoishi na kutaabika na saratani kwa kuwapatia huduma ya ushauri nasaha, kugharamia matibabu ya upasuaji na madawa ya homoni, kuwapatia matiti bandia na sidiria maalumu baada ya kufanyiwa upasuaji au kuondolewa matiti”, alisisitiza Mhe. Simba.
Mhe. Simba aliongeza kuwa mkakati mwingine wa taasisi hiyo ni wa ujenzi wa majengo maalum ya wagonjwa wa saratani pamoja na ununuzi wa magari yenye vipimo vya digitali vya kupima saratani ya matiti.
Aidha katika kukabiliana na magonjwa hayo aliiasa jamii kuchangia zaidi ya kiwango kilichotajwa kwa kuwa taasisi hiyo ina mipango na mikakati inayopimika na kutimizika, ambapo Serikali kwa upande wake imeweka mazingira mazuri ya uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa hao wa saratani nchini.
“Hawa ni wanawake jasiri waliokuwa wahanga wa saratani ya matiti hivyo ni Majemedari katika kupigana vita kwa niaba ya wenzao, kuonyesha njia ya wapi tuelekeze nguvu zetu dhidi ya saratani na mbinu zipi zitumike katika kuwasaidia wahanga, familia zao na jamii kwa ujumla” alisisitiza Mhe. Simba.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Tiba toka Hospitali ya Saratani ya Ocean Road ambaye pia ni Mshauri wa Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (TBCF) Dkt. Deonista Kombe alisema kuwa Saratani ni chembechembe ambazo si za kawaida kwani zinazozaliana mwilini kwa haraka bila mpangilio maalum.
Dkt. Kombe alibainisha kuwa saratani ya titi ni mabadiliko ya chembechembe ambazo zinaathiri titi na matezi yaliyo karibu na titi, wakati saratani ya mlango wa kizazi ni ukuaji wa chembe hai usio na mpangilio kwenye ngozi laini inayozunguka mlango wa kizazi.
Aidha aliongeza kuwa asilimia 40 ya aina zote za saratani zinatokana na saratani ya shingo ya kizazi huku akifafanua kuwa taasisi hiyo imepanga kufanya matembezi ya hisani .
Akitaja baadhi ya vichocheo vinavyoweza kusababisha magonjwa hayo ya saratani, alisema kwamba unene uliokithiri, matumizi ya kemikali, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, utumiaji wa vyakula vya mafuta kutopata mtoto ndivyo vinapelekea mtu kupata magonjwa hayo.
Asasi hiyo imepanga kufanya matembezi ya hisani tarehe 26 Oktoba mwaka huu ambayo yanatarajiwa kuanzia katika hospitali ya Ocean Road kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa msaada zaidi kwa jamii

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!