Friday 17 October 2014

KIKWETE,APONGEZWA UMOJA WA MATAIFA



UMOJA wa Mataifa (UN) umempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kutoa uraia wa Tanzania kwa waliokuwa wakimbizi 162,156 wa Burundi.



Pongezi hizo za UN zimetolewa jana na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, Balozi Said Djinnit wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ikulu Ndogo, mjini Dodoma.
Balozi Djinnit amesema uamuzi huo wa Rais Kikwete kutoa uraia kwa mamia ya wakimbizi hao wa Burundi unathibitisha na kudumisha tunu za kihistoria ya ukarimu za Tanzania ambazo zimethibitisha mara kwa mara tangu Uhuru mwaka 1961. Balozi Djinnit alimwambia Rais Kikwete:
“Nikiwa Mwafrika na Mwakilishi wa Umoja wa Taifa ni jambo la kufurahisha na kutia matumaini sana kuwa Tanzania inaendelea kuwa mfano katika kupokea, kuwatunza na hatimaye kutoa uraia kwa wakimbizi. Ni mwendelezo wa tunu za kudumu za Tanzania.”
Aliongeza Balozi Djinnit, “Uamuzi wako huo Mheshimiwa Rais ambao ni uamuzi wa Tanzania na unakwenda sambamba na tunu za nchi hii ya Tanzania na pia tunu za Umoja wa Afrika (AU).”
Balozi Djinnit pia amempongeza Rais Kikwete na uongozi wote wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la Force Intervention Brigade (FIB) la Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Ushahidi uko wazi kuwa Kikosi cha Tanzania ndicho chenye nguvu kubwa zaidi na mchango mkubwa zaidi katika FIB na tunapongeza na kukushukuru kwa kukubali kutoa askari wa nchi hii kuingia katika FIB.Vijana wanafanya kazi kubwa na nzuri sana,” Balozi Djinnit amemwambia Rais Kikwete.
Aidha, Balozi Djinnit amempongeza Rais Kikwete na Tanzania kwa kukubali kusuluhisha pande zinazopingana ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha Sudanese People’s Liberation Movement (SPLM).
Jitihada hizo za usuluhishi ambazo zinafanywa kichama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza mjini Arusha baada ya maombi ya chama chenyewe cha SPLM yaliyowasilishwa kwa Rais Kikwete na uongozi wa chama hicho.
Rais Kikwete alimwambia Balozi Djinnit kuwa Tanzania imeamua kutoa uraia kwa waliokuwa wakimbizi wa Burundi kwa sababu wametimiza masharti ya kuweza kuwa raia wa Tanzania, ukiwemo ukweli kuwa wakimbizi hao wamekuwa wakiishi Tanzania kwa miaka 42.
Wakati wa utoaji wa Hati za Uraia kwa raia hao wapya wa Tanzania katika sherehe iliyofanyika mjini Tabora juzi Jumanne, Oktoba 14, 2014, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole alisema kuwa uamuzi huo wa Tanzania unaifanya Tanzania kuweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza duniani kutoa uraia kwa kundi kubwa zaidi la wakimbizi na kwa wakati mmoja

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!