Thursday 30 October 2014

RAIS JK AGUSWA NA KIFO CHA RAIS WA ZAMBIA




RAIS Jakata Kikwete ameelezea kuguswa, kushtushwa na kusononeshwa na taarifa za kifo cha Rais wa Zambia, Michael Chilufya Sata kilichotokea juzi Jumanne katika Hospitali ya King Edward VII, London, Uingereza, ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 77. Katika salamu zake alizomtumia Makamu wa Rais wa Zambia, Dk Guy Scott kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Kikwete amesema:



“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi, habari za kusikitisha za kifo cha Mheshimiwa Michael Chilufya Sata, Rais wa Jamhuri ya Zambia. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe Mheshimiwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako familia ya wafiwa na ndugu wa Hayati Rais Sata pamoja na Serikali na ndugu zetu wananchi wote wa Zambia kufuatia msiba huu wa ghafla.” Rais Kikwete ameongeza:
“Sata atakumbukwa daima kama mmoja wa viongozi wa mfano wa kuigwa katika Afrika. Katika kipindi chake kifupi cha uongozi wa juu wa Zambia, alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Zambia. Atakumbukwa pia kwa imani yake isiyoyumba ya kupigania uhuru, haki na usawa, sifa ambazo zilimfanya kiongozi mpendwa ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Zambia.
“Hivyo, huyu ni kiongozi ambaye siyo tu atakumbukwa na wananchi wa Zambia, lakini atakumbukwa na sisi sote wenzake na watoto wote wa Afrika.
“Katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na huzuni, tunaungana nanyi kuomboleza na kumwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira wana familia ya wafiwa, jamaa na ndugu zetu wote wa Zambia ili waweze kuhimili machungu ya kipindi hiki cha msiba mkubwa. Aidha, tuko pamoja nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya marehemu Michael Chilufya Sata.”
Kiongozi huyo maarufu kwa jina la utani la 'King Cobra' alikwenda Uingereza Oktoba 19 mwaka huu kutibiwa ugonjwa ambao hadi sasa haujawekwa wazi ingawa kuna madai kuwa, unahusu moyo.
Hali ya afya ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyeanza kuiongoza Zambia Septemba 2011 ilikuwa na utata tangu Juni mwaka huu kwa kutoonekana hadharani bila kuwepo taarifa rasmi ya Serikali, lakini baadaye ilidaiwa kuwa alikwenda Israel kutibiwa.
Mwezi uliopita mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1936 katika mji wa Mpika nchini Zambia alihudhuria ufunguzi wa Bunge la nchi hiyo jijini Lusaka na akasema ‘sijafa’.
Rais Sata hajaonekana hadharani tangu aliporudi Zambia kutoka New York, Marekani, mwishoni mwa Septemba mwaka huu. Kwa mujibu wa Serikali ya Zambia, Rais Sata aliaga dunia Oktoba 28 usiku. Baraza la Mawaziri la Zambia jana lilitarajiwa kuamua nani aiongoze nchi hiyo kabla ya uchaguzi wa Rais mwingine.
“Kwa moyo mzito natangaza kifo cha Rais wetu mpendwa,” Katibu wa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, Roland Msiska alisema jana kupitia televisheni ya Taifa.
“Naomba wote muwe watulivu, wenye umoja na amani wakati huu mgumu,” alisema Msiska na kuongeza kuwa, mke wa Rais Sata, Christine Kaseba, mtoto wao wa kiume na wanafamilia walikuwepo pembeni ya kitanda cha kiongozi huyo wakati anaaga dunia.
Sata amefariki dunia siku chache baada ya Zambia kuadhimisha miaka 50 ya uhuru walioupata kutoka Uingereza. Tangu Sata aende kutibiwa, Katibu Mkuu wa Chama cha Patriotic Front (PF) alichokiongoza mwanasiasa huyo, Edgar Lungu alipewa jukumu la kuwa Kaimu Rais na aliongoza maadhimisho hayo.
Mwanasiasa huyo ni Rais wa pili Zambia kufariki dunia akiwa madarakani, akitanguliwa na Levy Mwanawasa aliyefariki 2008.
Kabla ya kuwa mwanasiasa, Sata aliwahi kuwa Polisi wakati wa utawala wa kikoloni wa Mwingereza, baadaye alijifunza urubani nchini Urusi na amewahi pia kufanya kazi katika shirika la reli. Kabla ya kushinda uchaguzi wa Rais, Sata amewahi pia kuwa kiongozi wa jiji la Lusaka, Mbunge, Waziri wa Serikali za Mitaa, na Waziri wa Afya.
Alijiunga kwenye siasa mwaka 1963 wakati wa mapambano ya kutafuta uhuru kutoka Uingereza, akawa mwanachama wa vyama kadhaa kabla ya kuanzisha chama chake, PF, ambacho awali kilikuwa cha upinzani lakini sasa ndicho kilicho madarakani.
Makamu wa Rais wa Zambia, Guy Scott ni mzungu, wazazi wake wana asili ya Uskochi (Scotland) na hawakuzaliwa Zambia hivyo kwa kuzingatia Katiba ya nchi hiyo, hawezi kugombea urais.
Sata alishinda uchaguzi wa Rais wakati alipogombea kwa mara ya nne, ikiwa ni pamoja na uchaguzi wa mwaka 2001 alipopata chini ya asilimia nne ya kura za urais, mwaka 2006 alipata asilimia 29. Mwaka 2008 alikaribia kumshinda mpinzani wake, Rupiah Banda, ambaye chama chake kilikuwa madarakani kwa miaka 20, na mwaka 2011 alimshinda.
Sata amewahi kuwa mwanachama wa chama cha United National Independence Party (UNIP), kilichokuwa kikiongozwa na Dk Kenneth Kaunda, akahamia chama cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) kilichokuwa chini ya Frederick Chiluba, na alipoona chama hicho kinatishia ndoto zake za kuwa Rais, aliondoka mwaka 2001 akaanzisha chama chake, PF

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!