Sunday, 21 September 2014

TUUNGANE KWA PAMOJA KUPAMBANA NA UKEKETAJI!



Ukeketaji ni miongoni mwa matatizo yanayoukabili mkoa wa Singida. Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya mwanamke na pia hata ustawi wa watoto wa kike kwa ujumla.

Tatizo jingine linaloambatana na hili ni ndoa za utotoni. Kutokana na uelewa mdogo wa baadhi ya wakazi wa mkoa huu, matendo haya yamekuwa yakishamiri hata kupoteza taswira yake nzuri.
Baada ya kugundua tatizo hili tayari wadau kadhaa wamejitokeza kindakindaki kupambana na mila hizi potofu, lengo kubwa likiwa ni kuufanya mkoa huu kuwa sehemu salama ya kuishi kwa mwanamke na mtoto wa kike kwa ujumla.
Christowaja Mtinda, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) mwenyeji wa mkoa huu ni miongoni mwa wadau hao.
Kwa muda mrefu sasa amekuwa akijishughulisha na mapambano dhidi ya mila potofu mkoani Singida.
Kuna changamoto nyingi za kijamii mkoani Singida zinazowapata wanawake. Ukiachilia mbali mimba za utotoni, suala la ukeketaji limekuwa likisababisha vifo , ikiwa ni matokeo ya kumwagika damu nyingi wakati wa kufanyiwa vitendo hivyo.
Anasema pamoja na hilo pia wanawake wengi wamekuwa wakipata ugumu wakati wa kujifungua jambo linalosababisha kupoteza maisha ya mama na hata watoto.
“Baada ya kugundua matatizo hayo, nimekuwa nikitumia muda mwingi kuhakikisha wanawake wanapata elimu juu ya mapambano dhidi ya matatizo hayo,” anasema.
Anasema kupitia taaluma yake ya ualimu, imekuwa ikimpa urahisi wa kutoa elimu kwa akina mama.
“Katika kila mikutano yangu ninayoifanya na kinamama hata ile inayohusu siasa, huwa natumia muda mwingi kuwaeleza wanawake wenzangu juu ya madhara yanayoweza kupatikana kutokana na athari za ukeketaji,” anasema.
Tatizo jingine linaoukabili mkoa wa Singida, ni tabia ya wasichana wengi, kukimbilia mijini mara tu wanapomaliza shule ya msingi. Huko hujiingiza kwenye kazi za ndani
Anasema katika hilo pia amekuwa akizungumza na wazazi wa watoto na kuwaelewesha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike. Kwani siku zote anaamini kuwa elimu hasa kwa mtoto wa kike ndiyo mkombozi wa familia na jamii kwa ujumla.
Je, mama Mtinda alitokea wapi hasa?
Safari yake ya kufikia hapo alipo ilianzia mbali kidogo, kwani kutokana na taaluma yake ya ualimu aliyonayo, alianza kwanza kufundisha.
Baadhi ya shule alizofundisha ni pamoja na shule ya Sekondaru St. Mary’s 1999 -2000 na shule ya Sekondari Airwing 2000-2001.
Muda mfupi baada ya kufundissha shule hizo, aliamua kurudi chuoni kwa ajili ya kufanya shahada yake ya pili.
Mwaka 2006 akiendelea na masomo yake hayo, alipata ajira serikalini huko aliajiriwa kama Ofisa Mitihani daraja la pili kwenye Baraza la Mitihani la Taifa.
Akiwa kwenye nafasi hiyo, anasema alikuwa akivutiwa sana na siasa, na hivyo akaamua kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mara tu baada ya kumaliza masomo yake, aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Mkwawa Iringa ambapo alifanya kazi kwa muda kabla ya kuchaguliwa kushika nafasi aliyo nayo hivi sasa. Hivi sasa anachukua Shahada ya uzamivu nchini Uingereza.
Mama huyu wa watoto watatu, anasema kama kuna kitu anachopenda ni kuona Tanzania inakuwa na wanawake wasomi, wenye mtazamo wa maendeleo.
“Na hili linawezekana ikiwa tu kila mmoja wetu atawajibika katika nafasi yake. Tuhimizane katika hili, kwani kila mwanamke akihimiza elimu kwa mtoto wa kike, ni wazi kuwa Tanzania, itakuwa nchi ya wasomi” anasema.
“Hivi ni mwanamke gani msomi atakayekubali mtoto wake asiwe na elimu?” Anahoji.
“Ninaahidi kulisimamia hili kwa nguvu zangu zote. Na hakika siku moja tutafanikiwa katika hili”anasisitiza.
Akizungumzia mipango yake ya baadaye anasema kuwa, ni kuhakikisha anasimama katika uchaguzi na kugombea kuchaguliwa jambo analoamini kuwa linawezekana
“Wanawake tunakubalika kwa uwezo wetu. Naamini kutokana na mipango yangu mizuri niliyonayo, nitapata sapoti kubwa kutoka kwa wanawake wenzangu, na hata wanawake wenye uchu na kiu ya maendeleo”.
Kwa upande wa kitaaluma, anasema pia anajipanga kwenda mbele zaidi, baada ya kumaliza shahada yake ya Uzamivu.
Kila siku nimekuwa ninapenda kujifunza vitu vipya. Na hii ndiyo siri iliyonifikisha hapa nilipo. Hivyo wito wangu kwa wanawake wenzangu, nawaomba wasichoke kujifunza kwani elimu haina mwisho.
Kama vile haitoshi, kwa upande wa wanasingida anasema kuwa atahakikisha mila potofu zinakuwa historia. Kwani hadi sasa zinatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya mkoa huo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!