Tuesday 21 October 2014

TUEPUKE SIASA KATIKA VITA DHIDI YA EBOLA

Habari za kifo cha mwanamke mmoja aliyedaiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola, ambacho kilitokea wiki iliyopita katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, kimeacha maswali mengi yanayohoji kama kweli wataalamu wetu wa afya wamepewa nafasi stahiki katika vita dhidi ya ugonjwa wa ebola.

Mwili wa mwanamke huyo ulizikwa mwishoni mwa wiki katika makaburi ya misheni mjini Sengerema chini ya uangalizi maalumu.
Kifo cha mwanamke huyo pia kimedhihirisha kuwa, hapa nchini haujawekwa mfumo mzuri wa kutoa habari zinazohusu majanga, ikiwa ni pamoja na ugonjwa huo wa ebola.
Badala yake wananchi wameachwa kuyumbishwa na habari zisizo na uhakika kwamba ugonjwa huo tayari umeingia nchini na kusababisha kifo cha mwanamke huyo. Lakini hata baada ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mmbwambo kukanusha juzi kwamba kifo chake kilitokana na ugonjwa huo, bado habari hizo ziliendelea kuenea kwa kasi kutokana na kauli tata za watu mbalimbali, wakiwamo wanasiasa.
Ni jambo la kushangaza kuwa, wakati uongozi wa hospitali hiyo teule ya Wilaya ya Sengerema ukisubiri majibu ya sampuli ambayo tumeambiwa imepelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, baadhi ya wanasiasa walijipachika jukumu la kuwa wasemaji kuhusu ugonjwa huo. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ilitangaza juzi kwamba ingezungumzia ugonjwa huo jana, huku Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabiani Massawe akipiga marufuku wananchi kushikana mikono kama hadhari ya kuepuka maambukizo ya ugonjwa wa marburg wenye dalili sawa na ebola. Kauli hizo zilizidisha hofu miongoni mwa wananchi, hasa kutokana na taarifa kuhusu ugonjwa wa mwanamke huyo kuanza kukanganya.
Jana kulikuwa na taarifa mbili tofauti kuhusu sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mwanamke ambaye anasadikiwa kufa kwa ebola. Kwanza, kaimu daktari mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alieleza kuwa sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mgonjwa huo zimepelekwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kuzipeleka ama Mbeya ama Nairobi nchini Kenya ili kuthibitisha kama alifariki kwa ugonjwa huo hatari duniani kwa sasa. Pili, msemaji wa Wizara ya Afya naye akatoa taarifa tofauti kuwa kwa sasa Tanzania haina maabara inayoweza kuthibitisha sampuli zilizochukuliwa kama zina virusi vya ebola au la, isipokuwa nchi jirani ya Kenya.
Ukichanganya kauli hiyo na taarifa za wanasiasa kwamba nchi imeshajiandaa kukabiliana na ugonjwa huo ambayo inapingana na kauli ya msemaji wa wizara, ni dhahiri kuwa taarifa hizo tatu tofauti (ya kaimu daktari mkuu wa Mkoa wa Mwanza, msemaji wa Wizara ya Afya na wanasiasa) zinakanganya na kutia hofu wananchi kuwa nchi haijajiandaa barabara kukabiliana na ugonjwa huo. Jambo hili linazua maswali mengi ambayo kama yasipotafutiwa jibu la uhakika, wananchi wanaweza kuamua kutafuta njia zao za kukabiliana na ebola, jambo ambalo litakuwa hatari zaidi. Ni vizuri kwa Serikali kuwa makini na taarifa inazotoa, na pale itakapoona wataalamu wanahitajika ili kutoa taarifa hizo, waachiwe ili waeleze kwa kina nini kimetokea na nini kinatakiwa kifanywe. Kuwa na mfumo mzuri na imara wa utoaji wa taarifa zinazohusu ugonjwa huo, kutasaidia kuwafanya wananchi wajenge imani na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo, ambao siyo tu umetikisa bara la Afrika, bali dunia nzima.
Bahati mbaya bado Serikali imeshindwa kuhakikisha kwamba huduma kama vipimo vya sampuli za magonjwa kama ebola na dengue zinatolewa katika hospitali za mikoa na za rufaa. Haiingii akilini kuona hospitali za wilaya na mikoa zinalazimika kupeleka sampuli hizo Dar es Salaam, huku matokeo yakicheleweshwa kutokana na urasimu uliopo katika makao makuu ya wizara na taasisi zake. Iwapo tunataka kupunguza uzushi, uvumi na habari za mitaani kuhusu masuala nyeti kama magonjwa hatari kama hayo, lazima mamlaka husika zihakikishe huduma kama hizo zinapelekwa angalao kila mkoa.
Hoja tunayojaribu kuijenga hapa ni kwamba wataalamu wa afya wasiingiliwe katika kuongoza vita dhidi ya ugonjwa huo. Kauli za kisiasa kuhusu ugonjwa huo na majanga mengine ya kiafya zinakuza matatizo na kueneza hofu katika jamii. Matokeo yake ni kuwanyanyapaa watu wanaoonyesha dalili za maambukizo, badala ya kuwahudumia na kuwapa matumaini. Serikali itafanya vyema kwa kutambua kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuudhibiti ugonjwa huo unaoendelea kuenea kwa kasi
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!