Dunia hivi sasa inatikiswa na taarifa za kisayansi kwamba mojawapo ya dawa ya meno iliyopo kwenye soko ina kemikali aina ya triclosan ambayo ina sababisha ugonjwa wa saratani ambao kisayansi hadi hivi sasa hauna tiba.
Taarifa hizi ni za kushtusha na kuogofya kwa vile dawa hiyo ya meno ipo katika maduka ya rejareja na maduka makubwa hapa nchini. Kwa maneno mengine watanzania nao wako hatarini na tishio hili jipya.
Pamoja na kuwapo kwa taarifa hizo, Tanzania ambayo inaaminika ni jalala la bidhaa kutoka nje haijachukua hatua madhubuti na makini kuhakikisha inawanusuru Watanzania na matumizi ya dawa hiyo ya meno.
Nasema haijachukua hatua madhubuti na makini kwa sababu tangu kubainika kwa taarifa hizo, aina hiyo ya dawa ya meno imeendelea kuuzwa dukani bila hata kuthibitishwa kitaalamu kwamba haina madhara.
Taarifa za kemikali hiyo aina ya triclosan inayohusishwa na ukuaji wa seli za saratani, zimechapishwa kwa kirefu mwezi uliopita katika vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa, likiwamo gazeti dada la Mwananchi la The Citizen la Agosti 14.
Kwa faida ya wasomaji wa makala haya, mwaka 1997 dawa hiyo ilihalalishwa itumike duniani lakini kemikali zilizotumika zikafanywa siri hadi mwanzoni mwa mwaka huu.
Kutokana na sheria ya uhuru wa vyombo vya habari, shirika la habari la Blomberg lilifungua kesi likitaka kemikali zilizotumika kuzalisha dawa hiyo ya meno ziwekwe wazi ili jamii ijue mchanganyiko wake.
Wanasayansi watatu waliopitia ripoti ya Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliyowekwa kwenye mitandao juu ya dawa hiyo, walibaini kuwa wazalishaji hawakuweka wazi kemikali zinazotumika.
Taarifa zinasema wakati FDA ikiidhinisha dawa hiyo, iliegemea kwenye taarifa za kitafiti za wazalishaji wa dawa hiyo badala ya kuwajibika kikamilifu kuifanyia uchunguzi wa kimaabara na kujiridhisha kuwa ni salama.
Leo dunia nzima imetaharuki kwa vile dawa hiyo ndiyo inayoongoza kwa mauzo katika nchi mbalimbali duniani.
Tunapaswa kujiuliza, kama kweli inasababisha saratani, ni Watanzania wangapi wameshaathirika?
Kemikali hiyo ya triclosan inaelezwa kupatikana pia katika baadhi ya sabuni, vipodozi na dawa za kuosha kinywa. Taarifa hizi si za kupewa uzito mdogo na jamii ya Tanzania
Nimesoma kauli ya msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA), Gaudensia Simwanza alipohojiwa na The Citizen akikiri wamepata taarifa zinazodai dawa ina kemikali hiyo yenye madhara.
Simwanza anasema tayari TFDA imeshawaagiza wataalamu wake kuifanyia kazi ripoti hiyo ili kujua hatima ya bidhaa hiyo kwenye soko la Tanzania.
Simwanza alisema kwamba kwa ile iliyoidhinishwa hapa nchini ina asilimia 0.3 ya kemikali hiyo hatari.
Kwa maelezo ya Simwanza, kiwango hicho hakina madhara kwa watumiaji wenye umri wa kati ya miaka 12 na kuendelea lakini swali la kujiuliza, ni Watanzania wangapi wanajua juu ya jambo hilo?
Wazalishaji wa dawa hiyo wanawatoa hofu watumiaji kuwa dawa hiyo ya meno wasihofu kwani hatari ipo tu pale mtu atakapotumia kemikali hiyo kwa wingi.
Swali la kujiuliza, ni wingi upi unaozungumziwa hapa? Tangu mwanzo nilitangulia kusema kuwa nionavyo mimi TFDA bado haijachukua hatua zinazopaswa ili kulinda afya za Watanzania.
Ningekuwa mimi ndio TFDA, ningesimamisha kwa muda matumizi ya dawa hiyo hadi pale uchunguzi utakapokamilika na wataalamu wetu wa afya waishauri Serikali.
Tutapoteza nini kama tutaisimamisha kwa muda wakati wataalamu wa TFDA wakifanyia kazi taarifa hizo kama ambavyo Simwanza anataka Watanzania waamini?
TFDA inapaswa kujua kinga ni bora zaidi kuliko tiba? Sote tunafahamu namna Tanzania ilivyo jalala la bidhaa feki na za kugushi.
TFDA ilipaswa iende mbali zaidi badala ya “kuagiza” tu wataalamu wake waichunguze. Wanapaswa kufahamu watawajibika kwa Mtanzania yeyote atakayeathirika kwa dawa hiyo.
Watapaswa kujibu mbele za Mungu kwa sababu tumewakabidhi mamlaka zote za kushughulikia bidhaa za ina hii.
Kama waliweza kuzuia matumizi ya maziwa ya watoto, kwanini wasizuie dawa hiyo kwa muda tukisubiri uchunguzi?
Ni bora tukajiridhisha kwanza juu ya taarifa hizi vinginevyo tujue majuto ni mjukuu!.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment