Sunday, 21 September 2014

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA MBALIMBALI AMBAZO SERIKALI INAENDELEA KUCHUKUA KUFUATIA TISHIO LA UGONJWA WA EBOLA NCHI ZA AFRIKA MAGHARIBI NA KATI.



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA MBALIMBALI AMBAZO SERIKALI INAENDELEA KUCHUKUA KUFUATIA 
TISHIO LA UGONJWA WA EBOLA NCHI ZA AFRIKA MAGHARIBI NA KATI

Mnamo mwezi wa Machi 2014, Serikali ilipokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea katika nchi za Afrika Magharibi. Ugonjwa huu ulianzia katika Nchi ya Guinea na kusambaa katika nchi za Liberia, Siera Leone na Nigeria. Aidha Ugonjwa huu umeshatolewa tarifa pia nchini Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hadi kufikia tarehe 18 Septemba 2014, dadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huu imefikia 5335 na vifo 2662 (CFR=48.9%). 
Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Septemba 2014, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) idadi ya wagonjwa imefikia 71 na vifo 40.
Hali hii imepelekea Shirika la Afya Duniani (WHO) kuutangaza ugonjwa wa Ebola kuwa janga la Dunia (Public Health Emegency of International Concern).
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola. Virusi hivi vipo katika kundi la Familia ya “Filovirus”. Kuna aina tano (5) za “species” za virusi hivi yaani Bundibugyo, Côte d’Ivoire, Reston, Sudan na Zaïre. Aidha inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 90 ya waliopata maambukizo ya ugonjwa huu, hufariki dunia. Mlipuko uilotokea nchi za Afrika Magharibi umesababishwa na kirusi aina ya Zaire Kwa kawaida virusi hivi hubebwa na popo na uambukizo wa kwanza kabla ya kuenea kwa binadamu huanzia kwa wanyama hususan nyani na sokwe. 
Binadamu hupata uambukizo kupitia popo au kupitia wanyama (sokwe, nyani na swala wa porini) ambao wameambukizwa au waliokufa wakati wa shghuli za uwindaji. Mara binadamu anapopata uambukizo huu, anaweza kueneza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia njia zifuatazo;
kugusa damu au majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo
kugusa maiti ya mtu au mzoga wa mnyama aliyekufa kutokana na ugonjwa huu.
Dalili za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa damu ndani na nje ya mwili. Kipindi kati ya kupata maambukizi mpaka kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 21. Ugonjwa wa Ebola hauna Tiba maalum wala chanjo. Hata hivyo mgonjwa anatibiwa kutegemeana na dalili atakazokuwa nazo.
Hadi sasa hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hapa nchini. Kumekuwa na tetesi za wagonjwa wanne (4) kutoka mkoa wa Dar es salaam (2), mmoja (Nkasi) na mmoja (Geita) waliohisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola, lakini vipimo vimethibitisha kuwa HAWANA UGONJWA HUO. Kwa kuwa magonjwa hayatambui mipaka ya nchi, Serikali inaendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya Ugonjwa huu.
Hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na;
Uratibu: Uratibu wa shughuli unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu –Kitengo cha Maafa. Aidha sekta ya afya ndio msimamizi wa wa ugonjwa huu kwa kuwa maambukizi yako kwa binadamu. Kikosi kazi hukutana kila wiki siku ya alhamisi kufanya tathmini ya hali ya ugonjwa katika nchi zilizoathirika pamoja na mikakati iliyowekwa kitaifa. Vikao hivi vinasimamiwa na viongozi wa ngazi za Juu ikiwemo mawaziri na vinajumuisha sekta mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo. Mpango kazi umeendelea kuboreshwa kufuatia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani na kusambazwa mikoani na wilayani. AIdha kiasi cha Tshs500,000,000 zimeshapokelewa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na zinategemea kutekeleza yafuatayo;
Uimarishaji wa sehemu ya kuwahudumia wagonjwa kwa mkoa wa Dar es salaam “Isolation Unit” iliyopo katika eneo la hospital ya Temeke
Uendelezaji wa usambazaji wa elimu, tarifa na habari kwa jamii kutumia mabango, vipeperushi, radio, runinga, na meseji kwa njia ya simu 
Ununuaji wa vifaa cha kupimia joto (Thermoscanners) kwenye maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege
Mafunzo kwa watumishi wa afya
Katika uratibu vilevile, mnamo tarehe 9 Septemba 2014, Mheshimiwa Rais, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete alishiriki katika ukaguzi wa hatua zilizofanyika na kufanya majadiliano na kikosi kazi ya namna ya kuboresha baadhi ya mikakati iliyowekwa. 
Aidha viongozi wa juu wa Serikali wakiwemo makatibu wakuu na mawaziri wamekuwa wanahudhuria mikutano mbalimbali ya kanda (Regional body meetings) kama mikutano ya “Africa Union”, “SADC” na “EAC” ikiwa ni katika kupanga na kuweka maazimio ya pamoja kudhibiti ugonjwa huu barani Afrika
Kuimarisha ufuatitiaji katika viwanja vya ndege na mipakani: Serikali imeshaweka vifaa vya kuchunguza wageni wanaoingia nchini “Walk through Thermoscanners” kwenye viwanja vya ndege na mikapani kama uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, KIA, Mbeya, na Mwanza, na mipaka ya Namanga, Kabanga na Zanzibar. Aidha katika maeneo ya mipaka ya Holili, Sirari, Kasumulo, Mutukula na Pemba pia zimewekwa “Hand Thermoscanners”. Vifaa hivi si kwa ajili ya kutambua iwapo mgonjwa ana ugonjwa wa Ebola bali vinalenga kurahisisha utambuzi wa wasafiri watakaokuwa wanarudi na kuwa na dalili za mwanzo ambayo ni Homa. Fomu maalum za kuhoji wasafiri zinaendelea kutumika kwa wasafiri wanaobainika kuwa na ugonjwa huu. Orodha ya abiria kwenye ndege (Passenger manifest) pia inaendelea kutumika ikishirikisha maafisa wa Uhamiaji lengo likiwa ni kutambua kwa urahisi wasafiri ambao wamepitia nchi zilizoathirika. Ili wasafiri waweze kutambua kuwa kutakuwa na utarabu tajwa, mabango ya maelekezo yameandaliwa kuwekwa kwenye maeneo ya kuwasili (Arrival) na kutokea (Departure). 
Utoaji wa Elimu, Taarifa na Habari kwa jamii: Serikali imeendelea kutoa elimu kupitia njia nyingine zaidi ya redio na runinga. Aidha waandishi wa Habari walipewa semina kuhusu ugonjwa wa Ebola.. Vilevile, Asasi ya TAYOA imekubali kuchangia utumiaji wa mpango wa “toll free numbers” ambazo tayari zinatumika kwa ugonjwa wa UKIMWI na zitaanza kutumika pia kwa ugonjwa wa Ebola ili jamii iweze kupata ufafanuzi zaidi ya ugonjwa huu pindi itakapohitajika. Namba hiyo ya “Toll free number” ni 117 na itaanza kutumika punde kuanzia saa sita mchana na saa sita usiku kupata taarifa za ugonjwa wa Ebola.
Ufuatiliaji wa magonjwa katika vituo vya afya: Kupitia ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Serikali imetoa maagizo kwa Makatibu Tawala na Waganga wakuu wa mikoa wakati wa mkutano wa Waganga wakuu Septemba 2014, kuandaa mpango kazi wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu na kuandaa sehemu ya kutolea matibabu kwa wagonjwa watakaohisiwa kuwa na ugonjwa huu (Isolation Units). Kikosi kazi kitafanya ufuatiliaji wa karibu wa Agizo katika mikoa na wilaya. 
Mafunzo kwa watumishi wa Afya: Mafunzo yameendelea kutolewa kwa watumishi wa viwanja vya ndege, mipakani na vituo vya kutoa huduma za afya pamoja na Maafisa wa Idara ya Uhamiaji yalifanyika Agosti 2014 kwa kushirikiana na ufadhili wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Idadi ya watumishi waliokwisha kupata mafunzo ni;
100 kutoka Dar es salaam
45 kutoka mkoani Arusha, Kagera, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, na Kigoma na Zanzibar
Wizara pia imepata nafasi ya kupeleka watumishi watatu (3) nchini Congo Brazaville; watano (5) nchini Afrika kusini na wanne (4) nchini Uganda kwa lengo la kujifunza kutoka nchi nyingine na pia kuboresha mpango mkakati ambao umeshaandaliwa. 
Wizara kwa kushirikana na TAMISEMI inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu.
Vifaa vya kujikinga (Personal Protective Gears): Vifaa kinga vipo vya kutosha kwa ajili ya matumizi kwa watoa huduma kwa wagonjwa. Jumla ya vifaa vya kujikinga (Personal Protective Gears) 12,750 vimenunuliwa na kuanza kusambazwa katika hospital za wilaya, mkoa na rufaa. Tunatarajia kupata vifaa vingine kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirka la Afya la Marekani (CDC). Aidha idadi hii itaongezwa kadiri ya mahitaji yatakavyojitokeza.
Maeneo ya kutolea huduma za afya kwa watakaobanika na ugonjwa: Wizara imebainisha vituo vya kutolea huduma kwa mikoa yote endapo ugonjwa huu utatokea hapa nchini.. Katika mkoa wa Dar es salaam, Temeke Isolation Unit limetengwa kama eneo la kuwahudumia wagonjwa wa Ebola kwa mkoa huu. Sehemu hii inaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo maalum ili iweze kukidhi matibabu ya Ugonjwa huu. Aidha SUMA JKT wamepewa kazi ya ukarabati wa majengo na kazi hii imeshaanza kufanyika. 
Kuweka mkakati wa namna ugonjwa huu utakavyoweza kutambulika mapema: Mipango ya awali ni kutumia maabara ya KEMRI, Nairobi kwa sasa wakati uboreshaji wa maabara zetu unaendelea ili kupata ithibati na kuweza kufanya utambuzi hapa nchini.
Wizara inaendelea kuwasiliana na wadau mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo ili kuweza kupata msaada wa mahitaji mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye mpango wa dharura wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. Aidha mkutano wa pamoja wa wadau unaandaliwa mwezi Septemba 2014 ambapo utasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu..
Kupeleka wataalamu wa afya katika nchi zilizoathirika. Serikali itapeleka wataalam 9 katika nchi zilizoathirika ikiwa ni kwa ajili ya kujenga uwezo wa wataalam wetu hapa nchini. . Aidha upelekaji wa wataalam hawa unalenga pia kuimarisha dhana ya kusaidiana kama ambavyo Baba wa Taifa alivyokuwa anafanya miaka ya nyuma wakati wa kudai uhuru katika Bara la Afrika. 
Hitimisho
Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa Ebola hapa nchini. 
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari. Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni:-
Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola Kuhakikisha kuwa unanawa mikono kwa maji na sabuni au kwa kutumia kwa dawa ya kuua vijidudu (hand sanitizers) 
Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Wizara itaendelea na utaratibu wa kupashana habari na taarifa hizi kila wiki kuanzia leo tarehe 18.9.2014 ikiwa ni lengo la kushirikisha jamii ili iweze kushiriki katka utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini.
Imetolewa na 
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Tarehe 18 Septemba 2014.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!