Thursday 30 October 2014

NSSF KUUNGANISHA DAR-ZANZIBAR KWA DARAJA



BAADA ya ndoto ya kuziunganisha pande mbili za katikati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni kwa daraja lenye umbali wa meta 680, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linaangalia uwezekano wa kujenga daraja la kihistoria zaidi litakalounganisha Dar es Salaam na Zanzibar.



Kwa sasa, uongozi wa shirika hilo upo katika mazungumzo na wataalamu mbalimbali ili kuangalia uwezekano wa kujenga daraja hilo katika bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania Bara na Unguja, kwa upande wa Zanzibar.
Umbali kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni kilometa 73.43, sawa na maili 45.62 hivyo kuwapo kwa mradi huo ni jambo linalowezekana, kwani kuna madaraja marefu zaidi duniani yanayounganisha upande mmoja wa bahari na mwingine.
Kwa sasa, daraja refu kabisa duniani ni lile la Danyang–Kunshan lililopo China ambalo lina umbali wa kilometa 165, sawa na maili 102.4. Daraja hilo lilifunguliwa Juni mwaka 2011.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhan Dau wakati alipokuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda ambaye alitaka kufahamu kama kuna matarajio ya kujenga daraja kubwa zaidi, ikiwezekana la kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Alisema wapo katika mazungumzo na wataalamu mbalimbali ambapo mazungumzo hayo yakienda sawa, ujenzi wa daraja hilo huenda isiwe ndoto, bali ukweli.
"Hilo wazo lipo mheshimiwa na tayari tumeshaanza mazungumzo ya awali, kwa hiyo hilo wazo lipo na sisi tulilifikiria," alisema Dk Dau.
Kamati hiyo ilifanya ziara katika miradi mikubwa mitatu ya shirika hilo ambayo ni daraja la Kigamboni, ujenzi wa nyumba za Mtoni Kijichi na 'Dege Eco village' ambao una nyumba zaidi ya 7,000.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Mtanda alisema, kamati yake imeridhishwa na miradi hiyo ya NSSF ambayo inaendelea huku akitaka kuongezwa kwa kasi ili watanzania waanze kunufaika na miradi hiyo.
"Muangalie na hilo la ujenzi wa daraja la kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na mradi wa makazi bora na salama ambao utaweza kubadili taswira ya Jiji la Dar es salaam," alisema.
Alisema kamati yake isingependa kuona changamoto zozote ambazo zinaweza kukwamisha miradi hiyo na kwamba serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itaangalia namna ya kuunganisha miundombinu karibu na miradi hiyo.
"Lakini pia tumesikia kuwa serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi, tunashauri serikali kuilipa mifuko hii ili kuifanya kuwa na nguvu na kuweza kuleta maendeleo," alisisitiza Mtanda.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!